Uchaguzi Marekani: Donald Trump Trump 'hayuko tayari' kuachilia mamlaka kwa amani

Rais Donald trump wa Marekani

Rais wa Marekani Donald Trump amekataa kujitolea kupokezana madaraka kwa amani akishindwa katika uchaguzi mkuu wa Novemba.

"Tutaona kitakachofanyika," rais alisema akizungumza na wanahabari katika Ikulu ya White House. "Mnajua hilo."

Bw.Trump pia alisema anaamini matokeo ya uchaguzi huenda yakaamuliwa katika mahakama ya Juu zaidi, akielezea kwa mara nyingine tena mashaka yake kuhusu upigaji kura kwa njia ya posta.

Majimbo zaidi yanatoa wito wa upigaji kura kwa njia ya posta, yakisisitiza umuhimu wa wapiga kura kuwa salama dhidi ya maambukizi ya corona.

Trump alisema nini?

Bwana Trump aliulizwa na wanahabari Jumatano usiku kama atajitolea kukubali matokeo ya uchaguzi "akishinda, kupoteza au kutoka sare" dhidi ya mgombea wa Democrat Joe Biden.

''Napinga vikali upigaji kura kwa njia ya posta ," Bw.Trump, wa Republican, alisema. "Na upigaji kura wa namna hiyo ni majanga."Mwanahabari alipo mkatiza na kumwambia kwamba "watu wanaandamana", Bw. Trump alijibu: "Futilieni mbali uchaguzi, na kutakuwa - na amani - hakutakuwa na suala la kupokezana madaraka, kwa kweli, kutakuwa na muendelezo."

Mwaka 2016, Bw. Trump pia alikataa kujitolea kukubali matokeo ya uchaguzi katika kinyang'anyiro kati yake na mgombea wa Democratic , Hillary Clinton, hatua ambayo alitaja kama shambulio dhidi ya demokrasia ya Marekani.

Hatimaye alitangazwa kuwa mshindi, licha ya kuwa hakupata kura za wengi ambazo pia bado anatilia shaka.

Democrats wamesema nini?

Mwezi uliopita, Clinton alimuomba Bw. Biden mara hii asikubali kushindwa "katika mazingira yoyote" katika mbio za mwisho usiku wa uchaguzi.

Alielezea hali ambapo Warepublican wangelijaribu "kuwatumia ujumbe wapigaji kura ambao hawajapiga kura" na kutumia kundi la mawakili kupinga matokeo ya uchaguzi.

Wahafidhina wamemlaumu Bw. Biden kwa kuchochea vurugu katika uchaguzi aliposema mwezi Augosti: "Kuna mtu anaamini hakutakuwa na vurugu nchini Marekani ikiwa Donald Trump atachaguliwa?"

Trump amesema nini kuhusu Mahakama ya Juu zaidi?

Awali siku ya Jumatano, Rais wa Marekani alitetea uamuzi wake wa kumtafuta Jaji wa Mahakama ya Juu zaidi kabla ya uchaguzi kujaza nafasi ilioachwa wazi na marehemu Ruth Bader Ginsburg, akisema kuwa anatarajia matokeo ya uchaguzi yakifikishwa mbele ya mahakama hiyo.

"Nafikiria [uchaguzi] utaishia Mahakama ya Juu zaidi, nadhani ni muhimu tuwe na majaji tisa," rais alisema.

"Nadhani ni vyema tukienda kwa uchaguzi, kwa sababu nafikiria hii ni njama inayochezwa na Democrats, na njama hiyo itafikishwa mbele ya Mahakama ya Juu Zaidi ya Marekani."

Trump alikuwa anaashiria kwa mara nyingine madai yake yaliozua utata kwamba kura inayopigwa kupitia mfumo wa posta inaweza kuibiwa.

Rais amesema atamteua jaji wa kike kuongoza mahakama hiyo Jumamosi hii. Atachukua nafasi ya Jaji Ginsburg, aliyefariki Ijumaa iliyopita.

Wafuasi wa Bw.Trump, wanaamini mteuzi wake akiidhinishwa na Bunge la Seneti, atadumisha takwimu ya 6-3 ya Wahafidhina kuongoza mahakama hiyo ya juu zaidi katika siku zijazo.

Kura inayopigwa kwa posta inaweza kuibiwa?

Idadi ya kura zitakazopigwa kupitia njia ya posta zinatarajiwa kuongezeka katika uchaguzi huu kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini Ellen Weintraub, kamishena wa Tume ya Uchaguzi, amesema: "Hakuna msingi wowote wa kufanyika kwa udanganyifu ama njama ya kuiba kura"

Kumekuwa na visa vichache vya udanganyifu katika mfumo wa upigaji kura kwa njia ya posta, kwa mfano katika uchaguzi wa mchujo wa mwaka 2018 North Carolina, ambapo uchaguzi ulirudiwa tena baada ya kubainika mgombea wa Republican aliingilia mchakato wa upigaji kura.

Pia kulikuwa ma kisa kingine mwaka huu New Jersey ambapo madiwani wawili wa Democratic walishitakiwa kwa kuhusika na udanganyifu uliohusisha upigaji kura kupitia posta.

Lakini kiwango cha udanganyifu katika mchakato wa uchaguzi wa Marekani uko chini sana kati ya asilimia 0.00004 na 0.0009, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2017 uliofanywa na Kituo cha Haki cha Brennan.