Grace Omutoni: WhatsApp yamuunganisha 'kimiujiza' yatima wa mauaji ya kimbari na familia yake Rwanda

Je unanifahamu? Grace Omutoni alichapisha picha hizi zake katia mtandao wa kijamii

Chanzo cha picha, GRACE UMUTONI

Maelezo ya picha,

Je unanifahamu? Grace Omutoni alichapisha picha hizi zake katia mtandao wa kijamii

Msichana aliyekuwa yatima akiwa na umri wa miaka miwili wakati wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994 hivi karibuni amepatana na jamaa zake kupitia "miujiza" ya mtandao wa kijamii.

Grace Umutoni, ambaye hakujua jina lake la kuzaliwa, aliweka picha zake kadhaa katika makundi ya WhatsApp, Facebook na Twitter mwezi Aprili kuona kama zinaweza kumsaidia kutafuta watu wa familia yake - baada ya kushindwa katika juhudi za kuwatafuta kupitia njia rasmi.

Kile anachofahamu muuguzi huyo mwenye umri wa miaka 28 - kuhusu maisha yake ni kwamba alilelewa katika makazi ya watoto yatima katika mji mkuu wa Kigali, mtaa wa Nyamirambo akiwa na ndugu yake wa kiume aliyekuwa na miaka minne wakati huo na ambaye baadae alifariki dunia.

Kuna maelfu ya watoto kama Bi Utomoni, ambao waliwapoteza ama kutenganishwa na wazazi wao wakati wa ghasia zilizogeuka mauaji ya kimbari na kusababisha kuuawa kwa zaidi ya watu 800,000 kutoka jamii ya Tutsi na Wahutu waliokuwa na msimamo wa kadri ndani ya siku 100.

Baadhi yao bado wanawatafuta jamaa zao - hali ambayo wakati mwingine huwa vigumu kwa sababu kitamaduni familia hazitumii jina moja.

Baada ya kuweka picha zake mtandaoni, watu wachache walidai kuwa jamaa zake - lakini miezi kadhaa baadae kuna mtu aliyemfanya awe na hisia kwamba bila shaka ni mtu wa familia yake.

Antoine Rugagi baada ya kuona picha yake kwenye kundi la WhatsApp aliwasiliana naye na kumwambia anafanana sana na dada yake anayeitwa Liliose Kamukama, ambaye aliuawa siku za kwanza za mauaji ya kimbari ya Aprili 1994.

'Miujiza nilioomba'

"Nilipomuona, niliona jinsi tulivyofanana," Bi Umutoni aliambia BBC Idhaa ya Great Lakes kumhusu mtu huyo ambaye huenda ni mjomba yake.

"Lakini ni uchunguzi wa chembechembe za vinasaba vya (DNA) ndio ambao utathibitisha ikiwa tuna uhusiano. Kwa hivyo tulienda kufanya uchunguzi huo Kigali mwezi Julai."

Bi Umutoni alisafiri kutoka kusini mwa wilaya ya Gakenke ambako anafanya kazi naye Bwana Rugagi alikuja kutoka nyumbani kwake Gisenyi eneo la magharibi kuja kuchukua matokeo ya DNA pamoja.

Chanzo cha picha, GRACE UMUTONI

Maelezo ya picha,

Grace Umutoni na Antoine Rugagi walisafiri hadi mjini Kigali kupata matokeo ya chembechembe za DNA

Ilikuwa siku kubwa sana kwao kwa sababu matokeo yalionesha kuwa asilimia 82 huenda wanahusiana.

"Nilishtuka sana, sikuamini kilichotokea na mpaka leo inanikalia kama ndoto, ni miujiza niliyokuwa nikiomba," anasema Umutoni.

Mjomba wake waliyepatana upya alimwambia jina lake alilopewa na wazazi wake Watutsi lilikuwa Yvette Mumporeze.

Pia alimkutanisha na familia yake upande wa baba.

Miongoni mwao Shangazi yake Marie Josée Tanner Bucura, ambaye amekwama Switzerland kwa miezi kadhaa kutokana na janga la virusi vya corona.

Chanzo cha picha, GRACE UMUTONI

Maelezo ya picha,

Grace Umutoni kushoto na picha ya mamake Liliose kamukama kulia kutoka kwa picha ya familia iliopigwa zamani

Hata kabla ya matokeo ya uchunguzi wa DNA kutolewa, alikuwa na uhakika Grace Umutoni ni mtoto wa kaka yake kwa kumlinganisha na picha katika albamu ya zamani ya familia.

"Msichana huyu bila shaka ni binti ya kaka yangu Aprice Jean Marie Vianney na mke wake Liliose Kamukama. Wote wawili waliuawa katika mauaji ya kimbari."

'Tulidhani hakuna aliyenusurika'

Bi Bucura pia alimwambia jina la ndugu yake aliyempeleka katika makazi ya watoto yatima ni Yves Mucyo - alikumbuka jina la kwanza tu - ambaye pia alikuwa na ndugu mmoja wa kiume kwa jina Fabrice.

Mauaji ya kimbari yalianza baada ya ndege iliyokuwa imewabeba marais wa Rwanda na Burundi - wote kutoka jamii ya Hutu - kudunguliwa usiku wa Aprili tarehe sita 1994, mauaji yakaanza siku iliyofuata.

Wanamgambo wa Kihutu waliambiwa kuwasaka na kuwaangamiza watu kutoka jamii ya Watutsi walio wachache - mtaa wa Nyamirambo viungani mwa Kigali ukiwa moja ya maeneo yaliyolengwa kwanza.

Watu waliuawa kwa kukatwa mapanga majumbani mwao au katika vizuizi vya barabarani vilivyowekwa kuwakagua wale waliokuwa wakitoroka - baadhi yao walifanikiwa kukimbilia maeneo salama Kanisani na Misikitini ghasia za Nyamirambo zilipozidi.

Bi Bucura anasema kuna mtu alimuona mwanamke akimshika mkono Yves na kutoroka naye - lakini hakufanikiwa kupata taarifa zozote kumhusu. Hakuna kilichojulikana kumhusu dada yake.

Mauaji ya kimbari yalimalizika July 1994 baada ya waasi wa kundi la Tutsi, Rwandan Patriotic Front (RPF) wakiongozwa na Rais Paul Kagame, kuchukua madaraka.

"Tulidhani hakuna mtu aliyenusurika, na tumekuwa tukiwaomboleza kila mwezi April wakati wa ukumbusho wa mauaji ya kimbari," Bi Bucura alielezea.

PICHA.....MAP

Alipokuwa akikuwa, Bi. Umutoni hakuweza kupata maelezo zaidi kuhusu familia yake kwasababu Yves alifariki muda mfupi baada ya kufika katika makazi ya watoto yatima.

Aliambiwa alifariki kutokana na majeraha ya risasi aliyopata akitoroka mashambulio ya waasi wa Kihutu.

Akiwa na miaka minne alisaidiwa na kulelewa na familia moja ya Tutsi kusini mwa nchi, ambayo ilimpatia jina la Grace Umutoni.

'Niliishi kwa majonzi'

"Akiwa shule ya upili maafisa walimsaidia kurudi katika makazi ya mayatima mjini Kigali kuulizia kama kuna maelezo yoyote kuhusu alikotoka, lakini hakufanikiwa," anasema.

"Nimekuwa nikiishi kwa majozsi kwa kuwa mtu asiyekuwa na jamaa zake, lakini niliendelea kuomba Mungu nipate muujiza.

"Japo wazazi wangu wa kunilea walinitunza vizuri, sikuweza kamwe kuwafikiria wazazi wangu halisi. Nilichokifahamu kuhusu jamaa zangu ni jina la Yves na Nyamirambo -maelezo kidogo sana kuanza kufanya uchunguzi."

Anasubiri kwa hamu kujua mengi kuhusu wazazi wake - na hafla itakayozikutanisha familia inayopangwa nchini Rwanda na kwengineko, japo janga la corona limechelewesha mpango huo.

Kwa sasa, amekuwa akitambulishwa kwa familia yake kupitia WhatsApp - na sasa amegundua kuwa ana ndugu wa kambo anayeishi Kigali.

Baba yake alimzaa alipokuwa kwenye mahusiano kabla ya ndoa.