Vikosi vya Korea Kaskazini vyamuua mtu mmoja kuzuia maambukizi ya Covid-19 kuingia nchini mwao

Unidentified fishing boats before the North Korean coastline from a viewpoint on the South Korea-controlled island of Yeonpyeong near the disputed waters of the Yellow Sea at dawn.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Kisiwa cha Korea Kusini cha Yeonpyeong kiko karibu na mpaka wa Korea Kaskazini

Afisa mmoja wa Korea kusini ameuawa kwa risasi na kuchomwa moto na vikosi vya Korea Kaskazini, wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imeeleza, ikisema ''kitendo hicho ni cha kikatili''.

Seoul imesema kuwa mtu huyo aliyekuwa akifanya kazi na idara ya uvuvi, alitoweka kutoka kwenye boti ya doria karibu na mpaka na baadae alipatikana kwenye maji ya Korea Kaskazini.

Wanajeshi wa Korea Kaskazini walimpiga risasi, kisha kummwagia mafuta mwili mzima na kumchoma moto, wizara imesema. Iliamini kuwa ni hatua ya kudhibiti virusi vya corona.

Pyongyang haijasema chochote kuhusu tukio hilo.

Mpaka kati ya pande hizo mbili za Korea una ulinzi mkali na Kaskazini inadhaniwa kuwa na sera ya ''kupiga risasi hadi kifo'' kuzuia virusi vya Covid-19 kuingia nchini humo.

Tukio hilo litakuwa la pili kwa vikosi vya Korea Kaskazini kuua raia wa Korea Kusini. Mwezi Julai mwaka 2008, mtalii aliuawa na mwanajeshi katika eneo la mlima Kumgang.

Korea Kusini imesema nini?

Afisa huyo alikuwa kwenye doria yapata umbali wa kilomita 10 kutoka eneo la mpaka na Kaskazini, karibu na kisiwa cha Yeonpyeong, alipitoweka siku ya Jumatatu, wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imeeleza.

Afisa huyo, 45 ambaye ni baba wa watoto wawili aliacha viatu vyake kwenye boti.

Boti ya doria ya Korea Kaskazini ilimpata mtu huyo, aliyekuwa amevaa jaketi la kujiokolea, kwenye bahari hiyo majira ya saa tisa saa za huko siku ya Jumanne, Seoul iliongeza.

Waliweka maski zenye gesi na kumuuliza maswali akiwa mbali kabla ''amri kutoka kwa mamlaka ya juu'' kuwa auawe. Alipigwa risasi majini.

Kisha vikosi vya Korea Kaskazini vilichoma mwili wake baharini, maafisa wa wizara ya ulinzi Korea Kusini walieleza, wakiongeza kuwa wanaamini kuwa hii ni hatua ya kupambana na virusi vya corona.

Tukio hilo linazungumziwaje?

Rais Moon Jae-in ameeleza kuwa tukio hilo la mauaji ''linashtusha'' na kuwa haliwezi kuvumiliwa.

Ametaka Korea Kaskazini kuchukua hatua ya''kuwajibika'' kutokana na shambulio hilo.

Baraza la usalama la taifa limesema kuwa Kaskazini ''haiwezi kuhalalisha tukio la kushambulia kwa risasi na kuchoma mwili wa mtu ambaye hakuwa amejihami au kuonesha dalili ya ukaidi''.

''Hatua hii ya kijeshi ni ukiukaji wa kanuni za kimataifa,'' alisema Katibu Mkuu wa baraza la usalama Suh-Choo-suk. ''Tutalipa kila tukio litakalofanywa na Korea Kaskazini ambalo linatishia maisha na usalama wa watu wetu.''

Katika mkutano na wanahabari awali, wizara ya ulinzi ilisema ''inalaani vikali kitendo hicho cha kikatili na kuitaka Kaskazini kutoa maelezo na kuwawajibisha waliohusika.''

Maafisa walisema wamefanya ''tathimini ya kina ya kiintelijensia'' lakini haijawa wazi ni kwa namna gani waliweza kukusanya taarifa.

Nambari ya simu ya kijeshi kati ya Kaskazini na Kusini ilikatwa mnamo Juni, na ofisi ya uhusiano kati ya pande hizo mbili, ambayo ilijengwa kusaidia pande zote mbili kuwasiliana, iliharibiwa na Korea Kaskazini. Lakini jeshi la Korea Kusini linadaiwa kuingilia mawasiliano ya redio ya Kaskazini, shirika la habari la AFP limeripoti.

Ilikuwaje hapo awali?

Maafisa wa Korea Kaskazini labda wanaweza kuwa wanafanya kila kitu kuhakikisha kuwa nchi hiyo haiathiriki na virusi vya corona, Mwandishi wa BBC, mjini Seoul Laura Bicker anaripoti.

Mamlaka zinadaiwa kujiandaa kwa gwaride tarehe 10 mwezi Oktoba kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 75 ya kuanzishwa kwa chama tawala nchini Korea Kaskazini.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Korea Kaskazini imekuwa mpakani na China

Pyongyang ilifunga mpaka wake na China mwezi Januari kujaribu kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Mwezi Julai, vyombo vya habari vilisema kuwa nchi hiyo imetangaza hali ya dharura ya hali ya juu.

Mwezi uliopita, kamanda wa kikosi cha jeshi la Marekani nchini Korea Kusini, Robert Abrams, alisema kuwa Kaskazini imeanzisha eneo jipya la umbali wa kilomita moja au mbili katika eneo la mpaka na China, na kuwa nchi hiyo ilikuwa na vikosi vya operesheni maalumu wakiwa wameamriwa ''kuua kwa risasi'' mtu yoyote atakayevuka mpaka.

Wakati mmoja, Korea Kaskazini pia ilirudisha watu ambao walikuwa wakitangatanga katika eneo lao.

Mnamo mwaka wa 2017, shirika la habari la nchini humo KCNA lilisema maafisa wangerejesha mashua ya uvuvi ya Korea Kusini ambayo "ilivuka mipaka" kinyume cha sheria.

Lakini Korea Kaskazini imekuwa ikijulikana zaidi kwa kutoa adhabu kali kwa kuvunja sheria.

Nchi hiyo imekuwa ikitekeleza adhabu ya kifo mbele ya umma.