Mwanaume afariki dunia kwa kula pipi zilizotengenezwa kwa pombe zaidi ya mfuko mmoja kwa siku

Stock photo of liquorice

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Utafiti unaonesha kula pipi nyingi za susu zilizotengenezwa kwa pombe kunaweza kusababisha kiwango cha potasiamu kuwa chini zaidi kiasi cha kusabbaisha hatari

Mfanyakazi wa ujenzi Marekani huko Massachusetts amefariki dunia kwa kula susu (pipi zinazojivuta zilizotengenezwa kwa pombe maarufu kama liquorice), daktari amesema.

Mwanaume huyo ambaye hakutajwa jina lake alikuwa na umri wa miaka 54, alikula mfuko mmoja unusu wa pipi hizo nyeusi kila siku.

Kabla ya kupata mshutuko wa moyo hakuwa ameonesha dalili zozote za kuugua alipokuwa kwenye mgahawa wa kuuza chakula.

Akielezea kisa cha mwaume huyo, Jarida la Tiba la Uingereza, limesema daktari wake alisema asidi ya glycyrrhizic iliyopo kwenye pipi hizo ndio chanzo cha kifo chake.

"Tumearifiwa kwamba mgonjwa huyo hakuwa anapata lishe inayofaa na alikuwa anakula pipi nyingi. Je ugonjwa wake unaweza kuwa na uhusiano na ulaji wa pipi au peremende kwa kiasi kikubwa?" Dkt Elazer R Edelman amesema.

Alisema utafiti uliofanywa unaonesha kwamba asidi ya glycyrrhizic kiungo muhimu katika utengenezaji wa pipi hizo inasababisha shinikizo la juu la damu, kiwango cha chini cha potasiamu, mabadiliko makubwa ya mapigo ya moyo yenye uwezo wa kusababisha kifo na kushindwa kwenda haja ndogo" ambayo yote hubainika kwa mgonjwa.

Ugonjwa wa Hypokalemia ni pale kiwango cha madini ya potasiamu kinapokuwa chini zaidi na kuhatarisha maisha yake.

Mgonjwa huyo alikuwa amebadilisha aina ya pipi anazokula. Wiki kadhaa kabla ya kifo chake, alikuwa amebadilisha kutoka aina ya pipi nyekundu hadi nyeusi hizi zinazotengenezwa kwa pombe.

Aidha, daktari mwingine katika ripoti hiyo, Dkt. Andrew L Lundquist, alisema pipi hizo ndio chanzo cha kifo chake.

Aliandika: "Utafiti zaidi ulibaini kwamba hatua ya mgonjwa aliyekufa kubadilisha pipi alizokuwa anakula hadi hizi zilizotengenezwa kwa pombe kuwa na uwezekano mkubwa wa kusababisha kiwango cha chini cha potasiamu."