Felicien Kabuga: Mawakili wake wanataka mteja wao kushtakiwa the Hague na sio Tanzania

Felicien Kabuga

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Felicien Kabuga

Wakili wa Felicien Kabuga amesema kwamba watawasilisha ombi la mteja wao kupelekwa katika mahakama ya kimataifa kuhusu uhalifu wa kivita ICC mjini The Hague, baada ya mahakama kuu ya Ufaransa siku ya Jumatano kuunga mkono uamuzi wa mshukiwa huyo kushtakiwa nchini Tanzania.

Emmanuel Altit ambaye anaongoza mawakili wa bwana Kabuga aliambia BBC itakuwa ukiukaji wa haki zake kumpeleka katika mahakama hiyo ya Arusha ikizingatiwa mlipuko wa virusi vya corona, afya na umri wake.

Freddy Mutanguha, makamu wa rais wa Muungano wa manusura wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda IBUKA amesema wanataka mshukiwa huyo' kupelekwa nchini Rwanda'.

Bwana Kabuga amedaiwa kufadhili makundi ya wapiganaji akiwa mwenyekiti wa hazina ya kitaifa ya ulinzi .

Mwezi Mei alizitaja tuhuma hizo kuwa za uwongo. Bwana Kabuga ana mwezi mmoja kuhamishwa katika mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa kutoka Ufaransa , kulingana na sheria za uhamisho.

Bwana Altit alisema kwamba kwasasbau hawana kwengine kwa kukata rufaa nchini Ufaransa , watawasilisha ombi kwa mahakama hiy hiyo ya Arusha kumwachia mteja wake kupelekwa The hague mjini Uholanzi.

Bwana Mutanguha amesema kwamba uamuzi wa mahakama hiyo ulikuwa mzuri kwa manusura wa mauaji hayo na kwamba Muungano wa IBUKA umeandikia mahakama hiyo ya Arusha pamoja na Umoja wa mataifa ikitaka bwana Kabuga kupelekwa nchini Rwanda.

''Tungependelea kumuoa nchini Rwanda…sasa Kabuga yupo mikononi mwao, tunataka waamue'', Bwana Mutanguha alisema.

Je anashtakiwa na nini?

Kabuga anashtakiwa kwa kufadhili mauaji ya kimbari nchini Rwanda.

Anadaiwa kuwasaidia wapiganaji wa kabila la Hutu ambao waliwaua takriban raia wa Tutsi 800,000 pamoja na Wahutu walio na msimamo wa kadri 1994.

Alianzisha kituo cha habari cha redio Télévision Libre des Mille Collines (RTLM), ambacho kilidaiwa kutoa wito kwa watu kuwaua watu wa kabila la Tutsi .

Mwaka 1997 alishtakiwa kwa mashtaka 7 ikiwemo mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya binadamu na jopo la kimataifa lililokuwa likichunguza mauaji hayo.

Je alikwepa vipi mtego wa polisi?

Maafisa wa polisi wanasema kwamba bwana Kabuga alitumia majina 28 tofauti kujificha.

Akiwa mtoro , alidaiwa kuishi katika mataifa mbalimbali Afrika mashariki ikiwemo Kenya, ambapo yeye na familia yake walikua na biashara.

Chanzo cha picha, Rex Features

Maelezo ya picha,

Kujificha kwa Kabuga kwa miaka 26 kulizua maswali mengi

Muendesha mashtaka wa Ufaransa alisema kwamba amekuwa akiishi kupitia utambulisho bandia.

Je mahakama hiyo ya mjini Arusha ni ipi?

Miezi kadhaa baada ya mauaji hayo , baraza la usalama la umoja wa mataifa lilianzisha mahakama ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda mjini Arusha, kaskazini mwa Tanzania.

Lengo lake ilikuwa kuwashtaki viongozi wa mauaji hayo na zaidi ya watu 60 walihukumiwa.

Mahakama hiyo ilifungwa rasmi mwaka 2015 na baadaye utaratibu wa Mahakama za Kimataifa za Jinai MICT ulichukua usimamizi wake ili kuwasaka washukiwa wa mwisho.

Mahakama hiyo haina maafisa wa polisi wala uwezo wa kukamata, na badala yake imekuwa ikitegemea serikali tofauti kuchukua hatua hizo badala yake.

Je Filicien Kabuga ni nani?

Ndiye aliyekuwa mtu tajiri zaidi nchini Rwanda kabla ya mauaji ya 1994.

Akijipatia utajiri wake kupita biashara ya majani ya chai mwaka 1970 na alifanya biashara katika sekta chungu nzima nyumbani na katika mataifa ya kigeni.

Alikuwa mshirika wa karibu wa chama tawala cha MRND - na alikuwa na uhusiano na rais wa zamani Juvenal Habyarimana ambaye alifariki 1994.

Akituhumiwa kwa kuwa mfadhili mkuu wa mauaji hayo na kutumia biashara yake na uwezo wake kupanga na kufadhili mauaji.

Mmiliki wa kituo cha redio ya kibinafsi RTLM alishutumiwa kwa kuwachochea watu wa kabila la Hutu kuwaua Watutsi.

Mwaka 2006, jopo la kimataifa la Rwanda lililokuwa likichunguza mauaji hayo lilisema lina ushahidi kwamba bwana Kabuga alizuru nchini Kenya ama hata kuishi nchini humo, ambapo alikuwa akisimamia maslahi yake ya kibishara.

Miaka mitatu baadaye, Bwana Stephen Rapp, ambaye alikuwa balozi wa Marekani aliishutumu serikali ya Kenya kwa kukataa kumtoa bwana Kabuga.

Kulikuwa na ushahidi kwamba bwana Kabuga alihudhuria hafla zilizoshirikisha watu maarufu, alisema madai ambayo Kenya imekana.

Ni wazi kwamba familia ya bwana Kabuga ilikuwa ikimiliki mali nchini Kenya baada ya mali moja kuzongwa na kesi 2015 wakati mkewe, Josephine Mukazitoni , ambaye alikuwa mmiliki mwenza , alipojaribu kumiliki.