Nagorno-Karabakh: Iran yaonya hatari ya kutokea 'vita vya ukanda'

Rais wa Iran Hassan Rouhani

Chanzo cha picha, Getty Images

Iran imeonya kuwa mapigano mapya kati ya majirani zake Azerbaijan na Armenia yanaweza kuongezeka na kuwa vita pana ya ukanda.

Rais Hassan Rouhani alisema ana matumaini "ya kurejesha utulivu" katika eneo hilo kufuatia siku kadhaa za mapigano makali yanayosababishwa na eneo lenye mgogoro la Nagorno-Karabakh.

eneo hili ni sehemu rasmi ya Azerbaijan lakini inadhibitiwa na jamii ya Waarmenia.

Mapigano ya sasa ni mabaya zaidi kuwahi kutokea katika miongo kadhaa, na pande zote mbili zimelaumiana kwa machafuko .

"Lazima tuwe waangalifu kwamba vita kati ya Armenia na Azerbaijan isiwe vita vya kieneo," Rais Rouhani alisema Jumatano.

"Amani ndio msingi wa kazi yetu na tunatarajia kurejesha utulivu katika eneo hili kwa njia ya amani," ameongeza.

Rais Rouhani pia alisema "haikubaliki kabisa" kwa makombora yoyote yaliyokosea njia kutua kwenye ardhi ya Irani.

Maoni yake yalifuatia ripoti kwamba makombora yalikuwa yametua kwenye vijiji vya Irani, karibu tu na mpaka wake wa kaskazini na Armenia na Azerbaijan.

"Kipaumbele chetu ni usalama wa miji na vijiji vyetu," Rais Rouhani alisema.

Kamanda wa Walinzi wa Mipaka wa Irani Qasem Rezaei pia alisema vikosi vyake vimejitatiti.

"Tangu kuanza kwa mzozo ... makombora kadhaa ya roketi na roketi zimegonga eneo la [Iran]," alisema, kulingana na shirika la habari la Tasnim.

"Walinzi wetu wa mipaka wako macho na wamehamia kwenye maeneo muhimu. Wanafuatilia kikamilifu na kudhibiti mipaka."

Ni nini kingine kinachotokea?

Siku ya Jumatano, Rais wa Urusi Vladimir Putin alitoa wito wa kumaliza mapigano, ambayo alielezea kama "janga".

"Tuna wasiwasi sana," alisema kwenye mahojiano kupitia televisheni. "Tuna matumaini kuwa mzozo huu utamalizika katika siku za hivi karibuni.

"Watu wanakufa [na] kuna hasara kubwa pande zote mbili.

Bwana Putin pia alifanya mazugumzo mafupi ya simu na rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev Jumatano, Kremlin ilisema.

Urusi ni sehemu ya muungano wa kijeshi na Armenia na ina kituo cha jeshi nchini humo. Hatahivyo, pia ina uhusiano wa karibu na serikali ya Azerbaijan.

Marekani, Ufaransa na Urusi kwa pamoja wamelaani mapigano huko Nagorno-Karabakh na wametaka mazungumzo ya amani, lakini mzozo huo hauoneshi dalili zozote za kupungua.

Siku ya Jumatano Azerbaijan ilisema Waziri wa Mambo ya nje Jeyhun Bayramov atakutana na wapatanishi wa kimataifa huko Geneva siku ya Alhamisi.

Armenia ilijibu kuwa "haiwezekani kufanya mazungumzo kwa mkono mmoja na kuendelea na shughuli za kijeshi kwa mkono mwingine", na kwamba waziri wake wa mambo ya nje hatakutana na Bwana Bayramov huko Geneva.

Zohrab Mnatsakanyan wa Armenia hata hivyo anatarajiwa huko Moscow kwa mazungumzo wiki ijayo.

Uchabuzi wa Orla Guerin wa Tartar, Azerbaijan

Azerbaijan imesema inaendelea kusonga mbele karibu na eneo lenye mgogoro mrefu wa Nagorno-Karabakh. Ina nguvu zaidi ya moto, na silaha za kisasa zaidi.

Kwa sasa inaonekana kuwa na nguvu, lakini maeneo karibu na mstari wa mbele yapo ndani ya shabaha ya vikosi vya Waarmenia.

Jiji la Tartar - ambalo linapakana na Nagorno-Karabakh -ina makazi ya watu 100,000 lakini wengi wanaonekana kukimbia mapigano.

Barabara kuu imekuwa tupu na imejaa glasi na vifuniko vilivyovunjika. Maduka yameharibwa, na paa zimeezuliwa.

Tulipata familia chache zilizokuwa chini ya ardhi. Mwanamke mmoja mzee - ambaye mtoto wake wa kiume na binti wanapigana na vikosi vya Azerbaijan katika mstari wa mbele - alituambia alikuwa akingojea ushindi na hataondoka kamwe.

Kinachotokea sasa kwenye eneo la kivita

Mapigano hayo yamehamisha nusu ya wakazi wa Nagorno-Karabakh - karibu watu 70,000 - mwangalizi wa haki za binadamu wa eneo hilo Artak Beglaryan aliliambia shirika la habari la AFP.

Jiji kuu huko Nagorno-Karabakh, Stepanakert, limharibiwa na siku kadhaa za mashambulizi ya makombora. Wakazi wamekuwa wakijificha katika vyumba vya chini na jiji kubwa limeachwa bila udhibiti

Kulikuwa na mgomo mpya Jumatano asubuhi na moshi ulionekana karibu na Stepanakert, kwa mujibu wa ripoti za AFP.

Chanzo cha picha, Getty Images

Wakati huo huo, Azerbaijan ilishutumu vikosi vya kikabila vya Armenia kwa kupiga makombora maeneo ya mijini na kulenga majengo ya raia.

Jiji lake la pili kwa ukubwa, Ganja, limeshambuliwa na maafisa wa Azerbaijan walisema mamia ya majengo yaliharibiwa.

Mwishoni mwa wiki Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu ililaani "matukio ya kurusha makombora ya kiholela na mashambulio mengine yanayodaiwa kuwa haramu"

Zaidi ya watu 300 wamekufa tangu mapigano hayo yaanze tarehe 27 Septemba.

Lakini kuna hofu idadi halisi ya vifo kati ya vikosi vya jeshi kutoka pande zote pamoja na raia zinaweza kuwa kubwa zaidi, kwani madai ya majeruhi hayajathibitishwa.