Virusi vya corona: Rais Trump amesema kuumwa kwake ni 'baraka kutoka kwa Mungu'

Rais Donald Trump akivua barakoa baada ya kurejea Ikulu akitokea hospitali

Chanzo cha picha, Reuters

Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa anajisikia ni mwenye nguvu,baada ya kuugua ugonjwa wa Covid-19,ambapo amesema ugonjwa huo kwake ni 'Baraka za Mungu'

Trump hapo jana alirejea katika ofisi zake za Oval ikiwa ni chini ya wiki moja tangu alipo pimwa na kukutwa na virusi vya Corona.

Daktari wa rais Trump Sean Conley amesema kuwa rais hakuwa na dalili zozote kwa zaidi ya saa ishirini na nne na bila ya kuwa na homa yoyote ndani ya siku nne na kuongeza kuwa amepona.

Hata hivyo Trump mwenyewe amesema kuwa raia wa Marekani wanapaswa kupatiwa huduma kama aliyopewa yeye na ameahidi kutoa dawa bure ambazo zimetengenezwa na kiwanda cha dawa cha Regeneron.

Trump ameongeza kuwa kipimo cha kinga zake za mwili alichofanyiwa ni dawa tosha zaidi hata ya hizo alizopatiwa kwani ilibainika kwamba kinga zake tu zingetosha kukabiliana na virusi hivyo kwa kuwa zipo imara,japo kuwa pia hadi sasa dawa hizo za Regeneron haizjathibishwa kimataifa na shirika la afya duniani WHO.

"Hizi zilikuwa baraka za Mungu,nilibaini hilo,nilikwisha sikia habari za dawa hii,nikasema ngoja nitumie na kwa kweli inafaa''alisema Trump akisisitiza kwamba atatafuta kibali cha dharula kutoka kwa mamlaka ili ziweze kutumika. Kuhusiana na shutuma zake dhidi ya China, Rais Trump alirejea mashambulizi yake dhidi ya taifa hilo,na kuwaambia raia wa Marekani,wala hamtalipia gharama za janga hili lililotokea,maana hamstahili kulaumiwa,hii ni lawama ya China.Na China italipia gharama suala hili maana wanahusika na ilikuwa makosa yao.

Daktari wake rais Trump, Dr Conley amesema kuwa rais hakuhitaji msaada wa Oksijen tangu alipofikishwa hospitali siku ya ijumaa hadi aliporuhusiwa siku ya jumatatu.

Hata hivyo Trump ameonekana kukiuka masharti,tangu aruhusiwe na kurejea ofisini,na kuamua kuendelea kufanya kazi ofisini kwake Oval badala ya nyumbani kwake na pia kuonekana akishinikiza kuhutubia taifa na kuendelea na kampeni zake.

Lakini hadi sasa wasaidizi wake walio wengi bado wamejitenga.Mapema mmoja wa maafisa wa juu katika ikulu ya White house Mark Meadows amesema kila anayelazimika kukutana na Trump kwa sasa amejihami na mavazi maalumu kama vile barakoa na vifaa vingine.

Ripoti zinasema kwamba hata kabla ya rais Trump kubainika kuwa na Corona,ni kwamba hakukuwa na utamaduni wa watu ndani ya ikulu ya White House kuvaa barakoa,kitendo ambacho kinapingwa kwa nguvu zote.