Maharusi waliopendana licha ya vimo vyao Kenya

  • Roncliffe Odit
  • BBC Swahili
Maelezo ya picha,

Lilian Wawira Gatimu na mumewe Ezekiel Mwangi Maina

Hadithi ya Lilian Wawira Gatimu na mumewe Ezekiel Mwangi Maina ni kama filamu. Wapenzi hawa wawili wamegonga vichwa vya habari mitandaoni nchini Kenya baada ya kufanya harusi Jumamosi iliyopita, 19.12.2020.

Lakini si picha maridadi za harusi yao zinazozungumziwa, wengi wamekuwa wakizungumzia tofauti kubwa ya kimo kati ya wapenzi hao wawili.

Lilian Wawera Gatimu, mwenye umri wa miaka 28 ana urefu wa zaidi ya futi 7, huku mumewe Ezekiel Mwangi Maina, mwenye umri wa miaka 33, akiwa na urefu wa angalau futi 3.

Wanandoa hawa walikutana Aprili ya mwaka 2017 katika harusi ya rafiki yao wa karibu. Kwanza hawakuwa hata marafiki. Lakini Lilian anasema alivutiwa na ujasiri wa Bwana Mwangi.

'Mara moja tu aliponiona, yeye aliomba namba yangu ya simu. Nikajiambia huyu ndiye mume wa kweli.'

Maelezo ya picha,

Wanandoa hawa walikutana Aprili ya mwaka 2017 katika harusi ya rafiki yao wa karibu

Urafiki wao wa zaidi ya miaka mitatu ukaanzia hapo.

Lakini wanasema haikuwa safari rahisi; ilijawa na pandashuka za kila aina.

Kwanza, familia ya Bwana Mwangi haikutaka kabisa kumuona mwanao akiwa na mpenzi mrefu kama mlingoti.

Walijaribu kwa kila njia kumshawishi amuache na kutafuta mpenzi wa kimo chake.

'Walikuwa wanasema mimi ni mrefu sana, na pia nina umri mkubwa kumshinda,' anaeleza Bi Lilian.

Bi Lilian ni Munjilisti wa Kanisa la Anglikana mjini Baringo, naye Bwana Mwangi ni mfanyibiashara.

Baadhi mitandaoni wamedai kwamba Lilian alikubali kuolewa na mwanamume huyu mfupi kwa sababu Mwangi ana hela nyingi.

Lakini je, madai hayo yana ukweli wowote?

Bwana Mwangi anaeleza kwamba mapenzi yao hayajajengwa kwa msingi wa pesa.

'Kama tungekuwa na pesa nyingi, tungekuwa fungate Dubai ama Maasai Mara. Lakini sisi tuko hapa nyumbani tu.'

Basi ni nini haswa kilichomvutia Lilian kwa mumewe?

'Ni vigumu sana Mwangi akasirike, ana utu mwema, ni mtu ambaye sipati shida hata kidogo kuishi naye. Na ananipenda sana,' anasema Lilian.

'Ananiita 'baby' licha ya kwamba mimi ndio mrefu.'

Siku ya harusi yao, Jumamosi iliyopita, walijiunga na ndugu, jamaa na marafiki kusherehekea penzi lao ambalo sasa limedumu zaidi ya miaka mitatu.

Na hata familia ya Bwana Mwangi hatimaye wamemkubali mke wake, nao pia walihudhuria harusi yao.

Lakini wamepoteza baadhi ya marafiki waliowathamini hapo mbeleni.

'Wengine walinitusi, wakaniambia maneno yasiyofaa. Baadhi wakasema nitafute mtu mrefu kama mimi,' anasema Lilian.

Lakini licha ya hayo yote, wapenzi hawa wawili wameendelea kuwa imara katika penzi lao, huku Lilian akisisitiza kwamba anamheshimu sana mumewe licha ya kimo chake. Anasema yeye ndio kichwa cha familia yao.

'Mara kwa mara sisi pia hukosana kama tu wapenzi wengine. Lakini yeye ni mpole, na amenifundisha kuomba msamaha.'

Hata hivyo kwao nyumbani wanasema imewalazimu kutengeneza kitanda spesheli kwa sababu ya kimo cha Lilian. Hata godoro lao wananunua kutoka kwa kiwanda cha magodoro kwani hakuna godoro linalomtoshea madukani.

Mungu akiwabariki, wangependa kuwa na watoto wawili au watatu.