Vita vya Syria: Mashambulizi ya Israeli yadaiwa kulenga lenga ngome za Iran na kusababisha mauaji

File photo showing an Israeli F-35 fighter jet flying over southern Israel (27 June 2019)

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Israeli haijasema lolote kuhusiana na taarifa hizo lakini mara kwa mara imekuwa ikishambulia maeneo yenye kuhusishwa na Irani nchini Syria

Israeli imeripotiwa kufanya mashambulizi ya anga katika maeneo yanayosemekana kuwa ya waasi wanaoungwa mkono na Iran huko nchini Syria ikiwa ni shambulizi la nne la aina hiyo ndani ya wiki mbili.

Shirika la habari la Sana linalomilikiwa na Syria limesema ndege za Israeli zilishambulia maeneo ya magharibi ya Deir al-Zour na Albu Kamal.

Taarifa hiyo haikusema kama kuna yeyote aliyejeruhiwa lakini Shirika la Haki za Binadamu la Syria lenye makao yake Uingereza limesema kuwa wanajeshi wa Syria 14 na waasi washirika wake 43 wameuawa kwenye shambulizi hilo.

Israeli haijasema lolote lakini mara nyingi hushambulia maeneo lengwa yenye kuhusishwa na Irani nchini Syria.

Mkuu wa wafanyakazi wa vikosi vya ulinzi vya Israeli, Jenerali Aviv Kochavi, aliambia vyombo vya habari vya Israeli mwezi uliopita kwamba imefanya mashambulizi zaidi ya 500 mwezi uliopita.

"Muingilio wa Iran nchini Syria sasa hivi ni wa chini kwa sababu ya vikosi vya serikali ya Israeli lakini bado kuna mengi ya kufanya kumaliza malengo yetu," amesema.

Israeli imewashutumu maadui zake kwa kuimarisha jeshi ndani ya Syria na kutumia nchi hiyo kuingiza silaha za kisasa kwa kundila wapiganaji wa Hezbollah nchini Lebanon.

Iran inaaminika kuwa imepeleka mamia ya vikosi nchini Syria na pia imetoa silaha, kutoa mafunzo na kufadhili maelfu ya wanamgambo wa Kiislamu wa Shia - kutoka Lebanon, Iraq, Afghanistan na Yemen - kuunga mkono vikosi waaminifu kwa Rais Bashar al-Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria.

Shirika la habari la Sana limesema Israeli imefanya mashambulizi ya "anga" karibu na miji wa Deir al-Zour na Albu Kamal, ambao uko karibu na mpaka wa Iraqi, Jumatano.

Shirika hilo limesema bado uharibifu uliotekelezwa unaendelea kutathminiwa na kushutumu Israeli kwa kuingilia "moja kwa moja kuunga mkono mashirika ya ugaidi", hasa la kundi la jihadi la Islamic State (IS), ambalo limekuwa likiendeleza shughuli zake eneo hilo.

Shirika la haki za binadamu la Syria lenye makao yake Uingereza ambalo linafuatilia vita vya nchini Syria kupitia mtandao wa vyanzo kadhaa, limesema mashambulizi ya anga 18 ya Israeli yamelenga vituo vya kuhifadhi silaha za kijeshi na kambi moja cha jeshi viungani mwa mji wa Deir al-Zour, kambi za kijeshi huko Albu Kamal, na maghala yaliyopo nje ya Mayadin.

Takribani watu 57 waliuawa ikiwemo wanajeshi wa Syria, wapiganaji wa Iraq 16, 11 wa Afghan na wengine wengi walipata majeraha, shirika hilo limesema.

Vikosi vyenye kuhusishwa na vikundi vya Hezbollah, Fatemiyoun na waasi wa Kishia wa Afghan walikuwa wakiendeleza shughuli zao katika maeneo yaliyovamiwa, limeongeza.

Kituo cha televisheni kinachomilikiwa na Iran cha Al-Alam, kimenukuu chanzo kimoja kuwa "hakuna raia wa Iran, Syria, au wa kundi la Fatemiyoun waliokuwa ni wafiadini".

Pia inasemekana kuwa Israeli imetekeleza mashambulizi matatu ya anga nchini Syria wiki mbili yakilenga vituo vya kijeshi, mabohari ya silaha na maeneo lengwa kusini na magharibi viungani mwa eneo la Damascus na miinuko ya Golan.

Juni 2018, wapiganaji 55 wanaopendelea serikali waliripotiwa kuuawa katika eneo hilo hilo.

Shambulizi hilo linawadia wakati wasiwasi ukiendelea kuongezeka katika eneo hilo huku vikosi vya Israel na Marekani vikiwa katika tahadhari ya Iran kutekeleza mashambulizi ya kulipiza kisasi mauaji ya afisa wa ngazi ya juu wa nchi hiyo Qasem Soleimani aliyeuawa na Marekani mwaka mmoja uliopita.