Halima Aden: Hatua niliyoichukua imenifanya kuwa huru zaidi

Halima Aden

Chanzo cha picha, Giliane Mansfeldt Photography

Mwanamitindo wa kwanza Marekani kuvaa hijabu Halima Aden, aliachana na fani hiyo mwezi Novemba akisema kuwa inaenda kinyume na maadili ya dini yake ya Kiislamu.

Akiwa katika mahojiano na mwandishi wa BBC Sodaba Haidare - anaelezea namna alivyokuwa mwanamitindo, na kilichomfanya kuamua kuiacha.

Halima, 23, anaishi Minnesota, alipokulia akiwa pamoja na raia wengine wenye asili ya Somali. Amevaa nguo za kawaida na hajajipaka vipodozi huku akimpapasa mbwa wake, Coco.

"Mimi ni Halima kutoka Kakuma," anasema, akirejelea kambi ya wakimbizi Kenya, alipozaliwa. Wengine wamemuelezea kama mwenye udhubutu aliyekuwa mwanamitindo wa kwanza kuvaa hijabu na kuangaziwa katika jarida la urembo la kimataifa la Uingereza la Vogue - lakini yote hayo aliyapa kisogo miezi miwili iliyopita, akisema fani ya uanamitindo haikwendana na imani yake ya Kiislamu.

"Hatua niliyochukua imenifanya kuwa huru zaidi katika mahojiano," akiwa anacheka. "Kwasababu sikutumia saa 10 kujitayarisha, kuvaa nguo ambayo sitakuwa nayo baada ya hapo."

Mwanamitindo huyo, Halima alikuwa akichagua nguo za kuvaa. Mwanzoni mwa kazi yake, alikuwa akibeba begi lililojaa hijabu, gauni zake ndefu na sketi kila anapokwenda kupigwa picha. Alivaa hijabu yake nyeusi katika kampeni yake ya fesheni ya Rihanna ya Fenty.

Hata hivyo alikuwa akivaa gauni lake akiwa na hijab kila wakati anapokuwa kazini.

Hilo halikuwa na mjadala na mwaka 2017 aliposaini mkataba na kampuni ya mitindo ya IMG, moja ya kampuni kubwa za urembo duniani akaongeza kipengele katika mkataba wake cha hijabu na kuifanya kampuni ya IMG kutokuwa na uwezo wa kuondoa kipengee hicho.

Hijabu yake ilikuwa kila kitu maishani mwake.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Halima akifanya onesho la uanamitindo na kampuni ya Max Mara Februari 2017

"Hawa ni wasichana ambao walitaka kufanya kila kilichokwenye uwezo wao kuwa wanamitindo," anasema, "lakini nilikuwa tayari kuondoka kwenye kampuni hiyo iwapo wangekataa kipengee hicho."

Hiyo ilikuwa ni licha ya kwamba wakati huo hakuna aliyekuwa anamjua.

Lakini kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga mbele, alianza kuwa na udhibiti mdogo wa nguo atakazo vaa na akakubali kuvaa vitambaa vya kichwani alivyokuwa amevikataa awali.

"Nilitekwa na kazi yangu na ikafika wakati timu niliyokuwa nayo ndio ilikuwa inachukua jukumu la kunifunga hijabu."

Mwaka wa mwisho wa taaluma yake, hijabu yake iliendelea kuwa ndogo kila uchao, wakati mwingine inazunguka tu kwenye shingo yake na kifuani.

Na wakati mwingine badala ya hijabu, alijifunga kitambaa cha 'jeans' na aina nyingine ya vitambaa kuzunguka shingo yake.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Akionesha mitindo ya mavazi akiwa na kampuni ya Tommy Hilfiger London mwaka 2020

Kipengele kingine cha mkataba wa Halima kilimwezesha kuvalishwa katika sehemu anayoikubali yenye faragha.

Lakini haikupita muda mrefu, akaanza kuona kwamba wanamitindo wengine wanaovaa hijabu walikuwa hawapewi heshima kama anavyopewa yeye.

"Hilo lilinikera na nikaanza kujiuliza, hawa wasichana wananifuata mimi na sasa ni kama nimewatumbikiza pabaya."

Alitarajia kuwa watakao mrithi watapata haki sawa kama yeye. "Wengi wao ni vijana wadogo, inaweza kuwa tasnia yenye changamoto. Hata tafrija tunazohudhuria, kila wakati nilijiona nikiwa kama dada yao mkubwa na nilikuwa ninajikuta namshika mkono mmoja wa wanamitindo waliovaa hijab kwasababu amezungukwa na kundi la wanaume. 'Hii haileti picha nzuri, huyu bado ni mtoto.' Ningemtoa na nimuulize alikuwa na nani."

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Halima Aden

Sehemu ya kujulikana inayojitokeza ni historia ya Halima ambaye ni msomali.

Akiwa mtoto katika kambi ya Kakuma, kaskazini magharibi mwa Kenya, alifunzwa na mama yake namna ya kufanya kazi kwa bidii na kusaidia wengine.

Na hilo likaendelea hata baada ya kuhamia Minnesota nchini Marekani, Halima alipokuwa na umri wa miaka saba na kuwa sehemu ya jamii kubwa ya Somali nchini Marekani.

Kulikuwa na tatizo pale Halima alipotambuliwa shuleni kama malkia wa uvaaji hijabu. Alijua hilo lingemkasirisha mama yake ambaye alitaka azingatie masomo yake.

"Niliona aibu sana kwasababu unapochaguliwa, watoto huja nyumbani kwenu na mimi nikawaambia, musifanye hivyo kwasababu huwezi kujua kama mama yangu amekubali na pengine tunaweza kujitafutia shida zaidi.

Uoga wake ulikuwa sawa. Mama yake Halima alikataa kufanya tafrija ya kumkaribisha malkia nyumbani kwao.

"Unatumia muda mwingi kujishughulisha na rafiki zako na mashindano ya uanamitindo," alisema.

Lakini bado Halima alishiriki mashindano ya urembo ya kumtafuta Miss Minnesota USA mwaka 2016.

Alikuwa mwanamitindo wa kwanza aliyevaa hijab ambaye ameingia kwenye nusu fainali.

Chanzo cha picha, Alamy

Maelezo ya picha,

Akishiriki shindano la urembo la Miss Minnesota mwaka 2016

Kama haitoshi, mama yake Halima alipigwa na butwaa zaidi alipojua kuwa msichana wake anasomea kuwa mwanamitindo fani ambayo mama yake alifikiria inakwenda kinyuma na imani yake ya Kiislamu.

Hata alipoanza kushiriki matamasha mbalimbali ya urembo kama vile Yeezy na Max Mara, au kuwa jaji wa Miss USA, bado mama yake alisisita "atafute kazi nyinge".

Chanzo cha picha, Getty Images

Hitaji lake lilipoanza kuongezeka katika tasnia ya mitindo, alikuwa na muda kidogo sana na familia yake na alikuwa hapatikani wakati wa matamasha ya Kiislamu.

"Mwaka wa kwanza wa taaluma yangu nilikuwa nyumbani wakati wa sikukuu ya Eid na Ramadan lakini katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Nimekuwa nikisafiri tu. Nilikuwa ninapanda karibu ndege sita au saba kwa wiki," anasema. Halima alinza kuwa na mashaka na taaluma yake ya uanamitindo.

Mwaka 2019, aliangaziwa katika jarida la King Kong akiwa amevaa nguo nyekundu na macho yake yakiwa yamepakwa rangi ya kijani na kuvishwa vito vyenye ukubwa wa ajabu ambavyo viliziba kila kitu isipokuwa mdomo na pua.

"Mtindo wao na vipodozi walivyotumia vilikuwa vinatisha," amesema.

Na kilichomshangaza zaidi, alione picha ya mwanaume aliyekuwa uchi wa mnyama katika suala hilo hilo lake.

"Kwanini jarida hilo lilifikiria ni sawa kuwa na mwanamke wa Kiislamu aliyevaa hijabu huku mwanaume aliyekuwa uchi wa mnyama akiwa ukurasa wa pili?" anauliza. Ilienda kinyume na kila kitu alichokuwa anakiamini.

"Inasikitisha kuona Halima anajuta kufanya kazi na sisi na kwamba kulikuwa na picha katika suala aliloshirikishwa ambazo yeye mwenyewe hakuzipenda ingawa hazikuwa na uhusiano wowote na alichoangaziwa yeye," kulingana na mkuu wa jarida la King Kong.

Halima anasema alipoona picha yake kwenye ukurasa wa juu wa majarida uwanja wa ndege wakati anasafiri, ni mara chache sana angeweza kujitambua.

Chanzo cha picha, Alamy

"Hakukuwa na cha kunifurahisha kwasababu sikuweza kujiona. Unajua hilo linaweza kumtatiza mtu akili kwa kiasi gani? Ninapotakiwa kuwa na furaha kwasababu hiyo ni picha yangu lakini ilikuwa kinyume chake"."Taaluma yangu ilikuwa juu lakini nilikuwa ninatazika akilini."

Janga la virusi vya corona vimebadilisha mengi. Ugonjwa huo umefanya matamasha ya urembo hayafanyiki kama ilivyokuwa na akaamua kurejea nyumbani kwa mama yake.

Chanzo cha picha, GILIANE MANSFELDT PHOTOGRAPHY

"Nilikuwa nafikiria vile mwaka 2021 utakavyokuwa kwasababu nilikuwa nyumbani tu na familia yangu na rafiki zangu," anasema.

Hayo yote yanaelezea kwanini aliamua kuachana na uanamitindo.

Na ndoto ya mama yake hatimaye imetimia. Alifurahishwa sana na uamuzi wa binti yake wa kuachana na uanamitindo kiasi kwamba aliamua kupiga