Matokeo ya uchaguzi 2021: Mzozo wa mitandao ya kijamii Uganda waibua maswali kuhusu mawasiliano Afrika

Bobi Wine na Yoweri Museveni

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Sehemu kubwa ya kampeni kuelekea uchaguzi wa Alhamisi ilifanyika mtandaoni kutokana na vikwazo vya Covid-19

Baada ya Facebook kufunga akaunti za baadhi ya Waganda na mamlaka nchini humo kufuatia msururu wa kufungia mitandao ya kijamii na baadae kuzima huduma zote za intaneti, mwandishi wa BBC Dickens Olewe anatathmini athari za hatua hiyo kwa Uganda na maeneo mengine barani Afrika .

Facebook imesema ilikuwa inatekeleza masharti yake lakini hivyo sivyo Rais Museveni alivyochukulia hatua hiyo.

''Hakuna namna mtu yeyote anaweza kuja [hapa] na kucheza na nchi yetu na kuamua ni nani mzuri [na] nani mbaya," alisema alipotetea uamuzi wake kwa mujibu wa uamuzi wa kampuni hiyo kufunga akaunti zinazohusishwa na chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa Alhamisi.

Rais aliilaumu Facebook, ambayo yeye na wagombea wengine wamekuwa wakitumia kufanya kampeni, kuwa na "kiburi".

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Watu walipiga kuraUganda licha ya huduma za itaneti kukatizwa siku ya Alhamisi

Msemaji wake wa habari Don Wanyama, ambaye akaunt yake ilikuwa miongoni mwa zile zilizoathiriwa, aliiambia BBC kwamba mtandao huo wa kijamii umegeuka kuwa wa "kidikteta".

"Ni mtando wa kijamii tu, haustahili kugeuka na kuwa chama cha kisiasa. Lazima kuwe na kanuni zinazoongoza mitandao hii na shirika huru la uangalizi," Bw. Wanyama alisema, akiongoza kuwa Tume ya Mawasiliano ya Uganda lazima ihusishwe kuhakikisha "usawa unazingatiwa".

Katika taarifa yake, Facebook ilisema kwamba ilichukua hatua baada ya uchunguzi kubaini kuwa akaunti hizo zilihusika katika juhudi zilizoratibiwa za kuhujumu mjadala wa kisiasa nchini.

Licha ya umuhimu wa hatua hiyo, wachambuzi wameiambia BBC kwamba mtandao maarufu wa kijamii kama Facebook ulistahili kutilia maanani mazingira unaofanyia kazi.

'Mtando wa akaunti ghushi'

Wanapendekeza kwamba kampuni hizo ziwaajiri watu wengi kwa kuzingatia na kubuni kitengo cha kushughulikia masuala ya uchaguzi na ambacho kitafanya kazi na makundi ya kijamii ili kuwawezesha kubuni kanuni maalum kwa eneo fulani kuliko kutumia sera moja kubwa kufanya maamuzi

Bw. Wanyama alimlaumu mgombea mkuu wa upinzani Robert Kyagulanyi - maarufu Bobi Wine - kwa kuhusika na kufungwa kwa akaunti hizo.

Madai hayo yalipingwa na mtafiti Tessa Knight kutoka shirika la utafiti la Digital Forensic Research Lab, ambalo uchunguzi wake ulibaini kampeni zilizoratibiwa na NRM kulenga upinzani.

"Nilipokamilisha uchunguzi wangu, nilituma maelezo kwa Facebook. Walifanya uchunguzi wao wenyewe, uliokuwa huru na kuamua kwamba akaunti hizo zilikuwa zikitumiwa katika jaribio la kushawishi mijadala ya umma kabla ya uchaguzi ," Bi. Knight aliiambia BBC, akiongeza kuwa hakufanya kazi na Bobi Wine kama inavyodaiwa.

Facebook ilielezea kwamba hali hiyo hutokea wakati, makundi ya kurasa au watu wanapofanya kazi pamoja kupotosha wengine kuhusu wao ni nani au wanafanya nini kwa kutumia akaunti bandia.

Mfano mmoja ni ule wa baadhi ya akaunti kama Uganda investigation kutuma ujuma wa aina moja katika mtandao wa Facebook na Twitter, kuunga mkono msako wa polisi dhidi wafuasi wa upinzani:

Chanzo cha picha, DFRLab investigation

Mwishoni mwa mwaka uliopita Facebook ilitangaza kwamba imegundua shambulio kama hilo ililofanywa na akaunti za Ufaransa - na Urusi zikijaribu kushawishi maoni ya wapigakura Jumhuri wa Afrika ya Kati.

Kwa mujibu wa mtafiti wa sera za intaneti kutoka Kenya, Odanga Madung, hatua ya kuzifungia kurasa ambazo zinafungamana na chama cha NRM imefichua namna gani suala la udhibiti wa maudhui mtandaoni ni jambo nyeti, na hatua hiyo ikaipatia sababu serikali ya Uganda kutekeleza jambo ambalo walishalipanga.

"Mtu yeyote anayefuatilia siasa za Uganda alitarajia serikali itadhibiti huduma za intaneti kabla ya uchaguzi, kwa hivyo hatua ya Facebook - hususan bila ya kuwa na mpango wa kuwachukulia hatua wanaokiuka kanuni ya huduma zake - ilitoa nafasi kwa Museveni kuifungia kama hatua ya kilipiza kisasi," alisema Bw. Madung.

Tofauti na marufuku ya Trump

"Kitu ambacho kinajitokeza wazi katika mzozo huu ni kwamba hali hii itaendelea kushuhudiwa Afrika, hasa katika nchi za kimabavu, wakati kampuni za mitandao ya kijamii zinakabiliwa na shinikizo la kutekeleza masharti yao ya huduma, "aliiambia BBC.

"Lakini nadhani ni nafasi ya Facebook na mitandao mingine kuimarisha uwepo wao barani Afrika, zaid ya kuwa na maafisa wachache hapa na pale, na kushirikiana katika huhakiki taarifa," Bw. Madung alisema, akiongeza kuwa "lazima tukumbuke kwamba hizi ni kampuni binafsi na maslahi ya faida kwa wamiliki zinapewa umuhimu".

Baadhi ya wachambuzi wanasema tofauti na Marekani ambako mitandao ya kijamiii ilimpiga marufuku rais, nchini Uganda ni rais alitoa agizo la kufungiwa kwa mitandao hiyo.

Mchora katuni maarufu wa Tanzania Gado aliangazia hali hiyo kupitia sanaa yake ya uchoraji.

Katika kuhalalisha marufuku dhidi ya mitandao ya kijamii, serikali ya Uganda imeiga kauli ya kampuni za mitandao ya kijamii.

"Kumekuwa na utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii kueneza taarifa zisizokuwa na msingi ambazo zimekukwa zikiwakosoa maafisa wa serikali ... kama kweli tunazingatia demokrasia tunahitaji watu ambao wanawasilisha ukweli jinsi ulivyo," Waziri Betty Amongi aliiambia BBC.

Mchambuzi wa siasa Nanjala Nyabola, ambaye ameangazia kwa kina masuala ya teknolojia barani Afrika, amesema kupigwa marufuku kwa Rais wa Marekani Donald Trump kutumia mitandao mikuu ya kijamii kumefungua awamu mpya ya mjadala " wenye utata" kimataifa.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Wanasiasa na wanaharakati waandamana dhidi ya kodi ya mitandao ya kijamii iliyowekwe miaka mitatu iliyopita

'Raia dhidi ya serikali'

Anaamini kwamba mazingira yaliyochangia kuchukuliwa kwa hatua hiyo ni muhimu

"Mtandao huo wa kijamii huenda ungelichukuwa hatua sawa na hiyo katika maeneo mengine na tafsiri ingekuwa tofauti kabisa.

"Inategemea uhusiano uliyokuwa awali kati ya raia na serikali. Nchi Uganda serikali inasema marufuku hiyo inakiuka demokrasia lakini hoja hiyo pia inalingana na kukamatwa kiholewa na kukandamizwa kwa wagombea wa upinzani. Na historia ya vurugu kutoka kwa serikali dhidi ya raia imebadilisha mtazamo wa suala hilo baada ya kuondolewa kwa mitandao hii," aliambia BBC.

Kumekuwa na historia ya serikali ya Uganda kudhibiti mitandao ya kijamii.

Mwaka 2018 ilibuni sheria tata ya kutoza kodi mitandao ya kijamii, ambayo Rais Museveni aliitetea kama njia ya kukabiliana na "udaku " katika mitandao hiyo.

Sera hiyo badala yake imefanya huduma za intaneti kuwa ghali zaidi na matokeo yake yamekuwa kukosesha faida kampuni ya mawasiliani.

Athari za kiuchumi zitakazotokana na udhibiti wa sasa wa huduma za intaneti zitachangia hali kuwa ngumu zaidi.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Bw.Trump alikutana na Bw. Museveni mwaka 2017

Kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na kampuni ya Top1OVPN ulioangazia athari za kufungwa kwa intaneti mwaka 2020, zaidi ya watu milioni 50 katika eno la kusini mwa Sahara barani Afrika waliathiriwa na hatua hiyo iliyoathiri uchumi kwa takriban dola milioni 237 sawa na (£173m).

Nchini Uganda, kampuni ya Netbocks - ambayo inakadiria athari ya kukatizwa kwa huduma za intaneti - imekadiria kuwa nchi hiyo itapoteza karibu dola milioni 1.7m sawa na(£1.2m) kwa siku, kiasi ambacho kitakuwa na athari ya moja kwa moja na kwa biashara zinazotegemea huduma hiyo.

Sheria tofauti?

Hali hiyo inaibua maswali magumu kuhusu uhusiano kati ya makampuni ya mitandao ya kijamii na serikali endapo udhibiti utaimarishwa zaidi.

Bi. Nyabola ana wasiwasi kuwa ikiwa sheria zitabanwa zaidi, usawa hautakuwepo kwani sheria hizo zitanufaisha zaidi upande wa serikali.