Kuapishwa kwa Joe Biden: Amanda Gorman msichana aliyeghani ushairi uliovutia umma ni nani?

Amanda Gorman amekuwa ni mshairi mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutumbuiza katika sherehe ya kuapishwa kwa rais nchini Marekani.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Amanda Gorman amekuwa ni mshairi mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutumbuiza katika sherehe ya kuapishwa kwa rais nchini Marekani.

Amanda Gorman "alipiga kelele na kudensi kama mwenda-wazimu " wakati alipofahamishwa kuwa amechaguliwa kusoma mojawapo ya mashairi yake katika sherehe ya kuapishwa kwa Rais Joe Biden.

Akiwa na umri wa miaka 22, amekuwa mshairi mwenye umri mdogo zaidi kutumbuiza katika sherehe ya kuapishwa kwa rais na kwa maneno yake aliuvutia umma.

Hotuba yake katika tukio hilo kupitia ushairi aliouita "The Hill We Climb" ilisambaa katika mitandao ya kijamii na kampeni ya mtandao wa kijamii kupitia alama ya reli #AmandaGorman ikafurika kwenye mtandao wa Twitter.

Gorman aliiambia BBC kabla ya tukio hilo kwamba alihisi mwenye "msisimko, furaha, heshima na mnyenyekevu" alipoombwa kushiriki katika shehere ya kuapishwa kwa Bw Biden , "na wakati huohuo alihisi kuwa na uoga."

Ushairi wake, anasema ni utunzi mpya ambao ulitungwa kwa ajili ya "kuzungumzia wakati huo " na "kufaa kwa wakati huo."

Hii ni sehemu ya ushairi wa Amanda :

"Tumeona nguvu ambazo zingepasua nchi yetu na kuitengabadala ya kuiunganisha ,

Kuharibu nchi yetu kama hiyo sio demokrasia

Na juhudi hizi zilikaribia kufanikiwa.

Ingawa demokrasia inaweza kucheleweshwa kwa kipindi,

Haiwezi kushindwa daima,

Katika ukweli huu, katika Imani hii, tunaamini .

Kwasababu ili mradi macho yetu yanaangalia siku zijazo

Historia ina macho yake kwetu . "

"Nilitaka sana kutumia maneno yangu kuwa hatua ya umoja na ushirikiano," alisema kabla ya sherehe ya kuapishwa kwa rais.

"Ninadhani huu ni ukurasa mpya nchini Marekani ," alieleza kwa furaha, na kuongeza kuwa alitaka kuhusika katika tukio "kupitia umaridadi na ubora wa maneno ."

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Alizaliwa Los Angeles mwaka 1998, Gorman aliugua maradhi ya kigugumizi alipokuwa mtoto, ugonjwa ambao rais mpya wa Marekani pia alikuwa nao alipokuwa mdogo.

Alizaliwa Los Angeles mwaka 1998, Gorman aliugua maradhi ya kigugumizi alipokuwa mtoto, ugonjwa ambao rais mpya wa Marekani pia alikuwa nao alipokuwa mdogo.

"Sasa kuliko wakati mwingine wowote ule, Marekani inahitaji ushairi wa kuapishwa kwa rais,. Lazima tukabiliane na hali hizi halisi kuendelea mbele ," aliliambia gazeti la New York Times.

Alikuwa na kigugumizi kama tu Bw Biden.

"Imenifanya niwe mtumbuizaji na msimuliaji hadithi niliyehangaika ," alisema katika mahojiano ya hivi karibuni na gazeti la Los Angeles Times.

"Wakati unapotakiwa kujifunza kusema sauti na kuwa na hofu ya matamshi, inakupa aina fulani ya utambuzi wa sauti ,na ya uzoefu wa kusikiliza ," aliongeza.

Unaweza pia kusoma:

Gorman alipata umaarufu wa ushairi katika Los Angeles akiwa na umri wa miaka 16 .

Miaka mitatu baadaye, alipokuwa akisomea masomo ya Sociology katika Chuo Kikuu cha Harvard, alikuwa msichana wa kwanza kupata tuzo vijana wanaoghani ushairi.