Virusi vya corona: Afrika Kusini imeondoa marufuku ya uuzwaji wa pombe

Chanzo cha picha, Reuters
Serikali ilisema kuwa ni muhimu kupiga marufuku pombe ili kukabiliana vyema na janga la corona
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amelegeza masharti dhidi ya virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kuruhusu pombe kuanza kuuzwa tena.
Fukwe zitafunguliwa na nyumba za ibada zitafunguliwa kwa kuruhusu idadi ndogo ya watu.
Tangazo hilo limekuja wakati bwana Ramaphosa akifurahia ujio wa chanjo nchini mwake.
Dozi milioni moja za chanjo ya AstraZeneca - zinaweza kubadilisha hali ilivyo ya Covid-19 nchini humo.
Kwa barani Afrika, Afrika Kusini inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya maambukizi ya corona na vifo vilivyotokana na Covid 19.
Tangu janga la corona lianze, zaidi ya watu milioni 1.4 walipata maambukizi ya virusi vya corona na vifo 44,164 vilivyotokana na janga hilo kwa mujibu wa utafiti wa chuo kikuu cha Johns Hopkins.
Mataifa mengi yameiwekea vikwazo vya usafiri Afrika Kusini kwa kuweka marufuku kwa abiria kutoka taifa hilo kuingia nchini mwao ili kuzuia maambukizi ya wimbi jipya la virusi vya corona ambavyo vinadhaniwa kuwa vimeanzia nchini humo na vinavyoshukiwa kuwa sugu hata kwa chanjo iliyopo.
Masharti dhidi ya corona yamepunguzwaje?
Taifa hilo bado litakuwa na marufuku ya kutoka nje kwa muda fulani, lakini baadhi ya makatazo yataondolewa.
Wauzaji wa pombe kwenye maduka wanaweza kuuza kati ya saa nne asubuhi mpaka kumi na mbili jioni, siku ya Jumatatu mpaka Alhamisi na wenye leseni ya kuuza vinywaji kwenye maeneo ya burudani wanaweza kufunga saa nne usiku.
Muda wa marufuku ya kutotoka nje utakuwa saa tano usiku mpaka saa kumi alifajiri.
Tangu janga la corona lianze mnamo mwezi Machi, Afrika Kusini imefungia uuzwaji wa pombe mara tatu.
Chanzo cha picha, Reuters
Wafanyakazi wa afya mjini Pretoria, ndio watakuwa wa kwanza kupata chanjo
Serikali ilisema kuwa ilikuwa muhimu kuchukua hatua hizo ili kupunguza shinikizo kutoka mfumo wa afya.
Makatazo hayo hayajulikani na wengi katika sekta ya vinywaji walisema mamilioni ya watu wako hatarini kupoteza ajira zao.
Katika tangazo la hivi karibuni la mabadiliko, bwana Ramaphosa alisema: "Ninatoa wito kwa watu kunywa pombe wakati wakiwa wanawajibika ili tusiongeze idadi ya maambukizi kutokana na tabia za kizembe."
Aliongeza kuweka utaratibu wa kupumzika, watu 50 ndio wataweza kusali kwa pamoja ndani ya nyumba ya ibada huku watu 100 wakiwa nje.
Fukwe za bahari, mito pamoja na maeneo ya kupumzika na kuogelea yatafunguliwa.
Kwanini sasa?
Bwana Ramaphosa alisema kilele cha wimbi la pili la virusi vya corona limepita sasa, na kwa wastani maambukizi yameshuka ndani ya wiki tatu zilizopita.
Chanzo cha picha, Reuters
Wafanyakazi wakishusha mizigo ya chanjo iliyowasili Afrika Kusini
Rais alisema: "Mabadiliko haya yamewezekana kwa hospitali za majimbo yote kufanya jitihada za ziada."
Mapema alisafiri kwenda uwanja wa ndege wa OR Tambo mjini Johannesburg kupokea dozi za chanjo ya Oxford-AstraZeneca, inayotengenezwa na taasisi ya Serum iliyopo India.
"Kuwasili kwa chanjo hizi kunatoa ahadi kuwa tunaweza kukabiliana vyema na ugonjwa huu ambao umefanya taifa letu na dunia kwa ujumla kuwa na wakati mgumu sana," alisema.
Dozi milioni moja zitatolewa kwa wahudumu wa afya ingawa hakuna tarehe ya utoaji wa chanjo hizo iliyotajwa tayara, ingawa idadi ya chanjo hizo bado ni ndogo kwasababu wafanyakazi wa afya wa nchini humo wanahitaji dozi milioni 1.25.
Taifa hilo limesema bado linafanya majadiliano ya kupata dozi zaidi ya milioni 50 na kuweka lengo la kuchanja watu milioni 40 mwaka huu.
Bwana Ramaphosa amesema ni lazima kila mmoja afikiwe na chanjo hiyo.