Min Aung Hlaing: Jenerali aliyeongoza mapinduzi dhidi ya utawala wa Aung San Suu Kyi Myanmar

Chanzo cha picha, Reuters
Jenerali huo mwenye umri wa miaka 64 amehudumu kipindi chote cha kazi yake katika jeshi hilo lenye ushawishi
Min Aung Hlaing alipanda kwa kasi kupitia safu ya Tatmadaw, jeshi lenye nguvu la Myanmar, lakini kama kamanda mkuu kwa muongo mmoja uliopita pia alikuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa kabla ya mapinduzi ya tarehe 1 mwezi Februari.
Alifanikiwa kudumisha nguvu ya Tatmadaw hata wakati Myanmar ilibadilika kwenda kwenye demokrasia, lakini alipingwa na jumuia ya kimataifa na vikwazo vya kimataifa kwa kujihusisha kwake na mashambulizi yanayodaiwa kuwa ya kijeshi dhidi ya makundi ya kikabila ya wachache.
Wakati Myanmar inarudi kwenye utawala wa kijeshi chini ya uongozi wake, Min Aung Hlaing sasa anaonekana kupanua nguvu zake na kutengeneza mustakabali wa nchi hiyo.
Kupanda vyeo
Jenerali mwenye miaka 64 ametumia taaluma yake katika jeshi , ambalo alijiunga akiwa kadeti.
Mwanafunzi wa zamani wa taaluma ya sheria katika Chuo Kikuu cha Yangon, aliingia kwenye jeshi la ulinzi mwaka 1974 likiwa jaribio lake la tatu.
Kijana mdogo aliendelea kupandishwa mara kwa mara na kupandisha ngazi, mwishowe akawa kamanda wa Ofisi ya Operesheni Maalum-2 mnamo mwaka 2009.
Chanzo cha picha, Reuters
Myanmar ina jeshi la pili kwa ukubwa katika eneo la kusini mashariki mwa bara Asia
Katika jukumu hili, alisimamia operesheni Kaskazini-Mashariki mwa Myanmar, ambazo zilisababisha makundi ya wakimbizi wa kikabila kutoroka wilaya ya Shan na Kokang, karibu na eneo la mpaka na China.
Licha ya madai ya mauaji, ubakaji na uchomaji moto dhidi ya wanajeshi wake, Min Aung Hlaing aliendelea kupanda ngazi na mnamo Agosti 2010 alikua mkuu wa jeshi.
Chini ya mwaka mmoja baadaye, alipewa nafasi ya juu ya jeshi mbele ya majenerali wakuu zaidi, akimrithi kiongozi wa muda mrefu Than Shwe kama kamanda mkuu mnamo Machi 2011.
Wakati Min Aung Hlaing alikua mkuu wa jeshi, mwanablogu na mwandishi Hla Oo - ambaye alisema walikuwa wanafahamiana wakati wa utoto - alimtaja kama "shujaa hodari wa vita na Jeshi katili la Burma", lakini pia alimwita "msomi mkubwa na muungwana" .
Ushawishi wa kisiasa na 'mauaji ya halaiki'
Min Aung Hlaing alianza kipindi chake cha uongozi kama mkuu wa jeshi wakati Myanmar ilibadilika kuwa ya kidemokrasia mnamo mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya utawala wa kijeshi, lakini alikuwa na nia ya kudumisha nguvu ya Tatmadaw.
Ushawishi wake wa kisiasa na uwepo wa mitandao ya kijamii uliongezeka wakati Chama cha Union Solidarity and Development (USDP) kinachoungwa mkono na jeshi kikiongoza serikali.
Mnamo 2016, wakati chama cha Aung San Suu Kyi National League for Democracy (NLD) kilipoingia madarakani, alionekana kuendana na mabadiliko hayo kwa kufanya kazi na kuonekana kwenye hafla za Umma pamoja naye.
Chanzo cha picha, Reuters
Min Aung Hlaing alifurahia kufanya kazi na Aung San Suu Kyi
Licha ya mabadiliko hayo, alihakikisha Tatmadaw inaendelea kushikilia 25% ya viti vya bunge na nafasi nyingine muhimu za baraza la mawaziri linaloshughulikia usalama, wakati ikipinga majaribio ya NLD ya kufanyia mabadiliko katiba na kupunguza mamlaka za jeshi.
Mwaka 2016 na 2017, jeshi lilizidisha ukandamizaji dhidi ya watu wachache wa kabila la Rohingya katika jimbo la Rakhine kaskazini, na kusababisha Waislamu wengi wa Rohingya kukimbia Myanmar.
Mkuu wa jeshi alilaaniwa vikali na jumuia ya kimataifa kwa madai ya "mauaji ya kimbari", na mwezi Agosti mwaka 2018 Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lilisema: "Majenerali wakuu wa jeshi wa Myanmar, pamoja na Amiri Jeshi Mkuu Min Aung Hlaing, lazima wachunguzwe na washtakiwe kwa mauaji ya kimbari kaskazini mwa Jimbo la Rakhine, na pia kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita katika majimbo ya Rakhine, Kachin na Shan. "
Kufuatia taarifa ya baraza hilo, Facebook ilifuta akaunti yake, pamoja na ile ya watu wengine na mashirika ambayo ilisema "wamefanya au kuwezesha ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini".
Marekani ilimwekea vikwazo mara mbili - mwaka 2019 kwa jukumu lake linalodaiwa katika "kusambaratisha jamii za kikabila'' na ukiukaji wa haki za binadamu, na mwezi Julai mwaka 2020 Uingereza pia ilimuwekea vikwazo.
Kuchukua madaraka
Uchaguzi wa mwezi Novemba mwaka 2020 kulishuhudiwa ushindi wa kishindo wa chama cha NLD, kwa mujibu wa takwimu rasmi, lakini chama kinachoungwa mkono na jeshi USDP kiligomea matokeo.
USDP ilitoa madai ya udanganyifu mkubwa wa uchaguzi. Madai hayo yalitupiliwa mbali na tume ya uchaguzi kabla ya kikao cha bunge kilichopangwa kufanyika tarehe 1 Februari ili kudhibitisha serikali mpya.
Uvumi wa kuwepo mapinduzi ulikua wakati wa mvutano kati ya serikali na vikosi vya jeshi. Tarehe 27 Januari Min Aung Hlaing alionya kwamba "katiba itafutwa, ikiwa haitafuatwa", akitoa mfano wa mapinduzi ya kijeshi yaliyotangulia mnamo 1962 na 1988.
Ofisi yake inaonekana ilibadilisha msimamo huo tarehe 30 Januari, ikisema kuwa vyombo vya habari vilitafsiri vibaya maneno ya maafisa wa jeshi kuhusu kufuta katiba.
Hatahivyo, asubuhi ya tarehe 1 Februari, Tatmadaw ilimshikilia Mshauri wa Jimbo Aung San Suu Kyi, Rais Win Myint na viongozi wengine wakuu, na kutangaza hali ya hatari ya mwaka mzima.
Min Aung Hlaing alichukua madaraka yote ya serikali kwa kipindi hiki kama kamanda mkuu.
Mkutano wa Baraza la Kitaifa la Ulinzi na Usalama ukiongozwa naye ulisema utachunguza madai ya udanganyifu na kufanya uchaguzi mpya, ikibadilisha ushindi wa NLD.
Kamanda mkuu baada ya kufikia umri wa kustaafu wa miaka 65 mwezi Julai mwaka huu, lakini sasa amejipa angalau mwaka mwingine madarakani - Wakati Myanmar inakabiliwa na siku zijazo zisizo na uhakika na hali ya hatari, ameimarisha nguvu zake na kuchukua jukumu la nchi hiyo.