Mabaki ya watu wa kale waliowekwa ndimi za dhahabu yapatikana Misri

Inafahamika kwamba waliofariki waliwekwa ndimi za dhahabu ili waweze kuzungumza katika maisha ya akhera

Chanzo cha picha, EGYPTIAN MINISTRY OF ANTIQUITIES

Maelezo ya picha,

Inafahamika kwamba waliofariki waliwekwa ndimi za dhahabu ili waweze kuzungumza katika maisha ya akhera

Wanaakiolojia wamefukua mabaki ya watu wa kale wenye miaka 2,000 wakiwa na ndimi za rangi ya dhahabu Kaskazini mwa Misri, Wizara ya mambo ya kale nchini humo imeeleza.

Timu ya wanaakiolojia hao wa Misri na Dominica wanafanya kazi pamoja katika sinagogi la Taposiris Magna mjini Alexandria .

Ndani yake kulikuwa na mabaki ya watu wa kale ambayo hayakuhifadhiwa vyema.

Inadhaniwa kuwa watu hao waliokuwa wamekufa waliwekewa ndimi za dhahabu ili waweze kuzungumza katika mahakama ya mungu Osiris wa baada ya maisha ya duniani.

Wamisri wa kale waliamini kuwa Osiris ni mungu wa chini ya dunia na huwahukumu waliokufa.

Pia mungu huyo alikuwa kwenye picha katika mapambo yaliyofunikwa kwenye michoro - nyenzo iliyotengenezwa kwa matabaka ya plasta, kitani na gundi - kuzunguka moja ya mabaki hayo ya watu wa kale, kiongozi wa wanaakiolojia Kathleen Martinez wa Chuo Kikuu cha Santo Domingo alinukuliwa na wizara ya mambo ya kale.

Mapambo yaliyopambwa karibu na kichwa cha mabaki ya mtu wa kale wa pili yalionesha taji, pembe na nyoka aina ya swira, aliongeza.

Kwenye kifua, mapambo yalionesha mkufu ambao ulining'iniza kichwa cha falcon - ishara ya mungu Horus.

Chanzo cha picha, EGYPTIAN MINISTRY OF ANTIQUITIES

Maelezo ya picha,

Mabaki ya mwanamke pia yalipatikana

Khaled Abo El Hamd, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya mambo ya kale huko Alexandria, alisema ujumbe wa akiolojia huko Taposiris Magna pia uligundua kinyago cha mazishi ya mwanamke, shada la dhahabu, kinyago cha marumaru cha enzi ya Ugiriki na Kirumi

Wizara ya mambo ya kale imesema sarafu kadhaa za jina na picha ya Malkia Cleopatra VII ambaye awali alipatikana ndani ya sinagogi.

Cleopatra VII alikuwa malkia wa mwisho wa nasaba ya Ptolemaic inayozungumza Kigiriki, akitawala Misri kutoka 51-30 KK. Baada ya kifo chake, Misri ilikuwa chini ya utawala wa Warumi.