Mapinduzi ya Myanmar: Waandamanaji kufungwa hadi miaka 20 chini ya sheria mpya

Waandamanaji wakiinua mabango yaliyo na picha ya Aung San Suu Kyiwakati wa maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi, nje ya Benki kuu ya Myanmar mjini Yangon, Februari 15,2021

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Magari ya kivita yameonekana katika barabara za mji mkuu wa Yangon, Myanmar kwa mara ya kwanza tangu mapinduzi yalipofanyika

Jeshi la Myanmar limewaonya waandamanaji wanaopinga mapinduzi kote nchini humo kwamba huenda wakakabiliwa kifungo cha hadi miaka 20 jela wakizuia vikosi vya jeshi.

Vifungo virefu na faini pia vitapewa wale watakaopatikana na hatia ya kuchochea "chuki na dharau" dhidi ya viongozi wa mapinduzi, jeshi limesema.

Hatua hiyo ya kisheria imetangazwa huku magari ya kivita yakionekana barabarani katika miji tofauti.

Maelfu ya watu wamekuwa wakishiriki maandamano katika siku za hivi karibuni.

Waandamanaji wanashinikiza kuachiliwa huru kwa viongozi wao wanaozuiliwa, akiwemo Aung San Suu Kyi, na kuregeshwa kwa demokrasia Myanmar, ambayo pia inajulikana kama Burma.

Siki ya Jumatatu, wakili wa Bi Suu Kyi alisema kuwa amezuiliwa kwa siku mbili zaidi. Kisha atafunguliwa mashtaka mahakamani kupitia mtandaoni katika mji wa Nay Pyi Taw siku ya Jumatano, Khin Maung Zaw aliongeza kusema.

Bi Suu Kyi alikamatwa pamoja na maafisa wengine wa serikali yake Februari mosi, lakini kuzuiliwa kwake kulitarajiwa kufikia kikomo Februari 15, kulingana na shirika la habari la Reuters.

Mashataka dhidi yake ni pamoja na kuwa na kifaa chamawasiliano kinyume cha sheria - walkie-talkie inayotumiwa na maafisa wake wa usalama .

Chama chake kilipata ushindi wa kishindo Novemba iliyopita, lakini jeshi linadai kulikuwa na wizi wa kurabila kutoa ushahidi wowote.

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Waandamanaji walikusanyika katika barabara zilizopelekwa magari ya kivita karibu na Benki kuu ya Yangon

Kuna dalili gani za msako?

Jeshi limeongeza uwepo wake kuashiria kuwa huenda kukafanyika msako wa kuwakamata wanaopinga mapinduzi.

Jeshi pia limetangaza msururu wa mabadiliko ya kisheria, kuweka adhabu ya vifungo virefu na faini kwa mtu yeyote atakayepatikana akieneza chuki dhidi ya viongozi wa kijeshi, "kwa kutumia maneno, iwe ni kutamka au maandishi, au kwa ishara, au kwa uwakilishi unaoonekana".

Taarifa iliyowekwa katika tovuti ya jeshi siku ya Jumatatu, inasema kuwa watu watakaowazuia wanajeshi kutekeleza wajibu wao huenda wakakabiliwa na kifungo cha miaka 20 gerezani, na wale watakaochochea ghasia na vurugu za umma huenda wakafungwa jela kati ya miaka mitatu na saba.

Taarifa hizo zinajiri saa kadhaa baada ya mtandao kurejeshwa.

Kampuni za simu nchini humo zimesema mawasiliano ya intaneti yamezimwa kuanzia saa saba mpaka saa tatu majira ya saa za huko.

Jeshi lilisitisha sheria inayokataza kuzuia mtu zaidi ya saa 24 na kumchunguza maliza zake.

Waandishi watano ni miongoni mwa watu waliyokamatwa katika mji wa Myitkyina lakini baadaye waliachiwa huru.

Maelezo ya video,

Apiga picha akifanya mazoezi bila kujua serikali yake inapinduliwa

Daktari mmoja katika hospitali ya Nay Pyi Taw ameiambia BBC kuwa vyombo vya usalama vilikuwa vinawavamia watu nyumbani kwao majira ya usiku.

"Bado nina wasiwasi kwasababu marufuku ya kutotoka nje yapo kuanzia saa mbili mpaka saa kumi alfajiri na ndio muda ambao polisi wanatumia mwanya wa kukamata watu kama sisi," alisema daktari, ambaye jina lake limehifadhiwa kwasababu za usalama.

"Jana waliiba nyumbani kwangu, waliwavamia watu kinyume na sheria, Ndio maana nina wasiwasi."

Afisa wa ubalozi wa Marekani mjini Yangon amewataka raia wa Marekani kutotoka nje wakati huo wa marufuku ya kutoka nje.

Siku ya Jumamosi, jeshi liliwakamata wanaharakati saba wa kampeni za upinzani na kuonya umma kutowasaidia wanaharakati kutoroka ili wasikamatwe.

Picha za Video zikionesha watu wakipiga kelele na kugonga masufuria wakiwaonya jirani zao kuhusu uvamizi wa jeshi majira ya usiku.

Ofisi ya ubalozi wa Marekani mjini Yangon imewaomba raia wa Marekani kusalia majumbani mwao saa za kafyu.

Myanmar - mambo ya msingi

  • Myanmar, inajulikana pia kama Burma, ilikuwa chini ya utawala wa kijeshi kuanzia mwaka 1962 mpaka 2011
  • Harakati za ukombozi zilianza mwaka 2010, na kulifanya taifa hilo kuwa na uchaguzi huru mwaka 2015 na mwaka uliofuata serikali ya taifa hilo kuanza kuongozwa na kiongozi nguli wa upinzani Aung San Suu Kyi
  • Mwaka 2017, mgogoro mkubwa uliibuliwa na jeshi la Myanmar katika eneo la waislamu wa Rohingya ambapo mamilioni ya watu walikimbilia mpakani mwa Bangladesh, jambo ambalo baadaye Umoja wa Mataifa UN iliita kuwa "mfano wa kitabu cha utakaso wa ukabila"
  • Aung San Suu Kyi na serikali yake ilipinduliwa na jeshi Februari 1 February kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Novemba.