Virusi vya Corona: Rais Magufuli asema 'Hatujazuia matumizi ya barakoa'

Magufuli

Chanzo cha picha, AFP

Rais wa Tanzania John Magufuli amesema serikali yake haijamzuia mtu yeyote kuvaa barakoa, japo anashauri matumizi ya barakoa zilizotengenezwa nchini akisema anaamini baadhi ya zile zinazoagizwa kutoka nje sio salama.

Bw. Magufuli alisema hayo mapema siku ya Jumapili alipokuwa akiwahutubia waumini katika kanisa moja jijini Dar es Salaam. Tamko hilo linaashiria kuwa rais amebadili msimamo wake kuhusu ugonjwa wa Covid 19.

Kabla ya hapo, kiongozi huyo alisikika akibeza hadharani matumizi ya barakoa akisema nchi yake imefanikiwa kutokomeza maambukizi ya corona.

Lakini sasa kauli hiyo inaonekana kubadilika.

Akizungumza na mamia ya waumini kanisani, rais ailitoa wito kwa wananchi wenzake kuendelea kuchukuwa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa corona kama wanavyoelekezwa na wataalamu wa afya, akisisitiza kwamba serikali yake haijamzuia mtu yeyote kuvalia barakoa.

Bw. Magufuli pia amewahimizi Watanzania kutumia njia za kiasili kukabiliana na magonjwa ya kupumua ukiwemo ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kujifukiza (kupiga nyungu)

Tamko la rais linakuja wakati ambapo Tanzania imeendelea kuripoti vifo vya watu kadhaa mashuhuri miongoni mwao wandani wake wa karibu, japo kilichosababisha vifo vyao hakijawahi kuhusishwa rasmi na ugonjwa wa Covid 19.

Maelezo ya picha,

Ibada ya mazishi ya Katibu Mkuu Kiongozi mhandisi Balozi John Kijazi

Leo Jumapili pia ndio siku ya mwisho ya maombi ya siku tatu kwa taifa iliyotangazwa na Rais Magufuli kuomba viongozi wa kidini kufanya sala maalum ya kukinga nchi kutokana na maambukizi ya corona.

Huku hayo yakijiri, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa wito kwa mamlaka nchini Tanzania kuanza kutoa takwimu ya walioambukizwa Covid 19 nchini humo. WHO, linasema kuwa hatua hiyo itasaidia kuwalinda Watanzania na wale wanaotangamana nao.

Pia unaweza kusikiza

Maelezo ya sauti,

Magufuli: Unaweza ukafa kwa malaria,unaweza ukafa kwa kansa, ukafa kwa magonjwa mengine