Mahojiano ya Oprah na Meghan na Harry: Kwanini mwana wa mwanamfalme Harry na Meghan, Archie sio mwanamfalme?

Chanzo cha picha, Reuters
Duke na Duchess wa Sussex wakiwa na mwana wao Archie
Katika mahojiano na Oprah Winfrey, Meghan Markle Duchess wa Sussex alisema kwamba alipokuwa na ujauzito , kulikuwa na madai kuhusu siku za usoni za mwanawe ikiwemo wadhfa au taji atakalopatiwa.
Walikuwa wanasema kwamba hawakutaka awe mwanamfalme au Bintimfalme suala ambalo ni tofauti na itifaki ya ufalme huo, alisema.
Je itifaki ya ufalme huo inasemaje?
Sheria kuhusu ni nani anayepaswa kuwa mwanamfalme na pia kuitwa muheshimiwa wa ufalme zinajiri kutoka kwa barua ya hati miliki iliotolewa na mfalme George wa tano mwezi Novemba 1917.
Barua zenye haki miliki ni nakala rasmi ambazo huonekana kama barua ya wazi kutoka kwa ufalme. Hutumika kufanya tangazo au kumpatia mtu taji au wadhfa wa Kifalme.
Katika barua hiyo ya mwaka 1917, Mfalme George wa tano alitangaza kwamba vitukuu wa ufalme huo hawatakuwa wanawafalme , isipokuwa mtoto mkubwa wa mwana mkubwa wa mwanamfalme wa Wales.
Katika hali ya sasa , hiyo ina maana kwamba Mwanamfalme George , mtoto mkubwa wa mwanamfalme William , atakuwa mwanamfalme moja kwa moja lakini sio Archie , licha ya kwamba wote ni vitukuu wa malkia. Chini ya itifaki, watoto wa mwanamflame George , Charlotte na Louis pia wasingepatiwa wadhfa huo.
Lakini mnamo mwezi Disemba 2012, malkia pia alitoa barua rasmi iliosema kwamba wana wote wa mwanamfalme William watapewa wadhfa wa mwanamfalme na bitimfalme ili kupewa jina la heshima.
Pia unapokuwa mwanamfalme na Bintimfalme lazima uwe umetoka upande wa uume, ikimaanisha kwamba wana wa bintimfalme Anne hawatapata taji hilo licha ya kuwa wajukuu wa malkia Elizabeth .
Na je taji la Archie?
Kulingana na barua hiyo ya mwaka 1917, Archie ana haki ya kuwa mwanamfalme lakini bado.
Wana wa Harry na Meghan , watalazimika kusubiri hadi Mwanamfalme Charles , mrithi wa ufalme huo, kuwa mfalme hatua mbayo itawafanya watoto wao kuwa wajukuu wa mfalme huyo na hivyobasi kupewa taji la kuwa wanawafalme.
Hii ndio sababu wana wa kike wa mwanamfalme Andrew - Beatrice na Eugenie walikuwa na taji la mabintimfalme toka kuzaliwa kwao kwa mfano. Mwanamfalme Harry na Mkewe Meghan walikuwa wanajua kuhusu itifaki hii.
Katika mahojiano na Oprah alizungumzia kuhusu azimio la mfalme George wa tano na George wa sita kwamba mwanawe Archie atakuwa mwanamfalme wakati babake mwanamfalme Harry { Charles} atakapokuwa mfalme.
Lakini aliendelea kusema kwamba aliambiwa wakati alipokuwa na uja uzito kwamba wanataka kubadilisha azimo hilo kwa Archie ili asiweze kuwa mwanamfalme.
Hakutoa maelezo yoyote zaidi kuhusu hilo na kwamba kasri la Buckingham halijatoa tamko lolote kuhusu madai yake.
''Niliona kwamba Meghan alitaja kwamba kulikuwa na mpango wa kupunguza ustahiki na nafikiria hilo linatokana na matamshi ya mwanmfalme wa Wales kwamba kiwango cha familia hiyo ya ufalme inahitaji kupunguzwa'' , alisema Bob Morris kutoka kwa kitengo cha katiba UCL.
Hatahivyo hajatoa maelezo jinsi hilo linavyopaswa kushughulikiwa.