China na Urusi zimetangaza mpango wa kujenga kituo cha anga za mbali mwezini

An image of the moon

Chanzo cha picha, PA Media

Maelezo ya picha,

Picha ya mwezi

Shirika la anga za mbali la Urusi Roscosmos limesema kuwa limesaini makubaliano na kituo cha taifa la China cha utawala wa anga za mbali ili kutengeneza vifaa vitakavyosaidia kufanya utafiti wa sakafu ya mwezi, kwenye uzio (orbit) au eneo lote la mwezi.

Taarifa kutoka mashirika ya anga za mbali ya nchi zote mbili inasema utafiti huo utatumiwa na mataifa mengine pia.

Hii inakuja wakati Urusi ikijiandaa kusherehekea miaka 60 tangu chombo chake cha kwanza kabisa kutumwa katika anga za mbali.

Kituo cha kimataifa cha Kisayansi cha mwezi kitafanya utafiti mkubwa wa kisayansi ikiwa ni pamoja na kuvumbua na utumiwaji wa mwezi, imesema taarifa ya mashirika ya nchi hizo mbili.

"China na Urusi zitatumiwa uzoefu wao kwa pamoja katika sayansi ya anga za mbali, utafiti na kutengeneza na kutumia vifaa vya anga za mbali na teknolojia ya anga za mbali kushirikiana kutengeneza ramani kwa ajili ya kujenga kituo cha kisayansi cha utafiti wa kisayansi cha mwezini ," taarifa hiyo iliyoandikwa kwa lugha ya Mandarin ilisema.

Iliongeza kuwa nchi zote mbili Urusi na China zitashirikiana katika kupanga, kuunda, kutengeneza na katika shughuli za utafiti katika kituo hicho.

Chen Lan, mchambuzi ambaye aliyebobea katika masuala ya mpango wa anga za mbali wa China, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba mradi huo ni "mafanikio makubwa".

"Huu utakuwa ni mradi mkubwa sana wa ushirikiano wa kimataifa wa anga za mbali kwa Uchina, kwa hiyo ni muhimu," alisema.

China imechelewa kiasi inapokuja katika suala la uvumbuzi wa anga za mbali, lakini mwezi Disemba mwaka jana chombo chake cha anga za mbali kilifanikiwa kufika mwezini na kuleta mwamba na ''udongo'' kilichouchukua kutoka mwezini.

Wakati ule tukio hilo liliangaliwa kama dhihirisho la kuongezeka kwa uwezo mwingine wa nchi hiyo katika anga za mbali.

Urusi ambayo ilikuwa ya kwanza kufanya uvumbuzi wa anga za mbali, imepitwa na China na Marekani katika miaka ya hivi karibuni.

Mwaka jana ilipoteza ukiritimba wake wa kuwapeleka wataalamu wa anga za mbali katika kituo cha kimataifa cha anga za mbali kufuatia chombo cha SpaceX kufanikiwa kuondoka.

Marekani imetangaza mipango ya kurejea mwezini ifikapo mwaka 2024.

Mpango huo unaoitwa Artemis, utamuwezesha mwanamke na mwanaume kutembea katika sakafu ya mwezi ambapo itakua mara ya kwanza kwa binadamu kutembea mwezini tangu mwaka 1972.