Fatgbems: Kituo cha mafuta chauza maji badala ya mafuta Nigeria

"Fatgbems yauza maji badala ya mafuta

Chanzo cha picha, Screenshot

Video ya kituo kimoja cha Mafuta cha Fatgbems nchini Nigeria imesambazwa sana katika mitandao ya kijamii kwa kuuza maji badala ya Mafuta ya petroli kwa wateja wake, kulingana na BBC Pidgin.

Video hiyo ilisambaa baada ya baadhi ya wateja kujitokeza na kuanza kuwashutumu wamiliki wa kituo hicho kwa wizi huku baadahi ya wamiliki wa magari wakionyesha jinsi maji yanavyotoka katika injini zao za magari.

Lakini usimamizi wa kituo hicho cha Fatgbems ulitoa taarifa ukisema kwamba maji yaliingia katika Matangi yake ya kuhifadhi Mafuta.

Kulingana na taarifa, wamiliki wa kituo hicho wamesema kwamba ni bahati mbaya kwa tukio kama hilo na kwamba lengo lao ni kufanya biashara na sio kuwauzia wateja wao bidhaa zenye ubora wa chini.

''Tunawaomba wateja wetu na umma kwa jumla kuwa na subra, kwasababu tumeanza kuchukua hatua ili kuangazia malalamishi ya wateja wetu ambao wameathiriwa''.

Tukio hilo lilifanyika tarehe 14 mwezi Machi huko Abeokuta, kusini magharibi mwa Nigeria, wakati ambapo bei ya mafuta ilipanda katika baadhi ya vituo vya Mafuta nchini humo.

Shirika la kitaifa la Mafuta nchini humo lilisisitiza kwamba hakuna kuongeza bei ya Mafuta mwezi huu.

Hatua hiyo inajiri baada ya bodi ya kudhibiti bei ya bidhaa za Mafuta PPPRA kuchapisha bei mpya ya Mafuta katika mtandao wake siku ya Alhamisi.

Suala la Mafuta kuwa na maji sio jambo geni nchini Nigeria na hutokea mara kwa mara wakati kuna upungufu wa bidhaa hiyo.

Baadhi ya magari yaliharibika injini punde tu baada ya kuuziwa maji badala ya Mafuta.