Kifo cha John Magufuli: Tanzania bila kiongozi huyu kipi kifuatacho?

  • Rashid Abdallah
  • Mchambuzi
Jeneza la Magufuli
Maelezo ya picha,

Jeneza la Magufuli

Machi 19, 2021 cheo cha Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kimebadilika baada ya kula kiapo Ikulu jiji Dar es Salaam na kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mama Samia ni Rais wa sita akiendeleza miaka mitano ya utawala wa Rais John Pombe Joseph Magufuli aliyefariki kwa tatizo la moyo Machi 17, 2021. Kwa mujibu wa katiba kwa sababu Samia ataongoza zaidi ya miaka miwili huu unahesabiwa kuwa muhula wa kwanza kwake.

Samia amekuwa Rais wa kwanza mwanamke kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa wengine ni Rais wa kwanza kutokea upande mwingine wa Muungano, kwa maana ya Zanzibar.

Nje ya hapo ni Rais wa pili mwanamke katika jumuiya ya Afrika Mashariki, akitanguliwa na mwendazake Bi Sylvie Kinigi aliyekuwa Rais wa Burundi kutoka Oktoba 1993 hadi Februari 1994.

Tanzania inaandika historia mpya. Katika historia hii jambo kubwa linalojadiliwa ni namna gani Rais mpya ataiongoza nchi kutoka yale mazuri na mabaya ya utawala wa marehemu John Pombe Magufuli.

Magufuli wa sura mbili

Unaweza kuukosoa utawala wa Magufuli kwa mambo mengi lakini huwezi kuacha kuihusudu nia yake ya dhati ya kukuza uchumi wa nchi na kuiletea Tanzania maendeleo.

Uzalendo wake lilikuwa ni jambo lisilo na shaka kabisa. Alikuwa mkali dhidi ya watumishi wake pindi akiona wanafanya mambo ndivyo sivyo. Wala hakusita kufukuza kazi na kuweka wengine.

Amefariki huku nyuma akiacha miradi mingi mikubwa ambayo ikikamilika, itaiweka Tanzania katika ramani nyingine. Kuanzia ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme, miradi ya usafiri. Alikuwa na kitu kubwa ya maendeleo katika huduma za kijamii.

Alivutia wengi kwa msimamo wake usioyumba dhidi ya rushwa na ufisadi na matumizi mabaya ya mali za umma. Daima aliwaza kuitoharisha nchi na vitendo hivyo ambavyo vilirudisha nyuma kasi ya maendeleo.

Ni Magufuli huyo huyo aliyekuwa na sura ya pili, ambayo iliakisi zaidi malalamiko mengi na ukosoaji dhidi ya utawala wake ndani na nje ya Tanzania.

Kuanzia ukandamizaji wa demokrasia na uhuru wa kisiasa. Vyama vya upinzani havikuwa na sauti, havikuweza kutumia haki ya kikatiba kuandamana, au kufanya mikutano ya hadhara popote watakapo.

Wakati fursa hiyo ikikosekana Chama tawala cha Mapinduzi (CCM), kiliendelea kupeta. Magufuli akiwa Mwenyekiti wa chama alizunguka nchi nzima akifanya mikutano na kukutana na wananchi.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama, Dkt Bashiru Ali na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa Humphrey Polepole waliripotiwa mara kadhaa wakiendsha mikutano ya hadhara bila matatizo yoyote.

Ukandamizaji huo ulimea na kukua. Kiasi cha hata mikutano ya ndani ya vyama vya upinzani kuzuiwa au kuvamiwa mara kwa mara ya Jeshi la Polisi na kukamata viongozi wao.

Ni wakati ambao Tanzania ilishuhudia kesi nyingi dhidi ya viongozi wa upinzani, wakituhumiwa kwa uchochezi na mambo mengine. Tuhuma ambazo wenyewe waliamini zilichochewa kisiasa.

Uhuru wa kujieleza ulitatizika, sio katika mitandao ya kijamii tu hata kwa vyombo vya habari. Vipo vilivyofungiwa, kupigwa faini huku waandishi na wahariri wao wakikumbwa na homa kubwa ya hofu iliyowalazimisha wengi kukaa kimya.

Katika utawala wake kulishuhudiwa kukithiri kwa matukio ya watu kutekwa, kushambuliwa na kufunguliwa kesi hasa wale ambao walitazamwa kama ni wakosoaji. Kwa maneno mafupi hakukuwa na uvumilivu juu ya wakosoaji.

Uchaguzi wa Oktoba 2020 ulitoa sura mpya ya namna gani utawala wake haukuhitaji upinzani. Uchaguzi uliokumbwa na uvunjifu wa haki za binaadamu, kamatakamata, taarifa za wizi wa kura. Ndio ambao ulitoa ushindi mkubwa kwa CCM. Ushindi ulioacha wengi midomo wazi.

Maswali bila majibu

Mama Samia ni mzoefu wa siasa za Tanzania, alihudumu tangu akiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kabla hajafika kuwa makamu wa Rais.

Ingawa uzoefu huu bado hautoi jawabu juu ya namna gani ataiendesha Tanzania. Nchi ambayo bado inahitaji kiongozi imara kupinga ufisadi, kusimamia vyema rasilimali za nchi na miradi. Sambamba na kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma na kuleta maendeleo.

Swala la demokrasia iliyokuwa kitandani mahututi, ni mtihani mkubwa kwa utawala wake. Je, atazidi kuikaza kamba ya shingo iliyoachwa na mwendazake Magufuli dhidi ya vyama vya upinzani?

Au atafungua mlango wa kisiasa na mazungumzo na vyama hivyo, ili kujadili mambo muhimu ikiwemo Tume Huru ya uchaguzi na uhuru wa kisiasa! Ni kusubiri na kuona.

Uhuru wa kujieleza na wa habari ambao umedumaa. Kuondoka kwa Magufuli kutaleta ahueni kwa waandishi, vyombo vyao na mitandao ya kijamii?

Watanzania wana hamu ya kusikia msimamo wa Rais mpya juu ya mchakato wa Katiba mpya ambao Magufuli aliufungia katika kabati na kuusahau. Akieleza kwamba sio kipau mbele chake.

Tanzania itatakiwa kutathmini upya heshima yake ambayo imeporomoka kimataifa. Kulikochangiwa na sera za kikandamizaji katika mambo mbali mbali. Kiasi cha mataifa makubwa kujadili kuiwekea vikwazo.

Je, kuna matumaini?

Bila shaka ni mvinyo mpya, ila chupa ni ileile. Ingawa hilo haliwezi kuondoa dhana njema kuhusu Mama Samia. Kwa tabia yake ya asili ya upole. Wengi hawatarajii utawala utakaojiendesha kwa ujuba na ubabe.

Ikiwa uvumi kuwa Uviko-19 ndio sababu ya kifo cha Magufuli. Huenda hilo likamsukuma kubadilisha sera na misimamo. Ili kuziacha zile sera zenye utata za utawala uliopita.

Kulikosekana ukweli na uwazi kuhusu nani kaambukizwa, nani kafariki. Uviko-19 ipo au la. Watanzania walikuwa vitendawili vingi visivyo na jawabu juu ya ugonjwa huo. Nchi iligeuka na kuwa kituko cha dunia.

Wakati akiwa Makamu hakuonesha upinzani wowote wa wazi kwa sera yoyote iliyokosolewa ya utawala wa Magufuli. Kwa sasa anao uwezo wa kubadilisha upepo wa mambo, ikiwa aliamini kuna mambo hayakutendwa sawa.

Kwa faida ya kuandika historia nzuri. Itamlazimu kuchagua kuendeleza mazuri ya utawala uliopita na bila kuogopa kuyapa kisogo yale yaliyoleta ukakasi na ukosoaji mkubwa.