Kifo cha Magufuli: Je uhusiano wake na viongozi wa dini tofauti ulikuwaje Tanzania?

  • Aboubakar Famau
  • BBC Africa, Tanzania
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mfuti wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ally na Balozi wa Mororcco nchini Tanzania Abdellah Benyryane baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti mkuu wa Baraza Kuu la Waisalmu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohamed wa Sita wa Morocco Kinondoni jijini Dar es Salaam

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzznia

Maelezo ya picha,

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Mfuti wa Tanzania Sheikh Aboubakary Zubeiry Ally na Balozi wa Mororcco nchini Tanzania Abdellah Benyryane baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa msikiti mkuu wa Baraza Kuu la Waisalmu Tanzania (BAKWATA) unaojengwa kwa ufadhili wa Mfalme Mohamed wa Sita wa Morocco Kinondoni jijini Dar es Salaam

Kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kinaendelea kuleta simanzi ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Katika ibada maalumu iliyojumuisha viongozi wa dini mbalimbali huko wilayani Chato, viongozi hao walimuelezea Magufuli kama kiongozi aliyegusa nyoyo za watu madhehebu yote ya dini huku wakikumbuka mara kwa mara alivyokuwa akiwaita na kuzungumza nao.

Rais Magufuli ambae alikuwa Mkristo wa dhehebu la Kikatoliki lakini ni dhahiri kwamba mapenzi yake kwa dini nyengine yalikuwa makubwa.

Katika uzinduzi wa msikiti mkubwa uliojengwa kwa ufadhili ya mfalme wa sita wa Morocco jijini Dar es Salaam, rais Magufuli alisisikika akisema maneno mazito.

Rais Magufuli alisimulia jinsi alivyomuomba mfalme wa sita wa Morocco amjengee msikiti mkubwa kuliko yote Tanzania.

"Tulipobaki na mfalme wa sita wa Morocco nikamwambia naomba unifanyie kitu kimoja ambacho ninaamini moyo wangu utaguswa na nitakikumbuka katika maisha yangu hata nikitangulia mbele ya haki," alisema rais Magufuli wakati wa uhai wake.

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli akiwa katika Ibada kanisani

Leo hii ikiwa imebaki siku moja kabla kufika hapa mjini Chato ambapo pindo alipozaliwa na kukulia, lakini pia ndipo atakapozikwa, viongozi hawa wa dini waliohudhuria ibada maalumu ya kumuombea wanasema Magufuli kiongozi wa kisiasa ambae alikuwa hafanyi kitu ukiwemo kuanza kwa mikutano ya kisiasa bila dua au sala.

Baadhi yao wanasema,katika kipindi cha uongozi wake, ndio ilikuwa wakati pekee ambapo viongozi wa dini walijiona kuwa karibu na serikali.

Imani yake katika dini ilikwenda mbali zaidi. Katika mapambano dhidi ya janga la corona, mara kadhaa aliwahimiza wananchi wake kuomba ili Mungu awaepushe na jana hilo.

Msimamo wake huu, ulionekana kituko katika jumuia ya kimataifa katika kukabiliana na ugonjwa huo.

Hata hivyo aliwashangaza watu zaidi pale aliwataka viongozi wa dini kufanya maalumu kumshukuru Mungu kwa kutokomeza Corona nchini Tanzania.

Chanzo cha picha, Ikulu Tanzania

Maelezo ya picha,

Rais Magufuli alishiriki misa ya sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam

Sheikh Abdurahman Ismail Abdallah, sheikh mkuu wa wilaya ya Chato anasema Magufuli ni rais pekee ambae alikuwa na ujasiri wa kuitisha mchango wa kujenga msikiti ndani ya kanisa.

"Alikuwa ni mtu wa tofauti sana. Kwanza aliwapenda viongozi wa dini lakini pia aliwathamini, na viongozi nao wakampenda na kumthamini. Huyu ni kiongozi ambae alikuwa na ujasiri wa kipekee. Aliweza kuchangisha ujenzi wa msikiti kanisani," amesema sheikh Abdurahman.

Mchungaji Vincent Sylvester kutoka kanisa la PAG, Buserere, anasema rais Magufuli alikuwa kiongozi wa kitaifa ambae alitumia nafasi yake kuwaunganisha watanzania wa matabaka wote.

Nae mchungaji Zephrine Kahigwa kutoka kanisa la Tanzania Assemblies of God, amesema maombi yanayoendelea katika maeneo mbalimbali ni ishara tosha kwamba rais Magufuli alipendwa na watu wa dini zote