Makombora ya Korea Kaskazini: Biden anasema uzinduzi wa makombora ya masafa mafupi 'sio uchokozi'

Bwana Biden alikuwa akizungumza kwa vyombo vya habari siku ya jumanne usiku katika Ikulu ya Whitehouse

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Bwana Biden alikuwa akizungumza kwa vyombo vya habari siku ya jumanne usiku katika Ikulu ya Whitehouse

Rais wa Marekani Joe Biden amesema haoni kama uzinduzi wa Korea Kaskazini wa makombora ya masafa mafupi -kwa mara ya kwanza tangu aingie mamlakani -kama kitendo cha uchokozi.

Bw Biden aliongeza kuwa maafisa wa ulinzi waliutaja uzinduzi wa makombora hayo kuwa "shughuli ya kawaida".

Korea Kaskazini inasemekana ilifyatua makombora ambayo sio ya masafa marefu , ambyo hayakiuki maazimio ya Umoja wa Mataifa mwishoni mwa juma.

Tukio hilo lilitokea baada ya utawala wa Pyongyang kuikosoa Marekani na Korea Kusini kwa kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi.

Hii inakuja huku utawala wa Biden ukijaribu kuanzisha ushirikiano wa kidiplomasia na Korea Kaskazini.

Ufyatuaji wa makombora hayo, ambao uliripotiwa kwanza na vyombo vya habari vya Marekani ,umethibitishwa na maafisa wa wizara za ulinzi za Marekani na Korea Kusini.

Korea Kusini ilisema kuwa makombora hayo ya masafa mafupi yalifyatuliwa ndani ya bahari ya Manjano siku ya Jumapili kutoka eneo la Onchon ndani ya Korea Kaskazini.

Akijibu maswali ya waandishi wa habari Jumanne usiku, Bw Biden alisema : "Tumefahamu kuwa hakuna chochote kilichobadilika ."

Alipoulizwa iwapo anachukulia jaribio la Korea Kaskazini kama uchokozi alisema: "Hapana, kulingana na Wizara ya ulinzi, ni jambo la kawaida. Hakuna kilichobadilika katika kile walichokifanya."

Maazimio ya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, ambayo yamesababisha kuwekewa kwa vikawazo vikali dhidi ya Korea Kaskazini, yameizuia Pyongyang kufyatua silaha zinazotisha kama vile makombora ya masafa marefu.

Haya sio makombora ya "moto na ghadhabu " Kutoka Korea Kaskazini.

Ni kweli kwamba kila jaribio la makombora linalofanywa na Pyongyang husaidia kuboresha uwezo wake wa kijeshi na kwamba wakati wote huwa ni jambo la kutia hofu kwa jamii ya kimataifa.

Lakini jaribio la makombora ya masafa mafupi halivunji vikwazo vya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na Korea Kaskazini ina silaha kubwa zaidi katika ghala lake kama inataka kweli kuuchokoza utawala wa Biden.

Kile ambacho maafisa wa Ikulu ya White House wanakiangazia pamoja na washirika wao ni tathmini ijayo kuhusu sera ya Korea Kaskazini

Miongo ya vikwazo na mikutano kati ya Donald Trump na Kim Jong Un vimeshindwa kuizuia Pyongyang kutengeneza silaha kubwa na hatari za nyuklia.

Kwa hiyo, Rais Biden inawezekana sana huenda amepuuza jaribio la hivi karibuni la makombora kwa sababu nzuri - kuna changamoto kubwa zaidi ijayo.

Maafisa wa ngazi ya juu wa Marekani wamesema kando kwamba wamechukulia hatua hiyo kama ''shughuli ya kawaida zaidi ya kijeshi iliyofanywa na Korea Kaskazini'' .

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Rais Kim Jong un wa Korea Kaskazini

Waliongeza kuwa wako katika "hatua za mwisho" za tathmini ya sera ya Korea Kaskazini na wanapanga kuwakaribisha washauri wa masuala ya usalama kutoka mataifa ya Japan na Korea Kusini kwa ajili ya mazungumzo hivi karibuni.

Serikali ya Marekani awali ilisema kuwa imekuwa ikijaribu kwa wiki kadhaa kufanya mawasiliano kidiplomasia na korea Kaskazini.

Pyongyang bado haijatambua kuwa Biden sasa yuko mamlakani , na nchi mbili zimesalia kuwa na uhasama kuhusiana na mipango ya Korea Kaskazini ya nyuklia na makombora ya ballistic.

Wakati wa kapeni za uchaguzi, Bw Biden alimuita Bw Kim "mhuni " na akasema udhibiti wa nyuklia dhidi ya Korea Kaskazini utatakiwa kufanyika kabla ya kulegezwa kwa vikwazo vya kiuchumi vya Umoja wa Mataifa na Marekani.