Mzozo wa Tigray: Waziri Mkuu wa Ethiopia Ahmed Abiy akiri kuwa vikosi vya Eritrea viko ndani ya Tigray

Waziri Mkuu wa Ethioipia Abiy Ahmed alisema kwamba wanajeshi watakaopatikana

Chanzo cha picha, Getty Images

Kwa mara ya kwanza Waziri mkuu wa Ethiopia amekiri kuwa wanajeshi wa nchi jirani ya Eritrea wamekuwa ndani ya jimbo la Tigray kufuatia kuibuka kwa mzozo jimboni humo mwezi Novemba.

Kwa miezi kadhaa nchi zote mbili zimekuwa zikikanusha kwamba vikosi vya Eritrea vilivuka mpaka na kuingia Tigray.

Abiy Ahmed aliwaambia wabunge kwamba vikosi vya Eritrea vilikuja kutokana na hofu kwamba wangeshambuliwa na wapiganaji wa Tigray.

Mzozo ulianza baada ya wapiganaji wa Tigray People's Liberation Front (TPLF) kuziteka ngome za kijeshi katika jimbo hilo.

TPLF kimekuwa ni chama tawala katika jimbo hilo la kaskazini mwa Ethiopia, lakini kilikuwa na uhasama mkubwa na Bw Abiy kuhusu hali ya baadae ya mfumo wa shirikisho wenye misingi ya kikabila na jukumu lake katika serikali.

Maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao katika jimbo la Tigray katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.

Ingawa TPLF kiling'olewa madarakani mwishoni mwa mwezi Novemba na Bw Abiy kutangaza kwamba mzozo umeisha, mapigano bado yanaendelea katika baadhi ya sehemu za jimbo hilo.

Uhusika wa Eritrea katika mzozo ulikuwa ni upi?

Bw Abiy, ambaye ni mshindi wa zamani wa Tuzo ya Amani ya Nobel, hakukiri kwamba wanajeshi wa Eritrea walipelekwa katika miji ya Ethiopia.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanadai wanajeshi wa Eritrea walifanya maasi katika miji kama vile Aksum, ambayo ni pamoja na mauaji ya raia wasiokuwa na silaha, kuwabaka wanawake na uporaji mkubwa wa mali za umma na za kibinafsi.

Waziri mkuu aliliambia bunge kwamba Eritrea ilisema kuwa wanajeshi wake wanachukua hatua kulinda mpaka na kuchukua eneo ambalo lilikuwa limetelekezwa na wanajeshi wa Ethiopia waliokua wamekwenda kupigana.

Alisema kuwa alikuwa amezungumza na maafisa wa Eritrea kuhusu madai kwamba wanajeshi wa Eritrea walitekeleza maasi katika jimbo la Tigray.

"Baada ya wanajeshi wa Eritrea kuvuka mpaka na kuendesha shughuli zao ndani ya Ethiopia, uharibifu wote ambao jeshi hilo liliufanya kwa watu wetu haukubaliki ," Shirika la habari la AFP lilimnukuu Bw Abiy akisema.

Ukurasa wake wa Twitter uliongeza kuwa :''Ripoti zinaashiri kuwa maasi yametendeka katika jimbo la Tigray .

"Licha ya propaganda za TPLF za kutia chumvi, mwanajeshi yeyote aliyehusika na ubakajiwa wa wanawake wetu na kuipora jamii katika jimbo atawajibishwa kwasababu kazi yao ni kulinda."

Kwa waangalizi wengi imekuwa wazi kwa muda mrefu kwamba Bw Abiy alifanya makubaliano na rais wa Eritrea Isaias Afwerki kujumuisha vikosi na kumuondoa adui wao -serikali ya TPLF katika jimbo la Tigray. Lakini kwa pamoja wapotoshe ukosoaji kwamba wanajeshi wa Eritrean walikuwa ndani ya Tigray.

Bw Abiy aliuelezea mzozo kama sheria ya ndani ili kuzima ukosoaji wa kimataifa.

Alimwambia mkuu wa Umoja wa Mataifa kwamba wanajeshi wa Eritrea walikwenda tu katika maeneo yanayozozaniwa karibu na mpaka, ambao Ethiopia ilikuwa imekubali kuutoa.

Waziri mkuu huyo pia angekuwa na kazi ngumu ya kuwashawishi Waethiopia kwamba kuwakaribisha wanajeshi wa Eritrea lilikuwa ni wazo zuri.

Licha ya makubaliano ya mwaka 2018 ya amani bado watu wana kumbukumbu za hasira za vita vya mzozo wa mpaka baina ya nchi hizo mbili vilivyoanza mwaka 1998 hadi 2000.

Lakini kutokana na ripoti nyingi sana zilizoelezea kuwahusu wanajeshi wa Eritrea na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu pamoja na uporaji katika miji na vijiji, kujifanya wanapuuza ripoti hizo, lilikuwa ni jambo ambalo halingewezekana - Bw Abiy akaamua kubadilisha kauli.

Alichagua maneno kwa uangalifu-hakutaja uwepo wao katika mji wa Tigray. Badala yake alielezea eneo la mpaka-kauli ambayo ilikuwa wazi kwa mtu kuielewa kwa namna tofauti. Pia aliwanukuu maafisa wa Eritrea waliosema wanajeshi wataondoka mara tu jeshi la Ethiopia litakapoweza kudhibiti maeneo ya mapigano.

Kulikuwa na kukiri kwingine kutokana na kuongezeka kwa uzito wa ushahidi. Bw Abiy pia-kwa niaba ya nchi mbili-alilaani maasi yoyote ambayo yalifanyika.Taratibu ukweli wa kutisha unajitokeza.

Je maasi yanachunguzwa?

Juma lililopita, Umoja wa Mataifa ulisema utafanya kazi na Shirika la haki za binadamu la taifa la Ethiopia kuchunguza ripoti za mauaji ya raia yenye misingi ya ubaguzi na unyanyasaji mkubwa wa kingono.

Marekani imeelezea mzozo katika jimbo la Tigray kama uangamizaji wa jamii. Pia ilidai vikosi vya Eritrea viondoke ndani ya Ethiopia.