Mfereji wa Suez nchini Misri umezibwa na meli kubwa ya mizigo

The Suez Canal is blocked by a large container ship in Cairo, Egypt, 24 March 2021

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Meli imeziba karibu nafasi yote ya maji

Boti za kuvuta na wachimbaji wanafanya kazi ya kuisaidia meli kubwa ya kontena kuelea tena majini baada ya meli hiyo kuziba mfereji wa maji wa Suez nchini Misri, moja wapo ya njia zenye shughuli za biashara ulimwenguni.

Wamiliki wa meli hiyo yenye urefu wa mita 400 sawa na (futi 1312) wanasema ilikwama upande mmoja baada ya kupigwa na upepo mkali.

Misri imesema imefungua njia ya zamani kugeuza mkondo wa meli zingine ili kuzuia msongamano, huku kukiwa na wasi wasi njia ya sasa itazibwa kwa siku kadhaa.

Tukio hilo tayari limesababisha msongamano wa majini huku baadhi ya meli zikikosa njia ya kupita.

Karibu asilimia 10 ya biashara duniani zinafanywa kupitia mfereji wa Suez, ambao unaunganisha Mediterrania na bahari nyekundu (Red Sea) na kutoa njia fupi ya majini kati ya Asia na Ulaya.

Meli hiyo kwa jina The Ever Given, ilisajiliwa Panama, ilikuwa inaelekea mji wa bandari wa Rotterdam nchini Uholanzi kutoka China na ilikuwa inapata upende wa kaskazini kupitia mfereji wa Suez kuelekea Mediterrania.

Meli hiyo iliyo na ukubwa wa tani 200,000, iliundwa mwaka 2018 na ilikuwa ikiendeshwa na kampuni ya uchukuzi ya Taiwan, Evergreen Marine, ilikwama majini karibu saa 07:40 (05:40 GMT) siku ya Jumanne.

Chanzo cha picha, Vessel Finder

Meli hiyo iliyo na urefu wa mita 400m - sawa na urefu wa viwanja vinne vya soka - na upana wa meta 59-, imeziba njia za meli zingine ambazo zimekwama pande zote.

Evergreen Marine, imesema meli hiyo "huenda ilikabiliwa ghafla na upepo mkali, ulioifanya kupoteza mkondo… na kwa bahati mbaya kugonga chini na kukwama".

Picha iliyowekwa kwenye Instagram na Julianna Cona siku ya Jumanne, iliyoripotiwa kupigwa kutoka kwa meli nyingine ya mizigo - Maersk Denver - mojo kwa moja nyuma ya Ever Given, inaonesha meli iliyoziba sehemu ya njia ya majini.

Mamlaka ya Mferji wa Suez (SCA) zimesema zinafanya kilt juhudi kurudisha meli hiyo kubwa njiani, kwa kutumia vitengo vya uokozi na uvutaji, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP.

Mweyekiti wake, Admiral Osama Rabie, pia amesema wamefungua sehemu ya zamani ya mfereji huo wa Suez ili kukabiliana na changamoto za msongamano uliosababishwa na tukio hilo.

Dkt Sal Mercogliano, mwana historia wa masuala ya majini na mkazi wa jimbo la North Carolina nchini Marekani, ameiambia BBC kwamba visa kama hivyo ni nadra sana kutokea, lakini huenda vikawa na "athari kubwa Katina biashara ya kimataifa".

"Hii ni meli kubwa zaidi kuwahi kukwama katika mfereji wa Suez," alisema, akiongeza kuwa meli hiyo, ilikubwa na dhuruba kali na huenda ilipoteza uwezo wa kuendelea na safari.

"Endapo watashindwa kuivut aili iweze kuelea tena majini… katika mawimbi makubwa, watalazimika kutoa mizigo."

Meli hiyo ina uwezo wa kubeba makontena 20,000 yenye urefu wa futi 20.

Chanzo cha picha, PLANET LABS

Maelezo ya picha,

Picha zinazoonesha meli hiyo ilivyoziba njia ya mfereji wa Suez kupitia Setelaiti

Wataalamu wameonya oparesheni ya kuondoa Ever Given, ambayo inajumuisha kuondoa kiwango kikubwa cha mchanga iliyozunguka sehemu iliyokwama meli hiyo, huenda ikachukua siku kadhaa.

Karibu meli 19,000 zilipitia mfereji wa Suez mwaka 2020, kwa mujibu wa Mamlaka inayosimamia Mfereji wa Suez - inayokadiriwa kuwa karibu meli 51.5 kwa siku.

Mwaka 2017, meli ya mizigo ya Japan, iliziba mfereji huo baada ya kukwama majini kutokana na hitilafu za kiufundi.

Mamlaka nchini Misri, zilituma maboti kuvuta meli hiyo hadi ilipofanikiwa kuelea tena majini ndani ya saa kadhaa.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Wanaohusika pia wanatafuta namna ya kuhakikisha meli hiyo inapata nafasi kwa kuongeza njia ya ardhini