Mapinduzi ya Myanmar: Mtoto wa miaka saba auawa 'akimkimbilia baba yake’

Khin Myo Chit

Chanzo cha picha, Khin Myo Chit's family

Maelezo ya picha,

Khin Myo Chit alipigwa risasi Jumanne mchana, familia yake imesema.

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka saba ameuawa kwa kupigwa risasi nchini Myanmar na kuwa mwathiriwa mdogo zaidi katika msako uliofuata mapinduzi ya kijeshi ya mwezi uliopita.

Familia ya Khin Myo Chit imeambia BBC kwamba aliuawa na polisi alipokuwa anamkimbilia baba yake wakati wa msako dhidi ya nyumba yao katika mji wa Mandalay.

Majeshi ya Myanmar yamekuwa yakitumia nguvu kupita kiasi huku maandamano ya kupinga mapinduzi yakiendelea.

Shirika la kutetea haki la Save the Children linasema zaidi ya watoto 20 ni miongoni mwa watu waliouawa.

Kwa ujumla, majeshi yanasema watu 164 wameuawa katika maandamano, lakini wanaharakati wa chama cha kuwasaidia wafungwa wa kisiasa (AAPP) wanasema idadi ya waliofariki ni karibu watu 261.

Siku ya Jumanne wanajeshi walielezea masikitiko yao kufuatia vifo vya waandamanaji na kuwalaumu kwa kuzua vurugu na kusababisha ghasia nchini humo.

Lakini vikosi vya usalama vimekuwa vikitumia silaha za moto dhidi ya waandamanaji na kumetolewa ripoti kadhaa za mashuhuda zinazoashiria jinsi watu walivyoshambuliwa na wakati mwingine kupigwa risasi wakati wa msako wa kijeshi wa nyumba hadi nyumba kuwakamata wanaharakati na waandamanaji.

'Kisha wakampiga risasi'

Khin Myo Chit, dada mkubwa wa msichana alilyepigwa risasi ameambia BBC maafisa wa polisi walikuwa wakipekua nyumba zote za majirani zao katika mji wa Mandalay mchana wa Jumanne, mara wakaingia nyumbani kwao kutafuta silaha na kuwakamata watu.

"Walifungua mlango kwa mateke,"May Thu Sumaya aliye na umri wa miaka 25 alisema. "Mlango ulipofunguka, walimuuliza baba yangu kama kuna watu wengine nyumbani."

Aliposema hapana, walimlaumu kwa kusema uongo na kwanza kupekua nyumba, alisema.

Huo ndio wakati Khin Myo Chit alimkimbilia baba ili kumkalia mapaja. "Kisha wakampiga risasi," May Thu Sumaya alisema.

Pictures of Khin Myo Chit's family mourning her death

Chanzo cha picha, Aung Kyaw Oo

Maelezo ya picha,

Familia ya Khin Myo ikiomboleza kifo cha mtoto huyo

Katika mahojiano tofauti na chombo cha habari cha kijamii ya Waislamu wa Myanmar, baba yao U Maung Ko Hashin Bai alielezea maneno ya mwisho ya mtoto wake. "Alisema, 'Siwezi baba, ni uchungu sana'."

Alisema alifariki nusu saa baadae alipokuwa anakimbizwa hospitali kupata huduma za matibabu. Polisi pia walimpiga na kumkamata mwanawe wa kiume aliye na umri wa miaka 19.

Jeshi halijatoa tamko lolote kuhusiana na kifo hicho.

Katika taarifa, Shirika la Save the Children lilisema ''limegutushwa'' na mauaji ya mtoto huyo wa kike ambacho kimetokea siku moja baada ya mvulana wa miaka 14 kuripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi mjini Mandalay.

"Vifo vya watoto hawa vilitokea nyumbani ambako wanastahili kuwa salama. Ukweli ni kwamba watoto wengi wanauawa karibu kila siku na hii inaashiria kuwa vikosi vya usalama havijali kabisa maisha ya binadamu," kundi hilo lilisema.

Huku hilo likijiri siku ya Jumatano, mamlaka ziliwaachia huru karibu watu 600 waliokuwa wakizuiliwa katika gereza la Insein mjini Yangon (Rangoon), baadhi yao wanafunzi wa vyuo vikuu.

Mwanahabari wa Shirika la Associated Press, lilikuwa miongoni mwa wanahabari walioachiwa huru. Yeye na wanahabari wengine walikamtwa kwa kuangazia maandamano ya mwezi uliopita.

Chama cha AAPP kinasema karibu watu 2,000 wamekamatwa katika msako unaoendelea nchini humo kufikia sasa.

Waandamanaji wanapanga mgomo baridi huku maeneo kadhaa ya biashara yakitarajiwa kufungwa na watu kusalia majumbani mwao.

2px presentational grey line

Maelezo zaidi kuhusu Myanmar

  • Myanmar inajulikana pia kama Burma, ilikuwa chini ya utawala wa kijeshi kuanzia mwaka 1962 mpaka 2011.
  • Harakati za ukombozi zilianza mwaka 2010 na kulifanya taifa hilo kuwa na uchaguzi huru mwaka 2015 na mwaka uliofuata serikali ya taifa hilo ikaanza kuongozwa na kiongozi nguli wa upinzani Aung San Suu Kyi.
  • Mwaka 2017, mgogoro mkubwa uliibuliwa na jeshi la Myanmar katika eneo la waislamu wa Rohingya ambapo mamilioni ya watu walikimbilia mpakani mwa Bangladesh, jambo ambalo baadaye Umoja wa Mataifa iliitaja kuwa "mfano wa kitabu cha utakaso wa ukabila"
  • Aung San Suu Kyi na serikali yake ilipinduliwa na jeshi Februari 1 kufuatia matokeo ya uchaguzi wa Novemba.
2px presentational grey line
Map of Myanmar showing Mandalay, Nay Pyi Taw and Yangon

Pia unaweza kutazama:

Maelezo ya video,

Apiga picha akifanya mazoezi bila kujua serikali yake inapinduliwa