Kifo cha rais John Magufuli: Je kiongozi huyu atakumbukwaje nje ya Tanzania?

  • Rashid Abdalla
  • Mchambuzi Tanzania
Magufuli

Siku moja kabla ya mwili wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli kupumzishwa katika nyumba yake ya milele huko kijijini kwao Chato. Shughuli zilianzia Dar es Salaam, Dodoma, Zanzibar, Mwanza na hatimaye zinamalizikia Chato Kaskazini magharibi mwa Tanzania .

Maombolezo yanaendelea na shughuli za nchi zimesimama. Bado kuna vilio na huzuni. Salamu za rambirambi zinamiminika kutoka ndani na nje ya taifa hilo la Afrika Mashariki. Watanzania wamepewa fursa ya kumuaga.

Mtawala anapofariki, kinachosalia ni kumbukumbu. Watanzania wanayo mengi ya kumkumbuka Magufuli kwa utawala wake wa miaka mitano na miezi kadhaa.

Swali, Je nje ya Tanzania mwendazake huyo atakumbukwa kwa mambo gani?

Ndani ya Afrika

"Mwanamapinduzi," "mtoto wa bara la Afrika," Mwafrika wa kweli," shujaa dhidi ya ufisadi." Ni kauli kutoka marais wa Afrika waliohudhuria shughuli ya kumuaga katika uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma.

Licha ya kuwa ni kawaida kwa wanasiasa wa Afrika kusifiana mmoja wao anapofariki. Sifa za Magufuli zimeenda mbali zaidi hadi kutoka kwa raia wa kawaida wa bara hilo.

Baada ya kifo chake nilipokea simu kadhaa na kuzungumza na watu mitaani katika jiji la Kampala nilipo sasa. Wakitaka kujua nini kimetokea. Katika mazungumzo hayo sikubahatika mtu ambaye anakosoa utawala wa Magufuli.

Wengi wanamkumbuka kama mtetezi wa Tanzania. Kiongozi aliyepigania maendeleo ya watu wake na kupambana na rushwa na ufisadi. Hakuvumilia wateule wake waliofanya uzembe na kutowajibika.

Yumkini ndani ya Afrika Magufuli alivutia wengi kwa uongozi wake uliojikita kuwatumikia Watanzania masikini. Akipambana na mianya ya matumizi mabaya ya pesa za umma, ubadhirifu na ufujaji.

Kiongozi aliyeipenda nchi yake kiasi cha kutofanya safari yoyote nje bara hilo. Daima aliwakilishwa na mabalozi, mawaziri au Makamu wake. Alibaki ndani ya Tanzania akihudumia raia wake.

Nilifanya mazungumzo na mchambuzi mmoja wa siasa ambaye hakupenda nimtaje jina. Nilimuuliza kwanini ndani ya Afrika jina la Magufuli linakumbukwa kwa mazuri zaidi licha ya ukosolewaji mkubwa uliopo pia?

"Ni kawaida ya Waafrika kupongezana. Na kwa kesi Tanzania ni wazi hawajui kilichokuwa kikiendelea baada ya miaka miwili ya uongozi wake. Ni mfano wa kitanda usichokilalia, hukijui kunguni wake."

Ndani ya Afrika utawala wake una uungwaji mkono mkubwa kuliko upinzani. Hilo linadhihirika kupitia maoni ya watu katika mitandao ya kijamii.

Nje ya Afrika

18 Machi, Shirika la kutetea haki za Binaadamu, Human Right Watch, katika taarifa yake baada ya kifo cha Magufuli lilieleza, "ameacha kumbukumbu ya ukandamizaji na uvunjifu mkubwa wa haki za binaadamu."

'Maiti husemwa kwa mazuri.' Ni moja ya msemo maarufu barani Afrika, ukichochewa na busara za kimila na imani za kidini. Huku Waafika wakidumisha msemo wao.

Nje ya bara hilo hasa katika mataifa ya Ulaya na Marekani, Magufuli hutajwa zaidi kwa ukandamizaji wa uhuru wa habari na kisiasa. Akitajwa kama mtu asiyetaka kukosolewa.

Mbinu zake zenye utata katika kukabiliana na uviko-19 ziliacha gumzo pia. Zikaibua ukosoaji mkubwa. Na bado zinaendelea kukosolewa hata baada ya kifo chake.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus
Maelezo ya picha,

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johson, ni miongoni mwa waliotoa hisia zao katika mitandao ya kijamii kufuatia kifo cha Magufuli.

Wote wawili walijikita kueleza masikitiko yao na kutoa pole kwa kifo hicho. Lakini hawakuzungumzia utawala wa Magufuli katika namna yoyote ile.

Ni tofauti na jumbe kutoka viongozi wa Afrika ambao walizungumza au kuandika katika mitandao ya kijamii. Hawakuishia kutoa masikitiko na pole pekee, pia walienda mbali kwa kumsifia Magufuli na utawala wake.

Kwa uchache Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wa Afrika Kusini Cril Ramaphosa, Paul Kagame wa Rwanda, Kaguta Museveni wa Uganda, kiongozi wa upinzani kutoka Kenya, Raila Odinga.

Lipo swali linalohusu uhaba wa salamu za rambirambi za wazi kutoka mataifa makubwa. Je, imetokana na ukosolewaji wa namna alivyoendesha utawala wake au ni urafiki finyu aliokuwa nao na mataifa hayo?

Disemba 2021, taifa la Marekani lilionya, chini ya utawala wa Magufuli, Tanzania imeshuka kidemokrasia na uhuru wa asasi za kiraia. Pia, ililaumiwa kwa kuzuka mashambulio yaliyochochewa kisiasa.

Maoni ya wachambuzi wengi yanaashiria nje ya Afrika Magufuli ni mtawala aliyeanza vyema siku za mwanzo za utawala wake lakini amemalizia vibaya. Wengine wamefika mbali na kumwita mtawala wa kiimla ama kidikteta.

Vyombo vya Habari

"Rais mkataa Corona afariki dunia." Ni utambulisho uliopamba vichwa vya habari katika vyombo vingi vya habari vya nje, wakati wakitoa taarifa ya kifo chake. Ni kana kwamba wahariri walielezana nini cha kuandika.

Anuani hiyo inayofanana imeandikwa na vyombo vingi, kwa uchache CNN, The Guardian, Economist, Telegraph, Deutsche Welle, News Sky, NBC, WSJ, Indian Express, Bloomberg, New York Times, 9News, News 24, National Post.

Tetesi za kuumwa kwake, ziliandikwa zaidi na vyombo vya kimataifa. Ndani ya Tanzania hakuna chombo kilichothubutu kuandika uvumi huo. Vilisubiri kuandika kitakachosemwa na serikali.

Mamlaka za Tanzania zilipokaa kimya, vyombo vya nje vilitumia wanasiasa wa upinzani kuandika habari zilizohoji alipo Magufuli na uvumi juu ya kuugua kwake.

Baada ya kifo chake vyombo vya habari ndani ya Tanzania vimeandika makala kukumbuka yale mafanikio katika utawala wake. Nje ya hapo anaandikwa zaidi kwa yale yenye sura hasi kuuhusu miaka yake mitano.

Ule msemo wa, 'habari mbaya ndio nzuri kwa vyombo vya habari.' Ndio umefanya kazi kwa vyombo vya nje. Makala zimeandaliwa, nyingi zikijikita kuzungumzia yale ambayo yanatazamwa ni kufeli katika uongozi wake.