Kifo cha rais John Pombe Magufuli: Fahamu Jinsi ya kuepuka mkanyagano katika maeneo ya umati mkubwa

Mkanyangano Tanzania
Maelezo ya picha,

Mkanyangano Tanzania

Vifo vya ndugu watano wanaodaiwa kufariki kwa kukanyagwa katika shughuli ya kuaga mwili wa hayati John Magufuli katika uwanja wa Uhuru huko Dar es Salaam Jumapili Machi 21, 2021 ni jambo ambalo limezua maswali kuhusua usalama na mikakati inayowekwa na mamlaka wakati wa shughuli inayowaleta watu wengi pamoja .

Hali ya maafa hayo haijaelezwa kwa undani na mamlaka lakini inaaminika palitokea mkanyagano ndani ya uwanja huo na wote kukanyagwa na umati wa watu waliokuwa wakijaribu kuingia uwanjani kuaga mwili wa aliyeuwa rais John Pombe Magufuli .

Miili ya Ndugu hao wa familia ya Daudi Mtuwa; Susan Mtuwa na watoto wake wawili Nathan (6) na Natalia (5) pamoja na watoto wengine wawili Cris (11) na Michelle (8) wa shemeji zake Susan itazikwa leo Alhamisi Machi 25, 2021 mkoani humo.

Usalama ndani ya umati

Mtaalamu wa usalama Chris Losuru ameweza kueleza kinachotekea wakati mwingi katika hali zinazochangia kufanyika kwa mikanyagano ambayo husababisha watu kujeruhiwa au kufariki dunia .

Anasema ni jukumu la mamlaka na watu katika eneo lililojaa kuhakikisha kwamba wapo salama kwa kuepuka kufanya baadhi ya mambo na pia kutii maelekezo . Bw. Losuru anasema cha msingi kwa mtu anayehudhuria shughuli yenye umati mkubwa ni kuhakikisha:

•Utulivu: Kuwa mpole ili kuhakikisha kwamba Iwapo kuna foleni basi unafuata utaratibu uliowekwa .Tatizo ambalo hutokea wakati mwingi katika hali kama hizo ni sehemu ya umati kutaka kutangulia kwa kuwasukuma watu .Hilo husababisha anachokitaja kama 'Mawimbi ya chuma' ambayo huweza kusababisha walio wanyonge kuanguka na kisha kukanyagwa .

•Kutii maelekezo: Hii ni changamoto kubwa sana katika hali ambazo kuna idadi kubwa ya watu .Mara nyingi maelekezo huwa yametangazwa mapema au kuandikwa ili wanaohudhuria shughuli kuyafuata. Maelekezo hayo ni pamoja na wakati maalum wa kuingia ama kuondoka eneo la shughuli na pia lango ama maeneo ya kutumia kuingia ama kuondoka ili kuzuia watu wengi kupindukia kujipata katika tundu linaoweza kuhatarisha maisha yao wakati panaotokea hali ya dharura .

Losuru anasema kando na kukumbuka tahadhari hizo za kibinafsi unaweza ukajipata katika hali ya mkanyagano na inapotokea unashauriwa kufuata hatua Zifuatazo:

Usiwe na wasi wasi/Hofu

Usitumie sauti yako kuzua ukemi ama kelele bali kuwatuliza wenzio.

Tumia uzani wako dhidi ya msukumo wa watu na uwashauri vivyo hivyo wanaokusuma .

Walinde watu wa umri wa juu/wanawake/Watoto. Kudi hilo ndilo litakalokuwa la kwanza kuangushwa na kukanyagwa endapo hali itakuwa mbaya

Mwongozo wa kujiokoa

Je, unafaa kufanya kipi unaponaswa ndani ya umati na kuhisi kwamba 'ukuta' umeanza kukubana? Huu hapa mwongozo wa baadhi ya unayoweza kufanya ili kuokoa maisha yako na ya wengine katika hali kama hiyo

1. Kuwa macho

Lengo lako kubwa ni kuondoka kutoka sehemu hiyo yenye watu wengi kwa haraka sana na kwa utulivu . Tathmini hali yako kwa kuangalia kote kisha jiamulie Iwapo ni bora kwenda mbele ama nyuma? Epuka kuelekea ambako kuna msukosuko zaidi ama palipo na watu wengi na uanze kwenda upande ambao idadi ya watu inapungua ama ni ndogo

2.. Ondoka mapema kadri ya uwezo wake

Iwapo umati utajikusanya karibu nawe nafasi yako kutoroka inaanza kupungua kwa haraka na utajipata katika hatari kubwa . Unapongoja ili kupata fursa ya kuondoka ndivyo unavyopunguza uwezo wako kuweza kujinasua -kwa hivyo unashauriwa kuchukua hatua pindi tu unapogundua kwamba idadi ya watu katika eneo uliko inazidi kuongezeka .Kwa kuondoka mapema pia unaondoa hatari kwa waliobaki kwa sababu idadi ya watu katika sehemu hiyo itakuwa ndogo.

3. Simama

Iwapo utachelewa kuondoka kutoka sehemu iliyojaa watu basi hakikisha kwamba umesimama na unaweza kujiinua .Katika hali kama hizo watu hubanana kwa haraka sana na wakati unapoanguka , kinachofuatia ni 'mporomoko' wa watu na uzito wao huwa kama vifusi vya jengo . Ni nadra sana kupona katika hali kama hiyo kwa hivyo hakikisha kwamba huanguki ama kuketi unapojipata katikati ya umati .

4. Okoa hewa yako

Pumzi ndio raslimali kubwa sana kwako . Idadi kubwa ya watu wanaofariki katika mkanyagano hutokea kwa sababu ya kukosa hewa . Epuka kupiga kamsa ama kelele isipokuwa katika hli ambazo ni lazima na udhibiti pumzi yako .

5. Mikono mbele yako

Iwapo presha ya umati itaongezeka, kunja mikono yako na uiweke mbele yako kama mwana ndondi. Katika hali kama hiyo utaweza kukinga kifua chako na kuweka pengo la sentimita kadhaa kati ya watu wanaokukaribia na mbavu zako pamoja na mapafu ili uweze kupumua .

6. Fuata mtiririko

Unaposukumwa , wakati mwingine utajibu kwa kusukuma pia upande wa pili . Lakini katika hali ya mkanyagano ukifanya hivyo basi unafanya kazi ya bure . Badala yake kubali kusukumwa na nenda na mtiririko huo ila hakikisha kwamba unasalia miguuni-usianguke

7.Songa mbali na vizuizi

Wakati mwingine ambapo kidokezo kilichotangulia hakiwezi kutumika ni muda unapojipata umekaribia ukuta,ua vizuizi vingine . Waathiriwa wa kwanza wa mkanyagano huwa watu waliobanwa dhidi ya vizuizi kama ilivyokuwa katika mikasa ya Turin mwaka wa 2017 na Heysel na Hillsborough miaka ya 1980. Ikiwezekana songa mbali na vizuizi kama vile ukuta ama ua na vyuma

8. Unafaa kuelewa idadi ya umati

Ili kufanya maamuzi yafaayo unafaa kuelewa hatari ya kila idadi ya watu katika sehemu moja .Hii hapa njia rahisi ya kukadiria hilo-Iwapo utajipata huwezi kuugusa uso wako kwa mikono yako ,hali ni mbaya na idadi ya watu waliopo hapo ni kubwa na kuna hatari -unashauriwa kuchukua hatua papo hapo.