Vladimir Putin: Kwanini kiongozi huyu wa Urusi huhusishwa katika kila msukosuko Marekani?

  • Yusuf Jumah
  • BBC Swahili
Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Urusi Vladimir Putin
Maelezo ya picha,

Rais wa Marekani Joe Biden na Rais wa Urusi Vladimir Putin

Rais wa Urusi Vladimir Putin huenda aliidhinisha majaribio ya kushawishi uchaguzi wa Marekani mwaka jana kwa niaba ya Rais wa zamani Donald Trump, maafisa wa ujasusi wanasema.Moscow ilieneza "madai ya kupotosha au yasiyothibitishwa" kuhusu mshindi wa uchaguzi huo , Joe Biden, kulingana na ripoti ya serikali ya Marekani.Lakini ilisema hakuna serikali ya kigeni iliyoathiri matokeo ya mwisho.

Urusi imekuwa ikikanusha madai ya kuingilia uchaguzi huo.

Ripoti hiyo ya kurasa 15, iliyotolewa Jumanne na Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Kitaifa, ilielezea kile ilichosema ni "shughuli za ushawishi" zilizosukumwa na Urusi na Iran pia.

Ilisema watu wanaohusishwa na Urusi walikuwa wameeneza madai yasiyothibitishwa juu ya Rais Biden kabla ya uchaguzi wa Novemba 3. Pia ilisema kampeni ya kutoa habari za kupotosha ilitaka kudhoofisha imani katika mchakato mzima wa uchaguzi.

Uhasama wa Putin na Marekani

Kuwepo kwa uhasama fiche kati ya Marekani na Putin ama nchi yake Urusi umekuwepo kwa muda na ushahidi umetokana na hatua nyingi wanazochukua dhidi ya kila mmoja.

Urusi imejipata ikifanya maamuzi ambayo yanapinga mataifa ya Magharibi na Marekani na hili linaweza kuonekana katika mizozo mbali mbali kutoka vita vivayoendelea Syria hadi katika mzozo wa Crimea . Kulikuwa na mjadala nchini Marekani wakati mmoja kwamba utawala wa rais Barack Obama haukuwa ukichukua hatua kali dhidi ya 'fujo za Putin' na katibu wa mashauri ya kigeni wakati huo Hillary Clinton alionekana wakati mwingi akitoa matamshi makali dhidi ya Putin na serikali yake .

Wakati rais Donald Trump alipochukua usukani ,kulikuwa na tofauti kubwa ya jinsi Putin alivyoizungumzia Marekani huku Trump akionekana kama rafiki yake na hata alimtetea dhidi ya madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Amerika ili kumsaidia Trump kupata ushindi .

Chini ya Rais Vladimir Putin, Urusi imekuwa serikali yenye mamlaka mengi, serikali ya kimabavu na imerudi kama mdau mkuu na muhimu kuhusu masuala mbali mbali ya ulimwengu, ikishindana na Amerika kwa ushawishi. Ingawa ni dhaifu kuliko Amerika kiuchumi na kijeshi, ina uwezo wa kuingilia kati kote ulimwenguni na kuvuruga maslahi ya Marekani. Washington na Moscow wana maoni tofauti kimsingi juu ya jinsi uhusiano kato yazo unavyoweza kufanikiwa .

Muda mfupi wa Ushirikiano

Kumekuwa na vipindi viwili katika historia ya hivi karibuni wakati ushirikiano kati ya Marekani na Urusi umefanya kazi vizuri: Pindi tu baada ya 9/11 wakati Urusi ilisaidia Marekani katika awamu ya kwanza ya vita huko Afghanistan, ikitoa habari ambayo ilikuwa imekusanya kutoka vita vyake vya miaka kumi iliyotangulia; na wakati wa kipindi cha 2008-12 cha "kuweka upya" uhusiani kati ya nchi hizo mbili kati ya Marais Barack Obama na Dmitry Medvedev, wakati Moscow na Washington zilishirikiana juu ya udhibiti wa silaha, Afghanistan, Iran, na maswala mengine mbali mbali.

Uhusiano ulianza kuwa mbaya wakati Putin aliporudi Kremlin mnamo 2012, akiamini kuwa Hillary Clinton alikuwa nyuma ya waandamanaji ambao walikuwa wamepinga kurudi kwake madarakani. Mwaka uliofuata, Putin alipeana hifadhi ya kisiasa kwa Edward Snowden, mwanakandarasi wa NSA ambaye aliiba mamilioni ya hati na stakabadhi za siri na kisha kukimbilia Urusi kupitia Hong Kong. Ilikataa ombi la Rais Obama la kumrudisha. Obama baadaye alisusia mkutano uliopangwa na Putin.

Kuvurugika kabisa kwa 'urafiki'

Vitendo vya Urusi mnamo 2014 vilisababisha pigo jingine kubwa kwa uhusiano huo.

Kufuatia maandamano ya miezi kadhaa, Rais wa Ukraine aliyeungwa mkono na Urusi Viktor Yanukovych alikimbilia Urusi na nafasi yake ikachukuliwa na serikali inayoungwa mkono na mataifa ya Magharibi.

Muda mfupi baadaye, wanajeshi wa Urusi waliingia na kuchukua Pwani ya Crimea, ambayo ilikuwa sehemu ya Ukraine tangu 1954, na hivyo kukiuka masharti ya Mkataba wa Budapest wa 1994 ambao Urusi, Amerika, Ukraine, na Uingereza walikuwa wameahidi kudumisha uadilifu wa eneo la Ukraine. Katika miezi michache iliyofuata, wanaotaka kujitenga walioungwa mkono na Urusi na askari wa Kirusi ambao hawakuwa na nembo katika sare zao za jeshi waliingia na kuchukua sehemu za mkoa wa Donbas kusini mashariki mwa Ukraine, na kuwaondoa mamlakani watawala halali wa maeneo ya serikali za mitaa.

Tangu mwaka wa 2014, Urusi na Ukraine wamekuwa wakipigana vita katika eneo la Donbas ambapo 14,000 wamekufa.

Ili kujibu hatua hiyo Marekani iliwawekea vikwazo watu wa Urusi walio karibu na Putin na uwezo wa Urusi kupata masoko ya kifedha.

Kuingia kwa Urusi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria mnamo 2015 kumuunga mkono Bashar al-Assad pia kumezua mvutano na Marekani ambayo ilikuwa ikiunga mkono vikundi vinavyompinga Assad.

Tangu wakati huo, Washington na Moscow zimelazimika kuondoa shughuli zao za anga huko Syria kuzuia migongano isiyotarajiwa. Baada ya Amerika kuondoa sehemu ya wanajeshi wake kutoka Syria, wanajeshi wa Urusi waliingia katika kambi zilizokuwa chini ya Marekani na kuunga mkono mashambulio makali ya Assad dhidi ya mkoa wa Idlib, ambao umewafanya mamilio ya watu kuwa wakimbizi .

Chanzo cha picha, Reuters

Muingilio wa Mataifa mengine

Watu wengine waliohusishwa na ujasusi wa Urusi pia walishinikiza taarifa na habari dhidi ya Biden kwa vyombo vya habari, maafisa wakuu na washirika wa Bw Trump, ripoti hiyo ilisema.Rais Biden alimshinda Bw Trump na akaapishwa mnamo 20 Januari.

Ripoti hiyo iliongeza kuwa, wakati Urusi ilikuwa ikitaka kuongeza nafasi ya Bw Trump kushinda, Iran ilikuwa imeanzisha "kampeni ya ushawishi wa siri nyingi" katika juhudi za kudhoofisha uungwaji mkono wake.Rais huyo wa zamani alifuata sera ya "shinikizo kali " dhidi ya Iran, akiweka vikwazo vilivyokuwa na madhara kwa Iran na kuongeza vita vya maneno kati ya mataifa hayo mawili.

Ripoti hiyo pia ilihitimisha kwa "imani kubwa" kwamba China, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikishutumiwa kwa ujasusi wa kimtandao na Washington, iliamua kutotumia "juhudi za kuingilia kati" kabla ya kura."Uchina ilitafuta utulivu katika uhusiano wake na Amerika na haikuona matokeo yoyote ya uchaguzi kama yenye faida ya kutosha kwa China kuhatarisha kuvuruga uhusiano huo ikiwa itashikwa," ilisema.Kulingana na ripoti hiyo, mchakato wa kupiga kura na matokeo ya mwisho hayakuingiliwa na mataifa ya kigeni.

Ripoti ya ujasusi ilitolewa wakati mmoja ambao pia ripoti za uchunguzi uliofanywa na idara za Haki na usalama wa kitaifa ,Homeland security ilipoafikia matokeo yayo hayo .

Ripoti yao ilisema "Kampeni pana za Kirusi na Irani zinazolenga sekta nyingi muhimu za miundombinu ziliathiri usalama wa mitandao kadhaa ambayo ilisimamia kazi kadhaa za uchaguzi"

Lakini ilisisitiza kwamba majaribio ya kuingiliwa yaliyodaiwa hayakuwa ya moja kwa moja.

"Hatuna ushahidi kwamba nchi yoyote ya kigeni ilijaribu kuingilia kati ... kwa kubadilisha hali yoyote ya kiufundi ya mchakato wa kupiga kura, ikiwa ni pamoja na uandikishaji wa wapiga kura, kupiga kura, kuhesabu kura, au kutoa ripoti za matokeo," inasema hati hiyo.

Jamii ya Intelejensia nchini Marekani imesema Agosti iliyopita kwamba Uchina, Urusi na Iran walikuwa wakijaribu kuingilia kati katika uchaguzi ujao wa urais.

Tathmini hiyo iligundua kuwa Urusi ilikuwa inataka "kumdhalilisha" Bwana Biden. Pia iligundua kuwa China na Iran zilitaka Bw Trump apoteze kura.