Msemaji wa Serikali Kenya afafanua zuio la Rais Uhuru Kenyatta la kutotoka nje

Msemaji wa serikali Kenya Cyrus Oguna

Chanzo cha picha, NATION MEDIA GROUP

Maelezo ya picha,

Msemaji wa serikali Kenya Cyrus Oguna

Zuio la kutotoka au kuingia katika kaunti tano nchini Kenya lililotangazwa na Rais Uhuru Kenyatta hapo jana, limesongezwa mbele hadi kesho saa mbili usiku, Jumapili.

Hayo ni kulingana na msemaji wa serikali Cyrus Oguna ambaye ametangaza kuwa agizo hilo limepewa muda zaidi kabla ya kuanza kutekelezwa.

Zuio hilo lililotangazwa jana na kuhusisha kaunti za Nairobi, Kajiado, Machakos, Kiambu na Nakuru limewekwa kama njia moja ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona nchini humo.

''Tunajua kwamba baadhi ya watu wetu wamekwamba katika maeneo hayo. Kwa walioathirika, serikali imewaruhusu kuwa na muda wa kusafiri hadi kesho, Machi 28, 2021 katika saa za kusalia ndani zilizowekwa. Hili linajumuisha kila ambaye tangazo hili lilimpata akiwa sehemu ambayo anahitajika ama kurejea au kutoka nje ya eneo husika, hili pia linajumuisha wanafunzi walio vyuoni vilevile,'' Oguna amesema.

Aidha, Msemaji wa Serikali Bwana Cyrus Oguna, amesema kwa wale wenye tiketi za usafiri kwa njia ya anga na treni ya SGR, muda wao wa kusafiri umesongezwa mbele zaidi hadi Jumatatu, Machi 29, na kuanzia hapo, usafiri wote kupitia njia ya SGR au ndege za ndani ya nchi katika maeneo yaliyotajwa utasitishwa lakini usafiri wa ndege za kimataifa utaendelea.

Pia alisema kuwa wenye pasi za kuwawezesha kusafiri wakati wa kusalia ndani uliowekwa, watatumia pasi zao za zamani hadi pasi mpya zitakapotolewa wiki ijayo na kuwa mchakato wa kutuma maombi unasalia kuwa vile vile kwa wahusika miongoni mwao wakiwa wahudumu wa afya na wanahabari.

Oguna pia amesema wafanyakazi wa zamu yaani usiku na mchana hawaathiriki na hatua mpya zilizochukuliwa.

Bwana Oguna amesisitiza kuwa hatua zote zilizowekwa kukabiliana na virusi vya corona ni lazima zitekelezwe ikiwa ni pamoja na kuwa na cheti kinachothibitisha kwamba mtu hana maambukizi ya virusi vya corona baada ya kupimwa ndani ya saa 96 kabla ya kusafiri.

Chanzo cha picha, IKULU YA RAIS

Maelezo ya picha,

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya

Akilihutubia taifa hapo jana, ijumaa Rais Kenyatta pia alifanyia mageuzi marufuku ya kutotoka nje ambapo sasa marufuku hiyo itaanza saa mbili usiku hadi saa kumi alfajiri katika kaunti hizo tano ilhali katika kaunti zingine ikiendelea kuanza saa nne usiku hadi saa kumi alfajiri.

Masharti mengine ni yapi?

Kando na kuzuia usafiri wa watu katika kaunti hizo tano Rais Kenyatta pia amepiga marufuku mikutano au mikusanyiko ya watu katika maeneo hayo.

Bunge nalo pia limechukua likizo pamoja na mabunge ya kaunti zilizotajwa kufungiwa.

Serikali pia imefutilia mbali pasi zilizokuwa zimetolewa kwa watu wanaotoahuduma muhimu kwani zimekuwa zikitumiwa vibaya na wizara ya Afya na ile ya usalama wa ndani zitatathmini upya mwongozo wa kuzitoa pasi hizo.

Shughuli zote zakuabudu katika kaunti za Nairobi, Nakuru, Machakos, Kiambu, na Kajiado zimezuiwa hadi wakati uamuzi huo utakapobadilishwa.

Katika hatua ambayo huenda tena ikawahamasisha wafanyibiashara katika sekta ya burudani, baa hazitaruhusiwa kuhudumu katika kaunti hizo tano husika na mikahawa imetakiwa kutoa huduma za kuuza chakula kwa wateja na pia imepigwa marufuku kuuza pombe

Hakuna masomo ya ana kwa ana yatakayokubaliwa na vyuo vikuu vyote na shule zimefungwa.

Wafanyikazi wa mashirika ya serikali na ya kibinafsi wametakiwa kufanyia kazi nyumbani isipokuwa kwa wale wanaotekeleza huduma muhimu zinazowahitaji kwenda kazini.

Hospitali zimetakiwa kupunguza idadi ya watu wanaokuja kuwaona wagonjwa hadi mtu mmoja kwa kila mgonjwa.

Mikutano yote itakayoruhusiwa itakuwa na watu wasiozidi 50 ilhali mazishi yataandaliwa ndani ya kipindi cha saa 72 na ni watu 50 pekee watakaoruhisiwa mazishini.

Serikali pia imesema watu walio na umri wamiaka 58 na zaidi ndio watakaokuwa wa kwanza kuchanjwa.

Chanzo cha picha, Empics

Maelezo ya picha,

Rais Kenyatta na Mke wake wakipata chanjo

Wakati huo huo, Rais Uhuru Kenyatta na mke wake waliwaongoza Wakenya katika shughuli ya upataji chajo hiyo.