Waasi Msumbiji: Wanamgambo wa Kiislamu 'wawavamia wafanyakazi waliokuwa wakitoroka hotelini'

Waasi

Wapiganaji wa kiisilamu wamevamia msafara uliokuwa ukijaribu kuwaokoa raia kutoka kwenye hoteli wakati wa mapigano Kaskazini mwa Msumbiji, ripoti zinasema.

Mwanamume mmoja raia wa Afrika Kusini amethibitishwa kuwa amekufa, lakini hakuna taarifa zaidi

Mamia ya watu walikimbia kutokana na mapigano hayo, ambayo yalianza Jumatano katika mji wa Palma. Waliotoroshwa walijumuisha wafanyikazi wa kigeni wa sekta ya gesi.

Kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa Total ilisema ililazimika kusitisha shughuli katika mradi mkubwa wa gesi ulio karibu na eneo lenye mapigano.

Kampuni hiyo ilikuwa imetangaza tu kuwa itaanza tena kazi kwenye mradi unaogharimu dola bilioni 20 ambao ulikuwa umesimama mwezi Januari kutokana na hali mbaya ya usalama.

Katika taarifa, kampuni hiyo ilisema hakuna mfanyakazi wake aliyeuawa katika tukio hilo.

Total iliongeza kuwa inaamini vikosi vya usalama vya Msumbiji, ambavyo vilikuwa vikifanya kazi ili kudhibiti wa eneo hilo.

Human Rights Watch ilisema kwamba mashuhuda walielezea kuwa waliona "miili barabarani na wakazi wakitoroka baada ya wapiganaji kufyatulia risasi kiholela watu na majengo".

Enao la Kaskazini mwa Msumbiji limekumbwa na uasi tangu mwaka 2017.

Wapiganaji wanaohusishwa na kundi la Islamic State (IS) ndio wanaosababisha mzozo katika eneo lenye Waislamu wengi la Cabo Delgado. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 2,500 na watu 700,000 wamehama makazi yao.

Map

Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa za raia wa Uingereza kunasa katika hoteli.

Msemaji wa ofisi ya mambo ya nje, Jumuia ya madola na Maendeleo ameiambia BBC: '' Ofisi yetu ya ubalozi mjini Maputo iko kwenye mawasiliano ya moja kwa moja na mamlaka za Cabo Delgado ili kupata taarifa zaidi kuhusu ripoti hizi.''

Waasi walianzisha shambulio la kushtukiza Palma mapema wiki hii wakishambulia maduka, benki na kambi za jeshi.

Mamia ya watu walikimbia mapigano, wakikimbilia kwenye misitu, mikoko au vijiji vya karibu. Karibu wafanyikazi wa kigeni 180 wa gesi na wazawa walitoroka katika hoteli ya Amarula Palma.

Wengine walijaribu kutoroka hoteli hiyo wakiwa na msafara wa magari Ijumaa, wakielekea pwani iliyo karibu, shirika la habari la Reuters lilimnukuu Lionel Dyck akisema. Bwana Dyck anaongoza kampuni ya usalama ya binafsi ya Afrika Kusini inayofanya kazi na serikali ya Msumbiji.

Lakini walivamiwa nje ya hoteli hiyo, Bw Dyck alisema, akiongeza kuwa watu wasiopungua 20 hapo awali walisafirishwa kwa usalama kwenye helikopta.

Mtu huyo wa Afrika Kusini aliyethibitishwa kuuawa alidhaniwa alikuwa akiendesha moja ya magari yaliyotumika kutorosha watu.

Chanzo kimoja kiliiambia BBC watu kadhaa walifanikiwa kuhamishwa na kufika mji wa Pemba, umbali wa kilometa 420 Kusini mwa Palma.