Bomu la kujitoa muhanga lalenga kanisa Jumapili ya matawi, waumini wajeruhiwa

Eneo lililotokea mlipuko mjini Makassar

Chanzo cha picha, Reuters

Shambulio linaloshukiwa kuwa la bomu la kujitoa muhanga nje ya kanisa Katoliki katika mji wa Makassar nchini Indonesia limejeruhi takribani watu 14 , polisi wanasema.

Polisi wamesema mlipuko ulitokea wakati washambuliaji wawili walipojaribu kuingia kanisani Jumapili ya matawi, siku ya kwanza ya Pasaka.

Pikipiki iliyoharibiwa na sehemu za mwili zilipatikana katika eneo la tukio na polisi walisema washambuliaji hao wawili walikuwa wamekufa.

Wanamgambo wa Kiislamu walishambulia makanisa hapo zamani lakini hakuna kundi ambalo lilikiri kutekeleza mashambulizi hayo.

Rais wa Indonesia Joko Widodo alilaani shambulio hilo kama "kitendo cha ugaidi" na akasema alikuwa amemwagiza mkuu wa polisi kuchunguza waliohusika.

"Natoa wito kwa kila mtu kupigana dhidi ya ugaidi na msimamo mkali, ambao ni kinyume na maadili ya kidini," rais alisema.

Waziri wa Masuala ya Kidini Yaqut Cholil Qoumas aliwasihi polisi kuongeza hatua za usalama katika sehemu za ibada.

Wakati wa misa ya Jumapili ya mitende huko Vatican, Papa Francis aliwaombea waathiriwa wa shambulio hilo.

Tunafahamu nini kuhusu shambulio hilo?

Mlipuko ulitokea majira ya saa nne na nusu saa za eneo hilo mwishoni mwa ibada ya Jumapili ya matawi.

''Kulikuwa na watu wawili wakiendesha pikipiki wakati mlipuko ulipotokea katika lango kuu la kuingilia katika eneo la kanisa- watu hao walikuwa wakijaribu kuingia katika uwanja wa kanisa, '' msemaji wa polisi Argo Yuwono alisema.

Kisha baadae, Mkuu wa usalama nchini humo, Mahfud MD, aliliezea tukio hilo kuwa ''bomu la kujitoa muhanga'' lililotekelezzwa na watu wawili, ambao wote walikufa.

Chanzo cha picha, Reuters

Padre katika kanisa hilo, Wilhemus Tulak, aliiambia Televisheni ya Metro TV kuwa walinzi walikuwa wamekabiliana na mtu mmoja anayeshukiwa kuwa mshambuliaji.

Mshambuliaji huyo, alisema, alifika kwa pikipiki na kujaribu kuingia kanisani.

Polisi walisema watu wasiopungua 14 walijeruhiwa, pamoja na maafisa wa kanisa ambao waliwazuia washambuliaji kuingia katika kanisa kuu.

Mlipuko huo ulitokea upande wa lango la kanisa. Picha za kamera za usalama zilionesha moto, moshi na kifusi katikati ya barabara.

Meya wa Makassar Danny Pomanto amesema kuwa mlipuko huo ungetokea kwenye lango kuu, ungeweza kusababisha athari zaidi.

"Kulikuwa na watu kadhaa waliojeruhiwa barabarani. Nilimsaidia mwanamke mmoja aliyejeruhiwa na kutapakaa damu," shahidi mmoja aliyetajwa tu kama Yosi aliliambia shirika la habari la AFP.

"Mjukuu wake pia alijeruhiwa. Kulikuwa na sehemu za miili kila mahali."

Gomar Gultom, mkuu wa Baraza la Makanisa la Indonesia, alisema shambulio kwa watu wanaosherehekea Jumapili ya mataei ni la "kikatili".

Aliwahimiza watu kuwa watulivu na kuamini mamlaka.

Chanzo cha picha, EPA

Makanisa yalilengwa huko nyuma na watu wenye itikadi kali nchini Indonesia, taifa kubwa zaidi la Waislamu ulimwenguni.

Mwaka 2018, watu kadhaa waliuawa katika shambulio la bomu kwenye makanisa na makao makuu ya polisi katika mji wa bandari wa Surabaya.

Polisi walishutumu mtandao ulioongozwa na wanamgambo wa Kiislamu, kundi la Jamaah Ansharut Daulah (JAD), kwa mashambulio hayo.