Kifo cha Magufuli; Vijana walipewa fursa gani katika ulingo wa siasa za Tanzania?

  • Markus Mpangala
  • Mchambuzi, Tanzania
Magufuli

Wakati wananchi wa Tanzania wakiwa bado katika siku za maombolezo ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Dkt. John Pombe Magufuli, katika upande wa pili amewaandalia vijana ambao wanatarajiwa kuwa hazina ya uongozi kwa miaka ijayo.

Magufuli katika kipindi chake cha miaka mitano alitoa nafasi kwa viongozi mbalimbali vijana katika ulingo wa siasa za Tanzania.

Kuanzia mawaziri, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala hadi kuwapitisha baadhi yao kuwania nafasi za ubunge katika bunge la Jamhuri.

Kupitia nafasi ya urais hadi uenyekiti wa CCM, Magufuli ametengeneza vijana ambao wapo tayari kutumikia taifa hilo bila kujali rangi, kabila, dini na ukanda.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa Magufuli hakujali itikadi zao ndiyo maana aliwachukua baadhi ya vijana kutoka vyama vya upinzani kama CUF na Chadema pamoja na wale waliokuwa nje ya uanachama wa CCM.

Pia anatajwa kuwavumilia baadhi ya vijana ambao wamewahi kutenda makosa ambayo aliamini yanarekebishika hivyo kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao kiuongozi.

Aidha, Magufuli anatajwa kufanikiwa kuwadhibiti viongozi vijana hao kwa nia ya kutaka waendane na mtazamo wake ambao ulikuwa uchapakazi, kutopoteza muda, kuleta matokea ya kazi pamoja na kuharakisha mipango ya maendeleo.

Baraza la Mawaziri

Baraza la Mawaziri Tanzania ni ngazi ya juu ya utendaji serikalini.

Baraza hili linaundwa na Rais, Makamu wa Rais, Rais wa Zanzibar, Waziri mkuu na mawaziri wote wanaoongoza moja ya Wizara za serikali.

Magufuli aliwabeba vijana na kuwafikisha katika ngazi hii na kutengeneza njia bora kwa vijana hao kuonesha vipawa vyao na kuwa hazina ya uongozi kwa Taifa hilo.

Ndani ya Baraza la mawaziri kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 pamoja na 2020 hadi 2021 Magufuli alikuwa na sura kadhaa za vijana ambao aliwateua ili wamsaidie kazi za kuwaletea maendeleo wananchi wa nchi hiyo.

Maelezo ya picha,

January Makamba

Miongoni mwa mawaziri vijana walioibuliwa na Magufuli pamoja na vyeo walivyokabidhiwa kwenye mabano ni Antony Mavunde (Naibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu), January Makamba na Luhaga Mpina (Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira).

Maelezo ya picha,

Seleman Jafo

Wengine ni Seleman Jaffo (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,Utumishi na Utawala Bora), Hussein Bashe (Naibu waziri wa kilimo), Dkt.Hamis Kigwangalla (Naibu waziri wa Afya na wizara ya Maliasili na utalii), Nape Nnauye (Waziri wa Habari Utamaduni,Wasanii na Michezo), Juliana Shonza (Naibu waziri wa Habari), Patrobas Katambi (Naibu waziri wa wizara ya Sera, Bunge, kazi, Vijana, Ajira na Walemavu).

Pamoja na David Silinde (Naibu Tamisemi), Geofrey Pinda (Naibu Katiba na Sheria), Ummy Nderiananga (Wenye Ulemavu), Doto Biteko (Madini), Innocent Bashungwa (Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo), Juma Aweso (Wizara ya Maji).

Wakuu wa mikoa na wilaya

Chanzo cha picha, JOKATE MWEGELO/TWITTER

Mwanamitindo Jokate Mwegelo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani alizua gumzo na wasiwasi endapo angefanikiwa kuendana na kasi ya Rais Magufuli.

Hata hivyo tangu alipoteuliwa hajawahi kuondolewa wala kubadilishwa kituo cha kazi, ikiwa na maana Rais Magufuli aliridhishwa na utendaji wa kiongozi wake huyo kijana.

Maelezo ya picha,

Paul Makonda

Wakati Rais Magufuli akiingia madarakani alimkuta Paul Makonda akiwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es salaam. Lakini alimpandisha ngazi hadi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam.

Makonda alikuwa mwanasiasa maarufu zaidi katika utawala wa Rais Magufuli, ambapo duru za kisiasa zinaonesha ndiye alikuwa kijana kipenzi cha kiongozi huyo licha ya kuandamwa na matukio mbalimbali yakiwemo kulumbana hadharani na viongozi wengine wa serikali wakiwemo Dkt. Philip Mpango (Waziri wa Fedha) kuhusu sakata la Makontena, pamoja na aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye kuhusu sakata la uvamizi wa kituo cha televisheni cha Clouds.

Chanzo cha picha, Godwin Gondwe/ INSTAGRAM

Maelezo ya picha,

Godwin Gondwe na Hayati Rais Magufuli

Akiwa mwanahabari mwandamizi wa kituo cha Televisheni cha ITV, Godwin Gondwe alipata nafasi ya kuteuliwa kuwa mkuu wa wilaya, na hadi Rais Magufuli alipofariki duniani amemwacha kijana huyo akiwa Mkuu wa wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam. Ni miongoni mwa wanasiasa ambao wanatarajiwa kutamba kwenye ulingo wa siasa nchini Tanzania miaka ijayo.

Picha inaonesha akitokwa na machozi, huzuni kubwa machoni pa Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya aliyekaa jukwaani wakati wa kumuaga Rais Magufuli mkoani Dodoma ni ishara ya kuguswa na pigo katika harakati zake za siasa nchini Tanzania.

Ole Sabaya ameibuka kuwa miongoni mwa wanasiasa vijana walioibuliwa na Rais Magufuli kwa kukabidhiwa majukumu ya kuwa sehemu ya serikali. Sabaya mwenye taswira mbalimbali katika ulingo wa siasa amekuwa maarufu na kuonesha kipawa chake cha uongozi chini ya Rais Magufuli.

Mwanahabari maarufu na aliyekuwa msemaji wa klabu ya soka ya Yanga, Jerry Murro aliibuka kuwa mtetezi mkubwa wa sera za Rais Magufuli kupitia mitandao ya kijamii. Miaka michache baadaye Rais Magufuli alimteua mwanasiasa huyo kijana kuwa Mkuu wa wilaya ya Arumeru iliyopo mkoani Arusha. Fursa ya kuonesha kipawa chake kwenye ulingo wa siasa ilimfanya awe gumzo nchini.

Chanzo cha picha, Mrisho Gambo/ FACEBOOK

Maelezo ya picha,

Mrisho Gambo akiwa na hayati Rais Magufuli

Mrisho Gambo alipata nafasi ya kuaminiwa na Rais Magufuli kutoka kuwa mkuu wa wilaya hadi Mkuu wa Mkoa wa Arusha. Awali mtangulizi wa Rais Magufuli, Jakaya Kikwete alimteua kijana huyo katika nafasi ya ukuu wa wilaya huko mkoani Tanga. Uteuzi wake kuwa Mkuu wa Mkoa Arusha ulimpandisha ngazi katika ulingo wa siasa na ndio mwanzo wa mwanaisasa huyo kuhusishwa na siasa za ubunge wa jimbo la Arusha Mjini ambalo alifanikiwa kuchaguliwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2020.

Ali Hapi alianza harakati za siasa ndani ya Umoja wa Vijana wa CCM na baadaye aliteuliwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Kinondoni kabla ya Rais Magufuli kumpandisha ngazi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa. Ni kijana aliyepata nafasi kwenye ulingo wa siasa za Tanzania chini ya uongozi wa Magufuli.

Richard Ngaya, madhiri wa Chuo Kikuu cha SUA na mchambuzi wa siasa na utawala bora amemwambia mwandishi wa makala haya, "Jambo linalofurahisha kwa baadhi yao ni kuachana na utamaduni wa kujitafutia umaarufu kupitia vyombo vya habari wakidhani ni aina ya uongozi thabiti.

Njia waliyochagua sasa kuchapa kazi na kusaidiana na wananchi hiyo ndiyo siri ya kuacha urithi bora kwa Taifa kama Magufuli mwenyewe aliyejenga kwa miaka 20 ya utendaji mahiri.

Vijana wa Magufuli wengi wataendelea kuwepo serikalini hata kama siyo maeneo waliyopo bali watakuwepo kwa namna moja au nyingine na huo ndio urithi na busara zao zitawapa maisha marefu ya uongozi nchini na hakika watafika mbali,"

Wabunge vijana

Kati ya mwaka 2007 hadi 2010 nilisoma na Husna Mbwambo katika Chuo Kikuu cha Dar es salaam kwenye ambaye ni mwanasiasa kijana aliyeibuliwa na Rais Magufuli. Nafasi ya kwanza aliyopewa kuongoza ni Ukatibu Tawala katika wilaya ya Nachingwea.

Husna Mbwambo amemwambia mwandishi wa makala haya kuwa haamini kama Rais Magufuli amefariki dunia na tangu mwanzo wa uteuzi wake hadi kuamua kuwania ubunge wa viti maalumu alikopitishwa na mwenyekiti wake huyo wa CCM ni habari kubwa maishani mwake na angeweza kuandika kitabu kuhusu uongozi wa Rais Magufuli.

Chanzo cha picha, MWANA FA- INSTAGRAM

Maelezo ya picha,

Hamisi Mwijuma (Mwana FA) mbunge wa Jimbo la Muhenza mkoani Tanga ambaye pia mwanamuziki wa Bongo Flava

Wanasiasa vijana wengine waliopewa nafasi na Rais Magufuli ni Juliana Shonza ambaye aliaminiwa kwa kupewa nafasi ya Naibu waziri. Kwa sasa Juliana ni Mbunge wa Viti Maalumu akiwakilisha mkoa wa Songwe. Mwingine ni mwanamuziki wa Bongofleva Hamis Mwinjuma anayejulikana kama Mwanafalsafa au MwanaFA, ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Muhenza mkoani Tanga. Mwanamuziki huyo msomi na mhitimu wa Chuo Kikuu cha Coventry nchini Uingereza alipata nafasi ya kuwania ubunge chini ya uongozi wa Uenyekiti wa Rais Magufuli. Meneja maarufu wa wanamuziki wa Bongofleva, Babu Tale aliteuliwa kuwania ubunge wa Jimbo la Morogoro Vijijini.

Maelezo ya picha,

Hampfrey Polepole

Humphrey Polepole aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM katika awamu ya kwanza ya uongozi wa Magufuli. Hata hivyo baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020, Rais Magufuli kwa mamlaka aliyonayo alimteua Humphrey Polepole kuwa Mbunge. Wanasiasa hawa wanawakilisha vijana waliaminiwa na kupewa nafasi katika ulingo wa kisiasa bila kujali.

Diana Madukwa, Katibu wa Umoja wa Wanawake(UWT) wa CCM Dodoma Mjini, amemwambia mwandishi makala haya, "Nami nitakuwa miongoni mwa watakaosema alikuwepo Rais aliitwa John Pombe Magufuli, alifanya hiki na hiki, hakika ninamshukuru Mungu hata kuwa sehemu ya uongozi wake kwani nimefanya kazi chini yake yeye mwenyekiti wa CCM Taifa na mimi nikiwa Katibu wa UWT wilaya ya Dodoma hivyo sina budi kumshukuru Mungu. Hata waliofanya kazi na Nyerere huwa tunawasikiliza watueleze alivyoongoza. Nikiwa kiongozi kijana nitayenzi matendo yake mema kwa masilahi ya Tanzania. Na uteuzi wa nafasi ya katibu nimepata yeye akiwa anaanza madaraka ya uenyekiti wa chama chetu,"