Uswisi kuruhusu kwa mara ya kwanza wanajeshi wanawake kuvaa nguo za ndani za kike

Uswisi ina matumaini ya kuwatia moyo wanawake kujiunga na vikosi vya kijeshi

Chanzo cha picha, IMAGE COPYRIGHTFABRICE COFFRINI/GETTY IMAGES

Uswisi itawaruhusu wanajeshi wanawake kuvaa nguo za ndani za kike kwa mara ya kwanza katika jitihada za kuongeza idadi kubwa ya wanawake wanaojiunga na jeshi, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.

Chini ya mfumo wa sasa, sare za jeshi zinazotakiwa kwa wanawake wanaojiunga na jeshi zinahusisha, nguo za ndani za kiume.

Majaribio , yatakayoanza mwezi ujao, yatahusisha sare za jeshi zenye nguo za ndani za wanawake za majira ya joto na za miezi ya baridi.

Wanawake ni sehemu ya takribani 1% ya jeshi la Uswisi, lakini nchi hiyo ina matumaini ya ongezeko la mpaka 10% ya wanawake ifikapo mwaka 2030.

Marianne Binder, kutoka baraza Baraza la Taifa la Uswisi, amesema kuwa kuwapa wanawake nguo za ndani zinazowafaa kunaweza kuwapa motisha wanawake kujiunga na jeshi.

''Mavazi yamebuniwa kwa ajili ya wanaume, lakini kama jeshi linataka kuwahusisha wanawake kwa wingi, hatua zinazofaa zinahitajika kuchukuliwa,''alisema.

Wanawake, mpaka sasa, wameripotiwa kupatiwa nguo za ndani za wanaume zinazowapwaya, mara nyingi zilizo kubwa kwa umbo, ambazo zinawafanya wanawake kukosa kujiamini wakizivaa.

Msemaji wa jeshi Kaj-Gunnar Sievert amesema kuwa mavazi na vitu vingine vilivyotolewa na jeshi vilikuwa vimepitwa na wakati.

Bwana Sievert alisema mapema wiki hii kwamba mabadiliko yalikuwa yakizingatiwa kuhusiana na vifaa vingine, kama mavazi ya kupigana, mavazi ya kinga na mkoba.

Waziri wa Ulinzi wa Uswisi Viola Amherd pia ameunga mkono hatua hiyo, akisema kwamba masuala haya ya 'ulinganifu ' yanahitaji kuboreshwa.

Sare za sasa za jeshi la Uswisi zililibuniwa kwa mara ya kwanza katikati ya miaka 1980, jukwaa la Swissinfo limeripoti.