Virusi vya Corona: Aina mbali mbali za chanjo zinazotolewa Kenya zawagawanya walionacho na walala hoi

Serikali ya Kenya imeidhinisha matumizi ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Sputnik V inadaiwa kuwa na uwezo wa kinga wa asilimia 91.6 ilhali AstraZeneca ina kiwango cha kinga cha asilimia 76 .

Utoaji wa chanjo ya Urusi ya Sputnik V umezua mjadala mkubwa nchini Kenya kuhusu utaratibu wa kuiidhinisha na wanaopewa chanjo hiyo kwani imefungua wazi tofauti kati ya walio navyo na wasio navyo.

Kwa mujibu wa matangazo ya mitandaoni kuhusu chanjo hiyo ,gharama yake ni kati ya shilingi 6000 hadi 9000 na baadhi ya watu wamethibitisha kuipokea.

Hali ni tofauti na chanjo ya AstraZeneca ambayo inatolewa na serikali kwa wananchi bila malipo

Utata umetokana na nini?

Hali inayozua maswali kuliko majibu ni kwamba baada ya kuibuka hofu kuhusu usalama wa chanjo ya AstraZeneca wengi walianza kujiuliza kuhusu mbadala unaoweza kutumika na hapo ndipo chanjo hiyo ya Urusi ilipoanza kuangaziwa . Iliingizwa nchini Kenya katika hali iyo hiyo ya usiri ingawaje wengi wanaodungwa chanjo hiyo wamevutiwa na kiwango chake cha juu cha kinga dhidi ya Chanjo nyinginezo. Sputnik V inadaiwa kuwa na uwezo wa kinga wa asilimia 91.6 ilhali AstraZeneca ina kiwango cha kinga cha asilimia 76 .

Serikali ya Urusi ilikuwa awali imejitenga na makubaliano ya kuingizwa chanjo hiyo Kenya ikisema wafanyibiashara wa kibinafsi wanaohusika na kuileta chanjo hiyo wana jukumu la kufuata sheria zote za Kenya .

Kaimu Mkurugenzi wa Afya Dr Patrick Amoth siku ya Jumanne aliwaambia Wabunge na Maseneta kwamba kampuni ya Dinlas Pharma EPZ haikuwa imeafikia masharti yote yafaayo kwa chanjo hiyo kuanza kuuzwa na kutolewa nchini .

WHO haijaidhinisha matumizi ya Sputnik V

Dkt Amoth aliwaeleza Wabunge na Maseneta kwamba Kenya inalenga tu kuidhinisha chanjo ambazo zimeidhinishwa na shirika la Afya Duniani WHO na Sputnik sio mojawapo ya chanjo hizo .

Kando na chanjo ya AstraZeneca, iliyotolewa kupitia mpango wa Covax Kenya inazingatia kununua chanjo ya Johnson and Johnson inayotengezwa nchini Afrika Kusini na ni dozi inayotolewa kwa sindano moja tu .

Uhaba wa chanjo ya AstraZeneca

Wakati mjadala kuhusu matumizi ya chanjo hiyo ya Urusi ukiendelea Hospitali mbali mbali za kibinafsi jijini Nairobi zikiwemo Karen Hospital ,Hospitali ya chuo kikuu cha Aga Khan na Nairobi Hospital zimetangaza kusitisha kutoa chanjo ya Covid-19 kutokana na uhaba wake, licha ya serikali kuwa na zaidi ya dozi milioni moja.

Hospitali ya Aga Khan ilitangaza kwamba itaendelea na huduma za utoaji chanjo wakati itakapopata chanjo zaidi kutoka kwa serikali.

Wizara ya Afya siku ya Jumanne ilisema ni watu 130,575 pekee ambao wamechanjwa kote nchini kufikia sasa, licha ya dozi 806,000 kusambazwa kati ya dozi milioni 1.12 zilizopo.

Hayo yanajiri baada ya hospitali nyingine ya kibinafsi kuanza kutoza ada ya kupata chanjo ya corona ya Sputnik V ya Urusi, ambayo serikali imetoa tahadhari dhidi ya utumiaji na usambazaji wake.

Serikali ya Kenya imeidhinisha matumizi ya chanjo ya Oxford-AstraZeneca.

Viongozi 'waongozakwa mfano' kwa kuchanjwa

Katika jitihada za kuwahamasisha wakenya wengi kujitokeza ili kukubali kuchanjwa rais Uhuru Kenyatta na maafisa wake wakuu walichanjwa hadharani wiki iliyopita na wakatoa himizo kwa wananchi kukubali kuchanjwa . Rais na mkewe walichanjwa katika siku ambayo alitangaza masharti zaidi ya kuzuia msambao wa virusi vya Corona ambapo alizuia usafiri wa kuingia na kuondoka katika kaunti tano ikiwemo mji mkuu Nairobi .

Kinachosalia wazi hata hivyo ni kwamba siku zijazo ,suala la ni chanjo ipi inapewa nani litakuwa kubwa kuliko ilivyo sasa .Tayari kuna foleni ndefu ambazo zimeanza kushuhudiwa katika vituo vingi vya afya ya watu wanaotaka kuchanjwa. Kinachowahofisaha wengi ni kwamba baada ya kuripotiwa kuwepo uhaba wa chanjo inayotolewa na serikali huenda baadhi ya watu wakalazimika kutoa kiasi kikubwa cha fedha kupewa chanjo zinazouzwa kwa kiasi cha juu cha fedha kama hiyo ya Sputnik V