Changamoto ya Afrika Mashariki kushindwa kufuzu michuano ya AFCON

Mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani huko Cameroon, yamehitimishwa rasmi Jumanne.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mashindano ya kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani huko nchini Cameroon.

Jumla ya timu za taifa 23 zimekata tiketi ya kushiriki AFCON mwakani baada ya kushika nafasi mbili za juu kwenye makundi 12 ya mashindano ya kufuzu yaliyoanza mwaka 2019.

Timu hizo 23 ambazo zina tiketi mkononi ya kwenda Cameroon mwakani ni Guinea, Mali, Burkina Faso, Malawi, Mauritania, Morocco, Cameroon, Cape Verde, Ethiopia, Ivory Coast, Guinea Bissau, Guinea ya Ikweta, Sudan, Ghana, Zimbabwe, Algeria, Nigeria, Tunisia, Comoro, Misri, Gambia, Gabon na Senegal.

Idadi ya timu 24 itatimia mwezi Juni baada ya kuchezwa mechi kati ya ya Sierra Leone na Benin ambayo ilishindwa kuchezwa Jumanne iliyopita baada ya Benin kugomea majibu ya vipimo vya Covid-19 yaliyoonyesha baadhi ya wachezaji wameambukizwa huku wenyewe wakidai wachezaji hao walikuwa wazima.

Sierra Leone ambao ni wenyeji wa mechi hiyo, wanahitajika kupata ushindi wenye utofauti wa kuanzia mabao mawili ili waweze kufikisha pointi saba na kufuzu lakini kwa Benin wenyewe wanahitaji matokeo ya sare au ushindi wa aina yoyote ili wakate tiketi ya kushiriki AFCON mwakani.

Licha ya kubakia kwa nafasi moja ili itimie idadi rasmi ya timu 24 zitakazoshiriki AFCON mwakani, hakutakuwa na uwakilishi wa timu yoyote ya taifa kutoka Afrika Mashariki katika mashindano hayo baada ya timu za Tanzania, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda na Sudan Kusini zote kila moja kushindwa kufanya vizuri katika mashindano ya kufuzu.

Hii ni tofauti na Fainali zilizopita za AFCON zilizofanyika Misri ambapo timu nne za Afrika Mashariki ziliweza kushiriki ambazo ni Kenya, Tanzania, Uganda na Burundi na ikiwa ni mara ya kwanza kwa ukanda huu kuwakilishwa na idadi kubwa ya timu katika mashindano hayo yenye thamani kubwa barani humu.

Ni jambo ambalo idadi kubwa ya wadau wa mpira wa miguu na wakazi wa nchi za Afrika Mashariki hawakulitegemea kama lingetokea na wengi wao waliamini kwamba katika fainali za mwakani idadi ya wawakilishi wao ingeweza kuongezeka kutoka nne walioshiriki fainali zilizopita ama kama itashindikana basi angalau iwe tatu kama ilivyokuwa katika awamu iliyopita.

Makala hii inaangazia sababu mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia kufanya vibaya kwa timu za Afrika Mashariki hadi kupelekea zishindwe kufuzu AFCON mwakani.

Mabadiliko ya mabenchi ya ufundi

Baada ya fainali za AFCON 2019, kulifanyika mabadiliko ya makocha kwa baadhi ya timu za taifa kutoka Afrika Mashariki ambazo zilishiriki fainali hizo.

Timu ya Taifa ya Tanzania, ilifanya mabadiliko kwa kuachana na kocha, Emmanuel Amunike ambaye aliwaongoza kwenda AFCON na wakampa kibarua hicho Etienne Ndayiragije ambaye aliiongoza katika mechi nne za kufuzu kabla ya kuvunjiwa mkataba na nafasi hiyo kupewa Kim Poulsen

Kenya wao walienda AFCON wakiwa na Sebastien Migne ambaye baada ya fainali hizo aliondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Francis Kimanzi lakini naye wakati tayari ameshaanza jukumu la kuiongoza timu kutafuta tiketi ya kwenda Cameroon mwakani, aliwekwa kando na nafasi yake kuchukuliwa na Jacob 'Ghost' Mulee.

Burundi walifanya mabadiliko na kumpa jukumu kocha Jimmy Ndayizeye badala ya Olivier Ninguyeko ambaye ndiye aliwaongoza kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na jambo kama hilo pia limefanywa na Uganda ambayo wakati ikiwa imeshaanza harakati za kufuzu iliachana na Johnathan McKinstry na nafasi yake ikachukuliwa na Abdallah Mubiru.

Mabadiliko haya kwa kiasi kikubwa yalichangia kuziangusha timu hizi kwani makocha wapya hawakupata nafasi ya kutosha kusuka vikosi vyao na kuingiza mbinu na falsafa zao lakini pia kwa upande mwingine iliwaathiri wachezaji ambao walijikuta wanashindwa kujenga uelewano wa kitimu jambo ambalo lilifanya zishindwe kucheza vizuri na kupata matokeo waliyokuwa wanahitaji.

Kutokana na kila kocha kuwa na aina ya wachezaji anaowaona wanafaa kuendana na mbinu zake, vikosi vya timu hizo vilikosa muendelezo na vikajikuta vikifanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara na hivyo kusababisha kila nyakati wachezaji wawe wanaanza upya.

Mfano baada ya kocha Kim Poulsen kuanza kuinoa Timu ya Taifa ya Tanzania, alifanya mabadiliko kwa kutema zaidi ya wachezaji 10 walioshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) na kuwaita wapya ambao hawakupata fursa ya kukaa pamoja kwa muda mrefu.

Udhaifu ugenini

Timu ambazo zimekuwa zikichanga vyema karata katika mechi za nyumbani, zimekuwa na nafasi kubwa ya kufanya vyema katika hatua ya makundi ya mashindano kama hayo ya kufuzu.

Lakini hata hivyo ili kujiweka salama zaidi, kuvuna angalau pointi mbili au zaidi katika mechi za ugenini kunaiweka timu salama na katika nafasi nzuri zaidi ya kumaliza katika nafasi za juu kwenye kundi.

Hata hivyo wakati mataifa mengine yakifanikiwa kuwa tishio katika mechi zao za nyumbani na pia kukusanya pointi muhimu ugenini, wawakilishi wa Afrika Mashariki kwa bahati mbaya hawakufanikiwa kuzoa pointi tisa za mechi zote tatu nyumbani lakini pia waliambulia pointi chache ugenini.

Uganda ilipata pointi moja tu ugenini kwenye kundi kundi lake, Tanzania haikupata kitu, Rwanda ilipata pointi mbili wakati huo ikivuna pointi pointi nne tu nyumbani na Burundi ilipata pointi moja tu ugenini.

Hili lilipelekea zikusanye idadi ndogo ya pointi ambazo hazikutosha kuwapeleka AFCON

Mchango duni wa wachezaji nyota

Nyota tegemeo wengi walishindwa kuzisaidia timu za taifa kutoka ukanda wa Afrika Mashariki licha yaa matarajio ya wengi kuwa wao ndio wangekuwa chachu ya mafanikio kwa timu hizo katika mashindano hayo ya kufuzu.

Tofauti na mataifa mengine ambapo nyota tegemeo wanaotamba katika Ligi mbalimbali za soka Ulaya wamekuwa mstari wa mbele kuzisaidia, nyota wengi wa timu za taifa za Afrika Mashariki walishindwa kufanya hilo.

Michael Olunga anayetegemewa Kenya alifunga bao moja tu kama ilivyo kwa Mbwana Samatta wa Tanzania na Emmanuel Okwi na Fahadi Bayo wa Uganda.

Mchezaji pekee aliyeonyesha mchango mkubwa ni Saido Ntibazonkiza ambaye yeye aliifungia Burundi mabao manne na kuwa ni mmoja kati ya wafungaji bora watano wa walifunga magoli mengi katika hatua ya kusaka tiketi ya Afcon .

Ugumu na ushindani wa makundi

Changamoto nyingine iliyoziweka katika wakati mgumu timu za Afrika Mashariki ni ubora wa timu ambazo zilipangwa nazo katika mashindano hayo ambazo nyingi zilikuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa katika ligi mbalimbali za Ulaya na Asia.

Kenya ilikuwa sambamba na Misri iliyotwaa ubingwa wa AFCON mara saba, Togo ambayo imewahi kushiriki hadi Kombe la Dunia na Comoro ambayo kikosi chake kinaundwa naa wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya.

Burundi ilikuwa pamoja na timu ngumu za Morocco na Mauritania, Rwanda ilikuwa na timu tatu ngumu ambazo ni Cameroon, Cape Verde na Msumbiji wakati Tanzania ilikuwa na Tunisia, Guinea ya Ikweta na Libya.