Virusi vya Corona: Jifunze kufanya mambo haya kwa njia ya kisasa, hali ya kawaida huenda haitarejea

Hata baada ya kupata chanjo, wataalamu wanasema uvaaji barakoa, kuosha mikono na kukaa kwa umbali au kuepuka mikusanyiko kunahitajika bado

Chanzo cha picha, Getty Images

Umekuwa ukingoja kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja kwa hali ya kawaida kurejelewa ili maisha yako yasonge mbele, hata hivyo janga la corona limebadilisha mambo mengi kote duniani na kadri muda unavyasonga mbele inakuwa wazi kwamba kuna vitu ambavyo vimebadilika kabisa kwa sababu ya janga hilo . Kuna kazi na taratibu za hapo mbeleni ambazo hazitawahi kufanywa kama ilivyokuwa.

Fahamu baadhi ya mambo ambayo janga la Corona lilibadilisha kabisa na mengine bado yapo njiani.

Kufanya kazi kupitia simu na kuvalia barakoa ni mambo ambayo hayataondoka sasa wataalam wanasema .

Janga la coronavirus ni dharura ya umma ya kiafya na pia mgogoro wa kiuchumi, ambayo haijawahi kutokea na imeleta msukosuko katika maisha ya kila siku. Hiyo inafanya janga hili kuwa kitu kingine pia , anasema Jeffrey Cole, profesa wa utafiti katika Chuo Kikuu cha Kusini mwa California: "Bila ya maandalizi au ruhusa, tunashiriki katika jaribio kuu la sayansi ya kijamii ."

Athari za kufutwa kazi, amri za kutotoka nje na vikwazo vikubwa vya kukabiliana na ugonjwa huu "zitadumu kwa muda mrefu hata baada ya tishio lote kutoka kwa virusi kuisha," anasema Cole

"Katika siku zijazo, tutazungumza juu ya 'BC,' kabla ya korona, na baadaye."

Utafiti uliofanywa na mashirika mbali mbali yakiwemo ya kukadiria athari zitakazotokana na janga hili umeoyesha kwamba hali ya 'kawaida' ya maisha haitawahi kurejea kuwa kama ilivyokuwa hapo awali . Janga hili litabadilisha sehemu hizi 10 za Maisha yetu.

Kufanyia kazi nyumbani

Mlipuko huo uliwafanya mamia ya mamilioni ya wafanyikazi kutumia simu kutekeleza kazi zao na wakiwa nyumbani na data kutoka Mradi wa Coronavirus Disruption Project unaonyesha wengi wao wanapenda.

Asilimia arobaini na mbili ya washiriki wa utafiti walisema uzoefu huo umewafanya watake kufanya kazi kutoka nyumbani zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Zaidi ya asilimia 60 ya wale ambao wanafanya kazi ya simu walisema wanafurahia mavazi yasio rasmi na viwango vya kujipamba, kubadilika zaidi na ukosefu wa safari, na asilimia 78 walisema wanafanya kazi vizuri hata wakiwa nyumbani.

"Nadhani kutakuwa na mazuri " kutokana na usumbufu uliosababishwa na janga la corona na wafanyikazi watataka kuhifadhi mazuri hayo ya kufanyia kazi nyumbani , anasema Debra Dinnocenzo, rais wa VirtualWorks, kampuni ya ushauri ambayo inazishauri kampuni juu ya kubadilika kwa hali ya kufanyia kazi mtu akiwa mbali na ofisi.

"Watu, familia, watatumia muda zaidi kuwa pamoja' anasema." Nadhani watu watasisitiza kuwa wanataka muda zaidi wa kufanya kazi nyumbani na wasirudi kwenye mtindo wa kusafiri huku na kule kama ilivyokuwa hapo awali. "

Kumuona daktari

Kabla ya janga la corona ilikuwa kawaida kwa mtu kukubaliana na daktari wake kuhusu tarehe ya kuenda kuonana na kutibiwa ama kukaguliwa .

Hata hivyo utafiti uliofanywa mwaka jana na Chuo kikuu cha Michigan ni asilimia 4 pekee ya watu walio na umri wa miaka 50 na Zaidi waliowaona madaktari wao Kupitia njia ya video mwaka uliotangulia .wengi wao hata hawakujua Iwapo madaktari wao waliweza kuwapa usaidizi kutumia simu ama kwa njia ya video .

Preeti Malani mtaalam wa maradhi a kuambukizana anasema hilo limebadilika haraka sana

Madaktari na wagonjwa ambao hapo awali hawakuwa wamelichukua suala la kuonana kwa njia ya video sasa wameikumbatia njia hiyo. Mtindo huo unawapunguzia gharama za usafiri na changamoto kama za kutafuta maegesho wakati wanapokwenda kumuona daktari .

Pia katika sehemu kama barani Afrika ,huduma zimeanza kutolewa kupitia mitandao ambapo wagonjwa na madaktari wanaweza kutangamana bila kulazimika kukutana ana kwa ana .

Mwanzoni pia wakati janga la Corona lilipoanza ,watru wengi waliogopa kwenda hospitalini wakihofia kuambukizwa virusi vya Corona kwani wakati huo hospitali zilitajwa kama baadhi ya sehemu zenye uwezo mkubwa wa mtu kukutana na mgonjwa wa corona ambaye labda hangekuwa na dalili za wazi.

Ununuaji wa bidhaa, mboga na matunda

Sio jambo la kushangaza kwamba watu wengi walianza kununua vitu kupitia mtandaoni na hata wengine kuletwa hadi majumbani mwao .

Kufikia Mwezi machi mwaka wa 2020 zaidi ya asilimia 55 ya watu waliokuwa na uwezo wa kununua vitu kupitia mtandaoni walitumia njia hiyo badala ya kutoka nyumbani kwenda sokoni au madukani kufanya ununuzi huo .Hayo ni kulingana na utafiti uliofanywa na RBC Capital Markets .

Idadi ya walioanza kununua bidhaa kupitia mtandao ilipanda mara dufu na watu waliopakua program za kuagizia vitu nyumbani kwao waliongezeka mara dufu ,kisha idadi hiyo ikawa mara tatu Zaidi na baadaye mara nne Zaidi katika kipindi cha mwezi mmoja pekee .

Takriban nusu ya watu waliokuwa wakinunua vitu mtandaoni ambao kuviagiza vipelekwe nyumbani waliokuwa wataendelea kufanya hivyo kwa muda mrefu sana au hata katika maisha yao yote .

Kutangamana/Kukutana

Janga la Corona liliwatenganisha watu wengi na jamaa ,marafiki na wenzao kazini .ilikuwa vigumu kwa wengi kukutana ana kwa ana na mitindo ya kuonana ikawa ya kidijitali kama vile kupitia simu za video ,zoom ,facebook live na njia nyingine nyingi za kisasa .

Hatua hiyo haimaanishi kwamba watu hawatamani kukutana katika baa na kujiburudisha pamoja lakini imebainika wazi kwamba sehemu hizo ni miongoni mwa maeneo yenye uwezo mkubwa wa mtu kuambukizwa virusi vya Corona na wengi wanaepuka aina hiyo ya kutangamana .

Kuvalia Barakoa

Kuvaa barakoa ili kuzuia maambukizo kwa muda mrefu imekuwa kawaida katika nchi nyingi za Asia na jamii zingine za Wamerakani wenye asili ya Asia . Na kuja kwa COVID-19, mtindo huo umeanza kufuatwa na Wamarekani wengi na watu wengi kote duniani. Robert Kahn, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Thomas huko St.Paul, Minnesota, anatarajia hali kusalia kuwa hiyo

Chanzo cha picha, Getty Images

"Barakoa sio vifaa vya kujikinga, ni vifaa vya kinga ya kijamii," Kahn anasema. "Kila mtu anajua mtu ambaye hana kinga ya mwili au ana sababu za hatari za COVID, na nadhani hiyo inaongoza hisia ya mtu kujiambia unapokwenda nje unaweza kutaka kuvaa maski

Kwenda katika kumbi za sinema

Biashara ya watu kwenda katika kumbi za sinema imekuwa ikidorora kwa muda mrefu sasa na hatima ya mkondo wa kuiangamiza kabisa imeharakishwa na janga la Corona . Watu wengi sasa wanaweza kuzitazama filamu wazipendazo kupitia huduma za kuzipeperusha mitandaoni kama vile Netflix na Amazon Prime .

Wakati utafiti ulipofanywa kuwaliza watu walichokosa kukifanya sana wakati walipozuiwa majumbani ni wachache sana waliosema wanakosa kwenda katika kumbi za sinema.

Kituo cha Digital Future kimesema shughuli hiyo imezibwa na uwepo wa huduma na njia nyingi mbadala ambazo watu wanazitumia kutazama filamu wanazopenda .

Usafiri wa ndege

Nauli, kuchagua njia za kutumia , kuamua ndege za kusafiria na hali zingine za usafiri wa angani ni mambo ambayo yatabadilika sana wakati sekta hiyo itakaporejelea hali mpya ya kawaida baada ya janga, wataalam wanasema. Lakini wasafiri wanaweza kutarajia kwa uaminifu hali tofauti katika viwanja vya ndege na kwenye ndege zenyewe kwa miaka ijayo.

"Tutaona usafi ni muhimu zaidi," anasema Gary Leff, mwandishi wa blogi ya masuala ya usafiri wa angani . "Wakati wa hali ya kawaida , mashirika ya ndege yamejulikana kwenda miezi 18 bila ndege zao kusafishwa ili kuokoa pesa .

Sasa, hata hali iwe ngumu vipi, mashirika ya ndege yatahitaji kuwashawishi wateja kwamba ndege zao ni safi na watakuwa salama kuzitumia .

Viwanja vya ndege vitalazimika kuzidisha pia hali ya usafi.Mara nyingi vitahitajika kusafisha maeneo ya umma na kutoa nafasi za kutosha ili kuzuia watu kukaribiana .

Usafiri wa Umma

Janga hilo limeweka mifumo ya usafirishaji wa umma katika hali ngumu kwani kumekuwa na miito ya kuwataka watu wasiitumie isipokuwa iwapo ni lazima .

Baada ya janga hili itakuwa vigumu kuwashawishi watu kurejea katika mabasi yanayowabeba watu wengi katika nafasi zilizobanwa .

Kulinda Usiri wako

Kwa ajili ya ukosefu wa chanjo, kuwatafuta na kuwafuatilia watu ambao huenda wameambukizwa corona kumesababisha kutumiwa kwa programu mbali za simu zinazotumia teknolojia ya kisasa . Teknlojia hizo zimefungua wazi hatari ya watu kutoa data za kibinafsi ambazo zinafaa kuwa siri.

Hata hivyo kampuni husika zinasema zimechukua hatua kubwa ili kulinda usiri wa watu kutumia mifumo hiyo ya simu za mkononi lakini hatari bado ipo .

Wadukuzi kila uchao wanatafuita mianya ya usalama wa mifumo hiyo iliyopakuliwa katika simu za watu ili kuiba maelezo yao na hata kuwadhuru kwa njia moja au nyingine

Kunawa mikono

Wengi wanafaa kulishukuru janga la Corona kwa kujua jinsi ya kuosha mikono vizuri ( na muda unaotumika kuimba wimbo wa happy birthday mara mbili) na hakuna atakayesahau umuhimu wa njia hiyo ya kujikinga dhidi ya virusi . Kwa mujibu wa kampuni nyingi za kutengeza bidhaa za kunawa na usafi idadi ya wateja wanaonunua bidhaa hizo imekuwa ikiendelea kuongezeka .

Chanzo cha picha, Getty Images

Utafiti uliofanywa na kampuni ya Bradley unaonyesha kuwa watu wengi hadi asilimia 76 walikuwa wakitumia sabuni kuosha mikono hadi mara sita kwa siku -kiwango ambacho ni cha juu kuliko ilivyokuwa hapo awali kabla ya janga la Corona . Na asilimia 88 wataendelea kuosha mikono na kudumisha usafi wao hata baada ya janga la Corona.