Zanzibar inatarajia nini katika utawala mpya wa Muungano?

  • Rashid Abdallah
  • Mchambuzi, Tanzania
Rais Samia

Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kutokea Zanzibar. Ni baada ya miongo mitano na marais watano tangu muungano wa Tanganyika na Zanzibar uundwe 1964.

Rais wa kwanza wa Tanzania kutoka Zanzibar alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi (1985-1995) japo hakuzaliwa Zanzibar kama ilivyo kwa Rais Samia.

Urais wake umeandika historia mpya kwa Tanzania na nje ya mipaka ya nchi hiyo. Ukweli mchungu ni kwamba Urais huo umetokana na bahati mbaya ya kisiasa baada ya kifo cha John Pombe Magufuli.

Wanawake huingia katika kinyanganyiro cha kugombea Urais katika uchaguzi mkuu na katika chaguzi za ndani ya vyama. Bado hakuna aliyebahatika kuwa Rais kwa kura za wananchi.

Magufuli na Muungano

Moja kati yatakayokumbukwa juu ya utawala wa Magufuli katika kutatua kero za Muungano, ni yale makubaliano ya kihistoria yaliyotiwa saini kati ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Oktoba 2020, Ikulu jijini Dar es Salaam, makubaliano sita yaliafikiwa. Lilikuwa ni tukio la kihistoria kwa kuzingatia ukongwe wa kero na ukongwe wa muungano wenyewe.

Mambo yaliyotajwa ni, mafuta na gesi siyo mambo ya muungano, kushusha gharama bandarini kwa mizigo kutoka Zanzibar, ushirikishwaji wa SMZ kwa masuala ya kikanda na kimataifa, ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na uwepo wa vikao vya pamoja kutatua kero zilizobaki.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Samia Suluhu was first elected vice-president alongside John Magufuli in 2015

Hoja hizo zilipatiwa makubaliano, ila bado serikali zote mbili hazikuweza kujigamba kwamba kero za muungano zimeisha.

Daima viongozi wa serikali husisitiza kwa ukali juu ya kuulinda Muungano, lakini hakuna aliyefanikiwa kuufanya muungano huo kuwa wa usawa.

Licha ya juhudi za utawala wa Magufuli, utawala huo ulikosolewa pakubwa kwa namna Zanzibar ilivyokoseshwa Waziri wa kuongoza katika serikali ya Muungano pale Rais huyo wa zamani alipounda baraza lake Disemba 2020.

Hata kwa mambo yanayohusu muungano, Zanzibar inaendelea kukosa Waziri wa kuongoza Wizara yoyote hadi sasa.

Zaidi ya kuwepo manaibu mawaziri wachache kutoka nchi mshirika huyo.

Katiba Mpya na Muungano

Wachambuzi wa mambo wanaamini mfumo wa serikali uliopendekezwa katika muswada wa katiba mpya ungeleta suluhisho la moja kwa moja na pengine la kudumu juu ya zile ziitwazo kero.

Kabla ya kwenda katika Bunge Maalum la Katiba na kukutana na upinzani mkubwa uliongozwa na Wabunge na Wawakilishi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), muswada huo ulipendekeza serikali tatu.

Ulitaka uwepo wa Serikali ya Zanzibar. Pia Tanganyika iwe na serikali yake na siyo kujificha katika koti la Muungano.

Kisha iwepo serikali ya tatu itakayosimama na kushughulikia mambo yatakayo kubalika kuwa ya Muungano.

Chanzo cha picha, Twitter

Mfumo wa sasa wa Muungano

Muungano huu ulianza kwa makubaliano kuwa mambo ya muungano ni matatu tu. Yalikuwa ni ulinzi, mambo ya ndani na mambo ya nchi za nje. Ila kwa sasa ukiuliza idadi ya mambo hayo, yamepindukia ishirini.

Kero za muungano ni matokeo, shida hasa ipo katika mfumo wake.

Ndio ambao unazalisha changamoto ambazo marais wanapita na kupituka na kuziacha vilevile. Tume zinaundwa, vikao vinaitishwa lakini bado kero zipo.

Mfumo wa muungano huu ni kama nyumba yenye msingi mbovu, hata ukipaka milango rangi na kubadilisha nondo za madirisha bado tataizo la ubovu wa nyumba liko palepale.

Chukua mfano mmoja tu; swala la ujenzi na uimarishaji wa miundombinu mfano barabara siyo jambo la Muungano.

Hivyo Magufuli na Marais waliopita hawakuwajibika na ujenzi wa barabara za Zanzibar.

Tatizo ni hili, wakati Serikali ya Muungano inayo uwezo wa kuomba mikopo moja kwa moja kutoka nje ili ijenge barabara za Tanzania bara.

Zanzibar haina uwezo wa kuomba mkopo moja kwa moja kwa sababu sio nchi kamili na wala haina serikali inayotambulika.

Mfumo wa sasa ni wa serikali mbili, nchi moja (Tanganyika) imevikwa madaraka kamili kuwa ndio serikali ya Muungano, yaani serikali kuu na imebeba kila kitu. Nyingine (Zanzibar) imebaki kuwa nusu serikali inayoongoza nusu nchi.

Kwa muktadha huo malalamiko ya Zanzibar juu ya kubinywa uhuru wake wa kiuchumi na mambo mengine ni ya msingi sana. Na pande zote za muungano zinakubali kwamba muungano huu una matatizo.

Rais Samia na Muungano

Watanzania wengi wanamtumainia Rais Samia kufungua ukurasa mpya, baada ya kuhitimika utawala wa hayati Magufuli. Zanzibar pia inatumainia ukurasa mpya wa Muungano wake na Tanganyika.

Ingawa matumaini hayo kwa Zanzibar yatatokana tu na huruma za mtawala. Kwa sababu hakuna msingi imara wa kimuundo, kisheria wala kikatiba unaolazimisha usawa katika muungano.

Baada ya Makamu wa Rais Mpango kula kiapo, moja ya jukumu alilopewa na Rais Samia ni kwenda kushughulikia kero za Muungano.

Hiyo haitokuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kujaribu kutatua kero hizo.

Kwa miaka mingi utatuzi wa kero umeonekana kuwa kitendawili kilichokosa jawabu ya haraka.

Kwa maneno mafupi, chini ya mfumo wa sasa wa Muungano ni kazi ngumu kutatua kero na pande zote kuridhika.

Ni swala la kusubiri na kuona Rais mpya atakuja na msimamo gani kuhusu katiba mpya. Ingawa hata akiamua kuendeleza mchakato huo kwa kuanza pale Bunge Maalum lilipoacha.

Bado haitokuwa mwarobani kwa sababu ni muswada wenye kutaka serikali mbili kama za sasa.

Hata kama Rais wa sasa anatokea visiwani Zanzibar, kuna sababu nyingi za kuamini kwamba kero za muungano alizozikuta, zipo ambazo ataziacha kama alivyozikuta. Hasa ikiwa mfumo utabaki kuwa huu.

Zanzibar ambayo ni mlalamikaji mkubwa bado ina safari ndefu ya kuendelea kulalamika hadi pale wanasiasa watakapoamua kwa udhati kusimikia msingi wa muungano utakao zalisha haki na usawa kwa pande zote.