Gerson Msigwa ateuliwa kuwa Msemaji wa serikali, Kidata Kamishna TRA

Gerson Msigwa/TWITTER

Chanzo cha picha, Gerson Msigwa

Maelezo ya picha,

Msemaji mpya wa serikali Gerson Msigwa

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara mbalimbali na Wakuu wa Taasisi.

Miongoni mwao ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Gerson Msigwa ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali.

Nafasi hizo mbili zilikuwa zinaongozwa na Dkt.Hassan Abbas ambaye amekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Hali kadhalika aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Alphayo Kidata ameteuliwa tena kwenye nafasi hiyo.

Kabla ya uteuzi huo, Bw.Kadata alikuwa Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara.

Mnamo mwezi Novemba mwaka 2018 aliyekuwa Rais wa Tanzania Hayati John Magufuli alitengua uteuzi na kumrejesha nyumbani Bwana Kidata aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada, kisha kumuondolea hadhi ya ubalozi.

Wateule wapya watakula viapo vyao hapo kesho.

Chanzo cha picha, Maelezo

Wiki iliyopita Rais wa Tanzania Samia suluhu Hassan alitaja baraza jipya la mawaziri wakati wa hafla ya kuapishwa kwa Makamu wa Rais Dkt Philip Mpango.

''Nimefanya mabadiliko madogo ndani ya baraza la mawaziri na nitalitaja baraza ambalo nimelipanga hapa, zege hailali wanasema ni hapahapa,'' Alisema Rais Samia.

Kabla ya kuzungumzia mabadiliko ya baraza, Rais Samia alitangaza kuwa amefanya uteuzi wa wabunge watatu;

Balozi Dkt. Bashiru Ally aliteuliwa kuwa mbunge, kabla ya uteuzi huo Dkt Bashiru alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Liberata Mulamula, na Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk kuwa mbunge.

Na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Balozi Hussein Yahya Katanga ameteuliwa kushika nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi.

Mawaziri waliongia katika baraza jipya la mawaziri chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu ,Wizara ya Fedha ni Mwigulu Nchemba, ambaye anajaza nafasi ya Makamu wa Rais wa sasa Dkt Philip Mpango.

Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, kabla ya uteuzi huu alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje, pia amewahi kuhudumu kama Balozi wa Tanzania nchini Marekani.

Chanzo cha picha, HABARI MAELEZO

Aliyekuwa waziri wa wizara hiyo Palamagamba Kabudi ameteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.