Bernard Tapie: Mmiliki wa zamani wa Adidas avamiwa na kujeruhiwa nyumbani kwake

Bernard Tapie

Chanzo cha picha, Getty Images

Mfanya biashara nguli aliyekuwa na kashfa na mmiliki wa zamani wa Adidas Bernard Tapie na mkewe washambuliwa baada ya kuvamiwa katika makazi yao karibu na jiji la Paris.

Wenza hao walifungwa na nyaya za umeme, kushambuliwa na kuibiwa vito vyao vya thamani.

Bernard Tapie, mwenye miaka 78 aliyewahi kuwa waziri kwa muda mfupi anadaiwa kuwa mkali na mtata.

Amekuwa kwenye mivutano ya kisheria kuhusu rushwa na udanganyifu kwa miongo kadhaa, na kutumikia kifungo gerezani.

Bw.Tapie na mkewe, Dominique, mwenye miaka 70, walikuwa wamelala wakati wanaume wanne walipowapita walinzi na kuvunja mlango kisha kuingia ndani majira ya saa sita na nusu usiku Jumapili.

Wavamizi hao walimvuta nywele Bi.Tapie ''kwasababu walitaka kujua ni wapi walipoweka hazina yao'', meya wa Combs-La-Ville, Guy Geiffroy, aliliambia Shirika la Habari AFP.

''Lakini hakukuwa na hazina mahali hapo, na kutokana na hali hiyo kwa ghadhabu'',

Bwana Tapie alipigwa na rungu kichwani akiwa amekaa kwenye kiti.

Dominique Tapie alikimbilia kwa jirani na kupiga simu polisi. Alipata majeraha ya uso baada ya kupigwa mara kadhaa na alipelekwa hospitali,ambapo ameripotiwa kuendelea vizuri.

Bwana Tapie alikataa kwenda hospitalini.

Wezi waliripotiwa kuiba saa mbili za mkononi, ikiwemo aina ya Rolex, herein, cheni ya mkononi na pete.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Bernard na Dominique Tapie katika hafla ya uzinduzi wa ukumbi mpta wa sinema mjini Paris mwaka 2007

Bernard Tapie ni nani?

Bernard Tapie ana orodha ndefu ya mafanikio ya miongo kadhaa:

  • Waziri wa masuala ya mjini mwaka 1992-3
  • Alikuwa na hisa nyingi katika kampuni ya mavazi michezo ya Adidas
  • Mmiliki wa klabu ya Olympique de Marseille
  • Mmiliki wa magazeti ya La Provence na mengineyo
  • Muigizaji, muimbaji na mwendeshaji wa vipindi vya redio na televisheni.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Olympique de Marseille ilishinda machuano ya Ufaransa mara tano wakati Tapie alipokuaa rais, na kupeleka nyumbani taji la UEFA Champions League mwaka 1993

Lakini pia alikuwa na msururu wa mvutano wa kisheria, na kutangazwa kuwa amefilisika miaka ya 1990 na kukaa gerezani kwa miezi mitano baada ya msururu wa kesi kuhusu rushwa, udanganyifu katika kulipa kodi na matumizi mabaya ya mali za ushirika.

Akijivunia utajiri wake kwa kununua klabu ya mpira, Olympique de Marseille ilishinda ligi ya mabingwa Ufaransa, wakati akiwa mmiliki wake, lakini alishutumiwa kupanga matokeo na klabu ilivuliwa ubingwa na baadaye ilishushwa daraja.