Kwa nini baadhi ya Wakenya wakerwa na mkopo wa IMF kwa serikali yao?

Dola na Pauni

Chanzo cha picha, Getty Images

Tangazo la Shirika la Fedha Duniani IMF siku ya Ijumaa kwamba limeidhinisha mkopo wa shilingi bilioni 255 au dola bilioni 2.34 kwa serikali ya Kenya limezua hisia kali kutoka kwa baadhi ya wakenya mitandaoni.

Wengi wameshangaa mbona IMF imeidhinisha mkopo huo ilhali tayari Kenya inazongwa na mzigo mkubwa wa madeni huku wananchi wakilalamikia ongezeko la gharama ya maisha. Kero zao hizo walizitoa katika mitandao ya kijamii na hasa kwenye kurasa za akaunti za twitter na facebook za shirika la IMF.

IMF siku ya ijumaa ilisema imekubali kuipa Kenya mkopo huo ili iweze kukabiliana na athari za kiuchumi za janga la Corona pamoja na kusawazisha mzigo wake wa madeni.

Isitoshe mkopo huo ndio wa pili chini ya mwaka mmoja ambao Kenya imepokea baada ya kupewa shilingi bilioni 806 mwezi Mei mwaka jana . Kenya imesema inalenga kuzitumia fedha hizo kupunguza makali ya janga la Corona kwa uchumi wake na pia kusawazisha madeni yake.

IMF imesema deni la Kenya linaweza kulipwa lakini Taifa lipo katika hatari ya kushindwa kutekeleza malipo ya madeni yake iwapo hali ilivyo sasa itaendelea . Serikali imeshauriwa na IMF kutekeleza mabadiliko mbali mbali ya kimuundo na kiuchumi ili kumudu hali hali.

Hata hivyo wakenya waliofurika mitandao ya kijamii chini ya hashtag #Stoploaningkenya wamekerwa sana na hatua ya IMF kutoa mkopo huo wakisema hawaoni manufaa ambayo yameletwa na kiasi kikubwa cha fedha zinazokopeshwa na serikali .Wengi wanawalaumu maafisa wa serikali kwa kutumia vibaya fedha pamoja na kuzifuja nyingine bila kuzingatia maslahi ya wananchi wengi wanaohangaika .

Kulingana na taarifa ya bajeti ya mwaka wa 2021 Deni la kenya kufikia Juni 2020 lilikuwa shilingi Trilioni 7.6 sawia na asilimia 65 ya jumla ya pato la taifa.

Waziri wa Fedha wa Kenya Ukur Yatani hata hivyo ametetea kutolewa kwa mkopo huo wa IMF kwa Kenya . Yatani ameliambia gazeti moja la nchini humo-The Star kwamba Kenya inalenga kuzitumia shilingi bilioni 34.5 kukabiliana na makali ya janga la Covid 19 na kuwapa afueni wananchi wake.

Yatani amesema mkopo huo mpya ni mkakati wa serikali kukoma kuchukua mikopo ya kibiashara.

Waziri huyo amesema janga la Corona limeyumbisha kabisa uchumi wan chi hiyo na fedha zilizochukuliwa zinalenga kutumiwa kuukwamua uchumi . Amesema mikopo kama hiyo ndiyo bora ya kuweza kushughulikia upungua wa bajeti ya serikali bila kuhitajika kuchukua mikopo ya kibiashara ambayo inavutia kiasi kikubwa cha riba .

Masharyi na vikwazo vya kuzuia kusambaa kwa Corona ni hatua ambazo serikali imechukua ila imekuwa na athari kubwa kwani malefu ya watu wamepoteza kazi zao