Virusi vya Corona Kenya: Mwanamke ambaye amekataa kushindwa na virusi

Josephine and her family

Chanzo cha picha, Josephine Muchilwa

Mwanzoni mwa janga la corona, Josephine Muchilwa alikuwa akifanya kazi ya upishi, lakini kama wengine wengi nchini Kenya na ulimwenguni kote, alipoteza kazi yake. Mwandishi wa BBC Ed Butler amefuatilia ni kwa namna gani mwanamke huyo alivyomudu hali katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

"Sina kazi yoyote, sina maisha, sina chakula chochote cha watoto wangu."

Maelezo hayo ya Josephine ni ukweli ulio wazi juu ya athari za hatua za kudhibiti virusi vya corona zilizowekwa mwaka mmoja kwa watu wengi maskini.

Siku chache tu baada ya serikali kutangaza hatua kali za kutotoka nje kuzuia kuenea kwa Covid-19, mama huyu asiye na mume , anayeishi katika mtaa wa mabanda wa Kibera mjini Nairobi alielezea shida ambayo watu wengi walikuwa wakikabiliwa nayo ghafla.

Kazi yake ya mshahara mdogo kama mpishi wa shule ya hapi mtaani iliisha wakati wanafunzi walipoambiwa kusomea nyumbani. Alibaki akijiuliza ni vipi atailisha familia yake ya watoto wanne.

"Ninajadiliana tu na Mungu," Josephine mwenye umri wa miaka 31 amekiambia kipindi cha BBC cha Business Daily. "Sijui nifanye nini."

Lakini baada ya kusikia juu ya shida yake, wasikilizaji kadhaa wakarimu waliingilia kati na kutoa msaada.

Haikuwa kiasi kikubwa - karibu $ 150 (Pauni 110) - lakini ilitosha kumruhusu Josephine kuanzisha biashara ya matunda na mboga.

Akisafiri kwa basi kwenda kwenye soko kubwa la jumla katikati mwa mji mkuu wa Kenya, alinunua magunia ya kilo 25 ya vitunguu, nyanya na zaidi, akirejesha bidhaa hizo Kibera ambapo alianza kuuza katika kibanda kidogo cha mbao.

Chanzo cha picha, Josephine Muchilwa

Josephine kisha akaanza kutuma shajara za sauti kutoka kwa chumba chake kimoja, kilichokuwa na ukuta wa matope juu ya juhudi zake za kufanya biashara yake ifaulu.

Hii ilikuwa ikitokea wakati Kibera, ambacho ni kitongoji kikubwa cha mabanda katikati mwa jiji la Nairobi ilipokuwa ikiingia katika hali mbaya.

Kwa kuwa wakazi wengi wa eneo hili hufanya kazi za nyumbani, kusafisha au madereva, waliathiriwa vibaya na kuvurugika kwa hali ya uchumi kwani waajiri wao ambao ni matajiri waliwauliza wakae mbali kwa kuhofia wataleta maambukizi.

'Watoto wanaweza kula'

Walakini, mwanzoni licha ya hali mbaya, Josephine alionekana kupiga hatua nzuri . Angepata wateja wanane au 10 kwa siku.

"Angalau leo nilipokea faida ya shilingi 170 ($ 1.50)," aliniambia katika mazungumzo wakati mmoja Mei iliyopita. "Watoto wako sawa, wanafurahi, angalau wanakula."

Lakini kila wakati alikuwa akipambana na hali mbaya.

Josephine hakuwa na uzoefu kama mfanyabiashara, wilaya hiyo ilikuwa chini ya amri ya kutotoka nje, kulikuwa na upekuzi wa polisi wa kawaida na vurugu kwa mtu yeyote aliyepatikana baada ya vizuizi kuingia na kusafiri nje ya mipaka ya jiji ilipigwa marufuku kabisa.

Isitoshe alikuwa na watoto wake wanne aliyofaa kuwajali na kulikuwa na ongezeko la visa vya uhalifu na hofu ya unyanyasaji wa kijinsia katika makazi duni.

"Kesi za ubakaji zinaongezeka," alisema. "Nikiacha watoto peke yao mtu yeyote anaweza kuingia na kuwafanyia chochote."

Na pia ni watu wachache sasa waliokuwa na kipato cha kulipia kile alikuwa akiuza. Majirani zake kama yeye walikuwa hawana kazi, wakiishi kutokana na akiba walizokuwa nazo.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Picha katika mitaa ya Kibera ikikumbusha watu kuvaa barakoa

Basi janga likatokea kweli. Josephine aliugua malaria na alilazimika kukopa pesa za matibabu kutoka kwa mkopeshaji wa pesa.

Kuongezeka kwa madeni ya kibinafsi kama hili inaonekana kuenea katika makazi ya mabanda. Mkopeshaji mmoja , aliyeitwa Rodgers, aliambia BBC kwamba alikuwa ameishiwa pesa ya kukopesh kuonyesha jinsi watu walivyokuwa na uhitaji mkubwa wa fedha

Wengi walishindwa kulipa mikopo, alisema, kwa hivyo alikuwa akiuza bidhaa za nyumbani ambazo walitoa kama dhamana.

Kwa upande wake, Josephine hakuwa na chochote cha kumpa kama dhamana.

Kioski chavunjwa

Hadi leo anaogopa kwamba mkopo wake ambao hajaulipa, unaofikia dola 30, unaweza kumletea shida kubwa.

Matarajio ya kulipa mkopo wake yalizidi kuwa mbali wakati mnamo Juni mwaka jana, tingatinga za serikali ziliingia kIbera kulima sehemu hiyo ambapo kibanda chake kilikuwepo ili kutengza nafasi ya mradi wa ujenzi wa reli . Serikali ilisema waliokuwa wamejenga katika eneo hilo walikuwa wamepewa ilani nyingi kuondoka . Lakini kama mpangaji, Josephine alisema hakuwa amepewa onyo yoyote.

Na kuzidisha masaibu hayo ni kwamba alikuwa ameweka tu idadi kubwa ya ya bidhaa zaidi katika kibanda chake amabazo zilipondwa pamoja na kibanada hicho cha mbao. Kwa mara nyingine, ndoto yake ya kufanikiwa kama mfanyibiashara ilikuwa imevunjika .

"Siku hiyo nililia sana - karibu siku tatu. Ninahisi uchungu sana. Sikuweza hata kula. Na ninapoangalia hali ya maisha yangu sasa, ikawa ngumu sana."

Janga lenyewe limewapata mamilioni nchini Kenya na kwingineko kwa njia hii, inaonekana.

Chanzo cha picha, Josephine Muchilwa

Janga lenyewe limewapata mamilioni nchini Kenya na kwingineko kwa njia hii, inaonekana.

Kulingana na takwimu rasmi za serikali kumekuwa na vifo 2,250 vya Covid nchini Kenya ingawa wataalam wengine wanaamini idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi kuliko hiyo.

Lakini kwa watu wa Kibera, kuna hisia kwamba jamii zao zimekuwa zikilengwa kikatili na masharti ya serikali ya kupambana na kusambaa kwa virusi vya Corona na kwamba hatua ya polisi kutekeleza masharti hayo mara nyingi imekuwa ya kutumia nguvu kupita kiasi

"Watu hawa wanaoishi chini ya $ 2 kwa siku, wanajua ikiwa utaugua, utakufa," anasema Kennedy Odede, mwanaharakati aliyezaliwa Kibera, na mwanzilishi wa shirika la uhisani la Shining Hope.

"Tunataka serikali kuhakikisha kuwa makazi duni yanapewa kipaumbele, kuhakikisha tunakuwa na barabara, huduma bora za afya, maji safi."

Lakini serikali haiko tayari kuondoa vizuizi hivyo hivi karibuni. Mwezi uliopita, amri ya kutotoka nje ya nchi nzima wakati wa usiku iliongezewa muda huku pakiwa na ushahidi kuwepo wimbi la tatu la maambukizo ya Covid.

Mwaka mmoja baada ya kuzuka kwa ugonjwa huo, Josephine anaendelea kuhangaika.

Bado hana kazi thabiti ya kumpa mapato na watoto wake wanalazimika kuishi kwa bakuli moja ya uji kwa siku.

"Siku moja nina ndoto ya kuwa daktari," binti yake mkubwa, Shamim wa miaka 11 aliniambia. "Leo naota chakula."

Josephine ameweza kupata kazi za mara kwa mara kama msafishaji, lakini mwanamke mmoja, aliniambia, bado hajamlipa kwa kazi ya siku tatu.

Lakini kutokana msaada wa Shining Hope, sura mpya katika maisha yake inaweza kuanza hivi karibuni.

Anajifunza kuwa mshonaji, ili kupata kazi ambazo wafanyikazi wenzi wenye uzoefu wanadai zinaweza kuwapatia dola kadhaa kwa siku.

Ingawa masomo ya miezi 12 iliyopita yamekuwa magumu sana, Josephine anaendelea kuwa na matumaini kwamba yeye na watoto wake wataibuka washindi kutokana na mateso yote waliyopitia.