Jinsi Saudi Arabia inavyohusika katika mzozo wa Jordan

A frame maker in a frame shop displays pictures of King Abdullah II bin Al-Hussein king of Jordan, in Amman, Jordan, 4 April

Chanzo cha picha, EPA

Maafisa wa Saudi Arabia wamepinga vikali madai kwamba nchi yao ilihusika katika jaribio la mapinduzi Jordan.

Siku ya Jumamosi Mwanafalme maaruufu aliyekuwa mtawala mtarajiwa, Hamzah aliwekwa chini ya kifungo cha nyumbani kwa tuhuma za kuhujumu usalama wa kitaifa baada ya kuhudhuria mikutano ya kijamii ambapo Mfalme Abdullah, ndugu yake wa kambo, alikosolewa hadharani.

Mwanamfalme Hamzah wakati huo aliwasilisha kanda mbili za video kwa BBC, akitaja nchi yake kuwa fisadi na isiyokuwa na uwezo akiongeza kwamba watu wanaogopa kuzungumza kwa kuhofia kuchukuliwa hatua na vikosi vya usalama.

Mzozo huo umetulia baada ya mjomba wa Mfalame kuingilia kati, lakini kumekuwa na minong'ono kuhusu jukumu la Saudi Arabia katika mzozo huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Faisal bin Farhan, alizuru mji mkuu wa Jordan, Amman akiwa na ujumbe wake kama ishara ya "kumuunga mkono Mfalme wa Abdullah wa Jordan na serikali yake". Hii wanasema, ilikuwa hatua ya kuonesha msimamo wa Saudia Arabia kuhusu suala hilo na kupuuza madai yanayoashiria nchi hiyo ilikuwa na njama ya kudhoofisha jirani yake ni "upuuzi mtupu".

Saudi Arabia inahusika vipi?

Wakati mzozo ulipofikia kilele wikiendi iliyopita, Maafisa wa Jordan walisema mashirika yao ya usalama yamekuwa yakifuatilia mienendo ya Mwanamfalme Hamzah na maafisa wengine kadhaa kwa muda.

Walizungumzia watu wasiojulikana "kutoka nje" ambao wamekuwa wakijihusisha na kile wametaja kuwa njama ya kudhoofisha nchi na familia tawala ya Hashemite - madai yaliyopingwa na Mwanamfalme Hamzah.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mfalme Abdullah na mke wake Malkia Rania (Mwisho kulia kwenye picha) walipohudhuria harusi ya Mwanamfalme Hamzah na mke wake wa kwanza Noor (kulia) pamoja na mama yake Hamzah Malkia Noor (wa kati) mwaka 2004

Kilichojitokeza katika mzozo huo ni mambo mawili tofauti. Kwanza Mwanamfalme Hamzah, Mwana wa mkubwa wa kiume wa Mflame marehemu Hussein, aliyekosana na wakuu wa usalama alipokutana na viongozi wa kijamii hivi karibuni. Wengine waliohusika ni maafisa wanaodaiwa kuwa na mafungamano na nchi nyingine moja.

Mmoja wa viongozi mashuhuri waliokamatwa Jumamosi ni Bassem Awadallah,Mkuu wa zamani wa mahakama ya kifalme ambaye sasa ni mshauri wa Mwamfalme Mohammed bin Salman. Ana uraia pacha wa Saudia na Jordan na anaonekana kuwa na msimamo wa kadri katika makongamano ya Saudi Araia ya masuala ya uwekezaji.

Gazeti la Washington Post liliripoti kuwa waziri wa mambo ya nje wa Saudia na ujumbe wake walizuiliwa kuondoka Jordan hadi watakapoandamana na Bassem Awadallah kwenda Riyadh. Ripoti ambayo maafisa wa Saudi Arabia wamesema si kweli.

Bassem Awadullah ana ushawishi mkubwa kimataifa, ikiwa ni pamoja na uhusiano wa karibu na Mwanamfalme na kiongozi wa Milki za Kiarabu UAE, Mwanamfalme Mohammed bin Zayed.

Ameripotiwa kuhusika katika mkakati wa ununuzi wa ardhi wa Palestina unaoungwa mkono na UAE-karibu na Yerusalem.

Saudi Arabia na Jordan, japo zinatofautiana pakubwa kiuchumi, zina uhusiano wa kihistoria wa muda mrefu.

Kwa miongo kadhaa nchi hizi mbili zimekuwa na uhusiano ambao umetokana na mafungamano ya kijamii katika mipaka yao ya pamoja jangwani.

Raia wa Jordan walikuwa wakiingia na kutoka Saudi Arabia, wakibadilishana bidhaa na kujuliana hali huku wakilisha mifugo yao.

Kama watawala wa Kiarabu wa Kisunni waliosalia katika sehemu ya ulimwengu misingi yao ili iliyumbishwa na vuguvugu la mapinduzi ya nchi za kiarabu lakini watawala wa Saudia na Jordan walishirikiana kwa maslahi ya mataifa yao.