Marekani yajiunga na mazungumzo ya Vienna kufufua tena makubaliano ya nyuklia ya Iran

European External Action Service (EEAS) Deputy Secretary General Enrique Mora and Iranian Deputy at Ministry of Foreign Affairs Abbas Araghchi wait for the start of a meeting of the JCPOA Joint Commission in Vienna, Austria (6 April 2021)

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Maafisa kutoka nchi sita wanahusika katika makubaliano ya nyuklia walifanya mazungumzo ya maandalizi Jumanne

Marekani imejiunga kwenye mazungumzo mjini Vienna yaliyolenga kufufua makubaliano ya nyuklia ya Iran, ambayo serikali ya Trump ilijiondoa mwaka 2018.

Rais Joe Biden amesema kuwa anataka kurejea kwenye makubaliano hayo.

Lakini nchi sita zilizosalia zinahitaji kutafuta njia ili kuhakikisha kuwa anaondoa vikwazo vilivyowekwa na mtangulizi wake na kwa Iran kurejea katika makubaliano kuhusu masharti ya program yake ya yuklia.

Iran imesema haitakutana na Marekani ana kwa ana mpaka pale itakapoondolewa vikwazo.

Maafisa wa kidiplomasia kutoka Uingereza, Ufaransa Ujerumani , Urusi na China wanahudhuria mazungumzo hayo.

Balozi wa Urusi wa mashirika ya kimataifa mjini Vienna, Mikhail Ulyanov, amesema mazungumzo yaliyofanya Jumanne yalikuwa na ''mafanikio '' huku makundi mawili ya wataalam yanayoshughulikia masuala ya vikwazo na masuala ya nyuklia kupewa jukumu la kutambua hatua madhubuti za kusonga mbele.

Bwana Ulyanov ameongeza kuwa wataalam wameanza kazi yao, lakini wameeleza kuwa kurejeshwa tena kwa makubaliano hayo hakutakuwa kwa haraka.

"''Itachukua muda. Kwa kiasi gani? Hakuna anayejua. Jambo la maana…ni kuwa kazi ya kufikia malengo hayo imeshaanza.''

Msemaji wa Wizara ya mambo ya nje Ned Price pia alitoa tahadhari kabla ya mkutano huo akiwaambia waandishi wa habari jijini Washington siku ya Jumatatu kuwa: '' Hatutarajii mafanikio ya mapema na haraka, kwani tunatatarajia mazungumzo kuwa magumu.''

Mjumbe maalumu wa Marekani nchini Iran, Robert Malley, alisema wiki iliyopita kuwa lengo lake ilikuwa ni ''kuona namna tunayoweza kukubaliana kwa pande zote mbili na kwamba Marekani ilijua kuwa ''itakwenda kuondoa vikwazo ambavyo vinatofautiana na makubaliano yaliyofikiwa na Iran''.

Maelezo ya video,

Milipuko ya Iran: Nani yuko nyuma ya ‘mashambulio’ hayo katika maeneo muhimu?

Alipoulizwa kuhusu suala hilo Jumanne, Msemaji wa serikali ya Iran Ali Rabiei amesema Iran imeona msimamo wao ni wenye uhalisia na wenye matumaini''.

''Tunaamini kuwa tuko pazuri, na kama nia ya Marekani itathibitika kuwa ya kweli, itakuwa ni ishara nzuri kwa mustakabali wa makubaliano haya,'' aliongeza.

Bwana Rabiei alisisitiza kwamba Iran ilikuwa "tayari kurudi kwenye majukumu yake yote kwa muda mfupi zaidi baada ya kuthibitisha kutimizwa kwa majukumu ya nchi nyingine pia''.

Chanzo cha picha, EPA

Iran, ambayo inasisitiza kuwa haina mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia , iliamua kukiuka makubaliano muhimu yaliyokuwepo kwenye mkataba.

Iran iliendelea na kuvunja makubaliano hayo katika shughuli zake za urutubishaji wa madini ya Urani ili kuweka shinikizo kwa Marekani.

Mkataba unairuhusu Iran kuzalisha na mpaka asilimia 3.67% ya madini ya urani ambayo inaweza kutumika kuzalisha mafuta kwa ajili ya mafuta ya vinu vya nyuklia.

Urutubishaji wa madini ya Urani kwa asilimia 90 yanaweza kutumuka kutengeneza silaha za nyuklia.