Je Rais Samia ni mvinyo mpya kwenye chupa ya zamani au chupa mpya yenye mvinyo wa zamani?

  • Ezekiel Kamwaga
  • Mchambuzi
Samia Suluhu Hassan

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Si mara nyingi ambapo uchambuzi wa kisiasa hujijenga kwenye chupa na mvinyo; lakini hii ni mojawapo ya mara chache ambapo hakuna mfano mzuri unaosadifu hali kuliko huu.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ameingia madarakani kufuatia kifo cha mtangulizi wake John Magufuli Machi 17 mwaka huu. Yeye na Magufuli waliingia madarakani kwa tiketi moja mwaka 2015; Magufuli akiwa Rais na Samia Makamu wake na kama uhai wa Magufuli usingesitishwa ghafla, mambo yote ya utawala wa Awamu ya Tano yangewaweka katika fungu moja daima dumu.

Hata hivyo, tangu aingie madarakani, Samia ameonekana kuwa tofauti na mtangulizi wake huyo katika mambo anuai kuanzia kwenye uzungumzaji, namna ya kufikisha ujumbe, uungwana na katika mambo mengine madogo madogo wakiwamo wasaidizi wake wanaoonekana naye kila siku.

Je, Mama Samia amefanya nini yaliyo tofauti na mtangulizi wake na nini hasa watu wanakiona kwamba - hata katika hatua hizi za awali - bado anaonekana ataendeleza yale ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele na wengi?

Mchezo wa Samia ndiyo mchezo wa CCM

Katika mahojiano niliyowahi kufanya na mmoja wa waasisi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Pius Msekwa, miaka michache nyuma, alipata kunieleza mojawapo ya siri kubwa ambazo zimekifanya chama hicho kubaki madarakani kwa muda mrefu kuliko karibu vyama vyote vya Afrika.

Aliniambia siri iko katika namna ambavyo chama kimekuwa kikibadilisha viongozi wake kila baada ya miaka 10 huku kiongozi mpya akionekana tofauti na mtangulizi wake ambaye kwa kawaida watu huwa wameanza kumchoka baada ya muda wake madarakani.

Julius Nyerere ndiye pekee aliyekaa madarakani kwa zaidi ya miaka 10 lakini aliyemfuatia, Ali Hassah Mwinyi, si tu alionekana kijana - ingawa hawakupishana umri sana - lakini alikuwa wa dini tofauti, maono tofauti, muungwana zaidi na mpole.

Mwinyi pia alikuwa akizungumza kuhusu kuachia soko lifanye kazi zake, kuachia wafungwa wa kisiasa, kuruhusu vyama vingi na vyombo huru vya habari na kuwapa watu uhuru wa kukosoa na kuzungumza.

Baada yake alikuja Benjamin Mkapa ambaye alikuja wakati Mwinyi akiwa anaitwa Mzee Ruksa; kwamba serikali yake ikiruhusu rushwa, ubadhirifu na uozo mwingine. Mkapa akaja na taswira ya mtu mchapakazi, asiye na madoa ya rushwa wala mzaha na wabadhirifu.

Baada ya miaka yake 10 madarakani, utawala wa Mkapa ukapewa jina la "Ukapa" ikimaanisha fedha zilikuwa nyingi mikononi mwa serikali lakini wananchi hawakuwa na kitu mifukoni.

Alipoingia Jakaya Kikwete, ikawa sawa na kupata hewa safi. Wakati Mkapa alikuwa akionekana kutotabasamu kila wakati, Jakaya alikuwa akitabasamu muda wote kiasi cha kufikia kuwaambia wananchi kwamba tabasamu lake lisiwadanganye.

Lakini, katika wakati wa Kikwete, wananchi hawakulia tena Ukapa kwa sababu fedha kwa kiasi kikubwa zilitoka serikalini na kuwafikia wananchi. Utawala wa Kikwete ndiyo uliofanikiwa kuwatoa Watanzania wengi zaidi katika umasikini kuliko utawala mwingine wowote uliopita.

Katika siku zake za mwisho za utawala wake, kulikuwa na tuhuma kwamba serikali yake ililea rushwa kiasi cha baadhi ya wapinzani wakisema Kikwete alikuwa Rais dhaifu kiasi kwamba sasa Tanzania ilihitaji Rais aliye tofauti na Jakaya.

CCM ikamleta Magufuli ambaye kwa haiba, malezi na tabia alikuwa tofauti na Kikwete. Wananchi wakampokea Magufuli - walau katika miezi yake ya awali - kwa sababu ilionekana Tanzania ilihitaji mtu wa aina hiyo baada ya miaka 10 ya Jakaya.

Ingawa Samia ameingia madarakani baada ya takribani miaka sita ya Magufuli na kuwa wote walikuwa katika chama na timu moja; Mzanzibari huyo ameanza kuonyesha mambo yanayoonyesha huenda yasiwe kama yalivyozoeleka miaka mitano nyuma.

Ni mambo gani mapya anayofanya Samia katika muda mfupi?

Chanzo cha picha, Ikulu, Tanzania

Uteuzi wa viongozi wapya ni jambo linalotarajiwa kwa kila Rais mpya anayeingia madarakani lakini jambo ambalo husubiriwa na wengi ni namna kiongozi atakavyoshughulika na mambo ya kisera au utendaji ya mtangulizi wake.

Katika hotuba yake ya kuwaapisha makatibu wakuu na viongozi wa taasisi za umma, Samia alitumia zaidi ya dakika 15 kuzungumza namna staili ya ukusanyaji mapato kibabe na isivyo na tija katika uchumi.

Huo umekuwa ujumbe wa Samia tangu siku yake ya kwanza madarakani. Ujumbe huo ni muhimu kwa sababu utawala wa Magufuli ulijulikana kwa staili ya ukusanyaji kodi kibabe na wakati mwingine ukihusisha hadi vyombo vya dola.

Samia ambaye amewahi kufanya kazi katika sekta binafsi, amekuwa akisisitiza kuwa endapo wawekezaji wataona mazingira ya Tanzania hayafai, wataondoka kwenda kwenye mazingira rafiki. Tayari Samia amembadili aliyekuwa Kamishina Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Edwin Mhede, ambayo ndiyo wahusika wakuu wa ukusanyaji wa mapato.

Jambo lingine kubwa kwenye utawala wa Samia linahusu msimamo wa serikali yake kuhusu ugonjwa wa Corona. Mtangulizi wake alikuwa akichukua hatua zilizokosolewa vikali na wataalamu ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) na sasa Rais Samia inaonekana atafuata njia nyingine.

Rais huyo wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania amesema ataunda timu ya wataalamu ambao watafanya utafiti kuhusu jambo hilo na kushauri namna serikali itakavyochukua hatua kuhusu ugonjwa huo ambao hadi sasa umeua mamilioni ya watu duniani kote.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mama Samia alikuwa Makamu wa Hayati Rais John Magufuli toka mwaka 2015.

Utawala wa Magufuli ulikuwa ukifahamika pia kwa kuchagua au kuteua watu katika nafasi mbalimbali kwa kuzingatia maono yake binafsi lakini inaonekana Samia anarudisha nchi kwenye kuchagua watu kulingana na taaluma zao au mambo wanayoweza kuyafanya kwa ufanisi zaidi.

Makamu Rais huyo wa zamani ameonyesha pia njia mpya kwa kuamuru kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyofungiwa na kutaka watu wasipelekwe mahakamani kama hakuna ushahidi wa kutosha wa makosa hayo.

Bahati mbaya, matukio ya kubambikia watu kesi na kupelekwa mahakamani kwa makosa ambayo matokeo yake huwa ni kuachia watu huru kwa kuwalipisha faini kubwa ni baadhi ya hiba (legacy) ya utawala uliopita.

Mvinyo uleule chupa mpya?

Kuna maeneo mawili ambayo wakosoaji wa Samia wanaona bado hajaonyesha makali yake kama kwenye maeneo hayo mengine mawili.

Kwanza, bado hajaonekana hadharani akiwa amevaa barakoa. Inafahamika kwamba zipo njia nyingi za kuonyesha uwajibikaji kwenye suala hilo lakini uvaaji wa kitambaa hicho ni namna ya wazi na inayoonekana kwa wengi.

Huenda Samia hataki kuonekana akiwa amevaa barakoa muda mfupi tu baada ya kifo cha Rais Magufuli na pengine utafiti huo wa wataalamu unaweza kumpa fursa ya kuonyesha mfano kwa kuvaa barakoa hadharani.

Jambo la pili liko kwenye uteuzi wa wanawake katika nafasi za juu za viongozi. Kwenye Baraza la Mawaziri, amemuongeza Balozi Liberata Mulamula na kufanya wanawake kufikisha asilimia 21 ya mawaziri wake wote kutoka asilimia 17 aliyoikuta.

Hata hivyo, bado hajafanya uteuzi wa aina yake ambao utawafanya watu kuelewa kwamba sasa nchi ina mwelekeo mpya. Kikwete alifanya hivyo kwa kuwateua Zakhia Meghji na Asha Rose Migiro kuwa mawaziri wa fedha na mambo ya nje mtawalia - wa kwanza katika historia ya Tanzania.

Tangu kupata Uhuru wake mwaka 1961, Tanzania haijawahi kuwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mwanasheria Mkuu, Waziri wa Ulinzi na taasisi nyingi nyeti za dola wa jinsia ya kike. Wengi wanataraji pengine huu ndiyo wakati wa kuvunja ukuta huo wa kioo wakati Rais akiwa mwanamke.

Bahati nzuri ya Samia ni kwamba wakati uko upande wake. Na kwa sasa, japo katika miezi hii mitatu ya kwanza, fungate ya kawaida ya kiongozi mpya na wananchi wake huwa bado ina nguvu.

lk