CAG ataja changamoto nne zinazoikabili ATCL

Ndege ya Dreamliner ilipowasili Tanzania Julai 2018

Chanzo cha picha, IKULU TANZANIA

Maelezo ya picha,

Ndege ya Dreamliner ilipowasili Tanzania Julai 2018

Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini Tanzania, Charles Kicheere, amesema Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limeingiza hasara ya takribani Shilingi Bilioni 150 kwa miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa CAG, kwa mwaka mmoja uliopita, ATCL imeingiza hasara ya Shilingi bilioni 60. Bw. Kicheere ameyasema hayo leo Alhamisi alipokuwa akiwasilisha ripoti ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 Bungeni mjini Dodoma.

"Nilifanya ukaguzi wa kiutendaji katika shirika la ndege na kubaini yafuatayo; Hadi kufikia Juni serikali ilikuwa imenunua ndege nane kwa gharama ya shilingi trilioni 1.28 katika juhudi za kufufua kampuni ya ndege...Pamoja na kununua ndege hizo, kwa miaka mitano serikali imeisaidia kampuni ya ndege kiasi cha shilingi bilioni 153 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji na maendeleo...kampuni imekuwa ikiingiza hasara kwa miaka mitano mfulululizo ya shilingi bilioni 150," ameeleza.

CAG pia amezitaja changamoto zinazoikabili ATCL na kushauri zishughulikiwe na serikali ili kampuni hiyo ili kuimarisha utendaji kazi wake.

Changamoto ya kwanza ni ukosefu wa uzoefu kwa bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo: " Nilibaini kuwa bodi ya wakurugenzi haina mjumbe hata mmoja ambaye mwenye uzoefu wa masuala ya usafiri wa anga. Hii ni changamoto kubwa, inabidi tuwe na wajumbe ambao walau wana uzoefu kwenye maeneo hayo kuisaidia menejimenti katika mikakati ya kuendesha shirika."

Changamoto ya pili ni uendeshaji wa shirika hilo wakati wa janga la corona lilipopamba na kulazimisha ndege zote kutokufanya safari. CAG ameeleza kuwa japo ndege zilikuwa hazitumiki, ATCL ailikuwa ikiendelea kutozwa gharama za ukodishaji ndege kutoka kwa Wakala wa Ndege za Serikali za Tanzania (TGFA) ambao ndio wamiliki wa ndege hizo.

"Hilo linatokana na mkataba baina ya TFGA na ATCL kukosa kifungu cha kuacha kulipishwa wakati wa majanga (force majeure). Katika kipindi baina ya Machi na Juni 2020 wakati shughuli zimesimama (kutokana corona) ATCL ilitozwa bilioni 15 kwa ajili ya ukodishwaji wa ndege wakati zilikuwa zimesimama, kwa hiyo hii inachangia hasara tunazozitaja," ameeleza CAG.

Bw. Kicheere ameeleza kuwa anatambua kuna majadiliano yanaendelea juu ya kubadilishwa kwa mkataba huo na ametoa rai kuwa kukamilika kwake kutaisaidia ATCL.

Chanzo cha picha, IKULU

Maelezo ya picha,

ATCL ilifufuliwa mara baada ya hayati John Pombe Magufuli kuingia madarakani nchini Tanzania mwaka 2015 kutoka kutokuwa na ndege angani na kufikisha ndege nane zilizopo sasa.

Changamoto ya tatu iliyotajwa na CAG inayoikabili ATCL ni madeni iliyoyarithi kutoka nyuma ambayo imemebeshwa kampuni mpya hata baada ya kufufuliwa.

CAG ameeleza kuwa madeni hayo yamekuwa kutokana na riba yake kuendelea kuongezeka na yamezuia ndege za shirika hilo kuenda baadhi ya nchi kwa hofu ya kukamatwa.

Ubora wa viwanja vya ndege nchini Tanzania pia ni moja ya changamoto kubwa zinazoikabili shirika hilo. Kwa mujibu wa CAG baadhi ya viwanja ndege haziwezi kutua usiku na kwengineko ndege haziwezi kutua ikiwa imepakia abiria wanaotakiwa.

"Kwa mfano Dodoma Airbus haiwezi kuja na abiria 162 kwa sababu uwwanja huo hauwezi kuhimili hilo. Na viwanja vipo kadhaa hapa nchini."

CAG ametoa wito kwa serikali kuangalia changamoto hizo, madeni pamoja na hasara zinazolikabili shirika hilo.

ATCL ilifufuliwa mara baada ya hayati John Pombe Magufuli kuingia madarakani nchini Tanzania mwaka 2015 ambapo alilinyanyua shirika hilo kutoka kutokuwa na ndege angani na kufikisha ndege nane zilizopo sasa zikiwemo ndege kubwa mbili aina ya Boeing Dreamliner.