Umoja wa Mataifa wataka hatua kuchukuliwa dhidi ya tabia ya wanawake kufungwa kizazi kwa lazima

Zishilo Dludla looking out of a window

Chanzo cha picha, BBC News

Maelezo ya picha,

Ushahidi wa kulazimishwa kufungwa kizazi umepatikana katika nchi 38 miaka 20 iliyopita.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ieonesha kuwa takriban nchi 38 zimeendeleza tabia ya kufunga kizazi kwa lazima katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, huku baadhi ya kesi hizo zikijumuisha wanawake waliofungwa kizazi kinyume na matakwa yao wakati wanajifungua.

Umoja wa Mataifa imetoa wito wa kusitishwa kwa tabia ya kufunga watu kizazi kinyume na matakwa yao ambayo imejitokeza katika kila bara duniani kulingana na utafiti uliofanywa na Profesa Sam Rowlands, na kutaka serikali ichukue hatua dhidi ya wanaotekeleza tabia hiyo.

Jamii za waliowachache, wanawake wanaoishi na ugonjwa wa virusi vya HIV na makundi ya waliotengwa ikiwemo waliobadilisha jinsia zao wote wamejikuta katika hali kama hizo kote duniani.

"Kuna historia ndefu ya ubaguzi duniani na nyanyasaji unaohusishwa na kufungwa kizazi kwa lazima, ambayo bado inaendelea hadi hii leo," anaelezea Dr. Tlaleng Mofokeng, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki ya kupata afya. "Hilo pekee, ni ukukaji mkubwa wa haki za binadamu."

Zishilo Dludla anasema hakukubali kufungwa kizazi wakati anajifungua katika hospitali moja nchini Afrika Kusini mwaka 2011.

"Kufungwa kizazi kwa lazima kumekuwa kitendo cha kinyama sana kwangu, kwasababu sijawahi kutaka kufanya hivyo, na sikukubali kwa hiari," anaelezea mama mmoja, 50, mwenye watoto watatu. "Natamani kama ningeweza kusahau kilichonitokea, lakini haiwezekani. Unakuwa sawa na mtu aliyefariki dunia ilihali uko hai.

"Mimi ni sawa na mtu aliyefariki dunia kwasababu nafahamu fika kwamba ni mtu nisiye na maana yoyote."

Zishilo anaamini kuwa alifungwa kizazi bila ridhaa yake kwasababu alipatikana na ugonjwa wa ukimwi.

"Wote waliofungwa kizazi walikuwa weusi, wengi wao kutoka maeneo ya vijijini. Walilazimishwa kusaini fomu ya kukubali kufungwa kizazi." amesema daktari Mofokeng.

Chanzo cha picha, BBC News

Maelezo ya picha,

Zishilo Dludla, ambaye anaishi na virusi vya Ukimwi hakuridhia kufungwa kizazi baada ya kujifungua.

Hospitali ambayo Zishilo alifungwa kizazi inasema kuwa rekodi zilizopo zinaonesha kabla ya mama huyo kwenda kujifungua alikubali kufungwa kizazi wakati anafanyiwa upasuaji.

Taarifa zinasema kwamba hii ni kwasababu tayari awali, alikuwa amefanyiwa upasuaji mara mbili na ilikuwa kawaida kwa wanawake ambao wamepitia hilo kuchagua kufungwa kizazi baada ya kupata mtoto wa tatu kwasababu ya hatari za kiafya zinazoweza kujitokeza mtu anapofanyiwa upasuaji mara nyingi.

Walizungumza na BBC: "Wanawake hawalazimishwi… kuna baadhi ambao walikataa na matakwa yao yaliheshimiwa."

Madai ya wanawake wengi kama vile Zishilo yalichunguzwa na Tume ya Usawa wa Kijinsia Afrika Kusini mwaka jana. Lakini Daktari Mofokeng anasema tangu wakati huo ni hatua chache ambazo zimepigwa.

"Mfumo wa Afya Afrika Kusini pamoja na serikali kwa ujumla, zimefeli wanawake waliojumuishwa kwenye ripoti ya Tume hiyo.

"Idara yenyewe pia haijakubali mbele ya umma kuwa ukiukaji wa haki za binadamau ulitendeka."

Pia, idara ya Afya Afrika Kusini haijajibu ombi la BBC kuzungumza nayo juu ya suala hilo.

Hata hivyo, kote duniani suala la wanawake kufungwa kizazi halijaegemea tu kwa wale waliopata maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Kwa mfano, ripoti ya Afya kote duniani imeangazia visa vya wanawake wa Canada ambao wanasema walipewa shinikizo kufungwa kizazi kati ya mwaka 2005 na 2010.

Chanzo cha picha, Zuno Photography

Maelezo ya picha,

"Inachosha kihisia. Lakini hatuna namna zaidi ya kusaidiana. Mimi mwenyewe ni mwanamke. Ni mweusi ninatoka eneo la vijijini Afrika Kusini. Najua baadhi ya marika zangu ambao wamepitia kitendo hichi kibaya katika jamii yangu na pia hakuna utayari wa kuchukua hatua," Dr Mofokeng amesema.

Shinikizo sawa na hilo pia limeshuhudiwa na wanawake wa Roma katika Jamhuri ya Czech, Hungary na Slovakia dakika chache baada ya kujifungua.

Nchini Japan, watu wanaobadilisha jinsia ni lazima wafungwe kizazi ili kuwaruhusu kisheria kuishi maisha ambayo wenyewe wanayapendelea. Ikiwa hawatofanyiwa upasuaji, haki zao za msingi zitabinywa kama vile kuoa au kubadilisha jinsia zao katika nyaraka zao muhimu mfano, kwenye pasipoti.

Nchini India, taifa hilo linatoa ruzuku katika kodi, ajira na elimu kwa wale ambao familia zao sio zaidi ya watoto wawili kama njia moja ya kudhibiti idadi ya watu.

Ripoti hiyo pia inasema, watu ambao hawataweza kutoa vyeti kuonesha kuwa wamekatwa kizazi pia nao wamenyimwa vidonge vinavyoongeza viritubisho mwilini kwa watoto wao.

Dr Mofokeng amesema: "Inachosha kihisia. Lakini hatuna namna zaidi ya kusaidiana. Mimi mwenyewe ni mwanamke. Ni mweusi ninatoka eneo la vijijini Afrika Kusini. Najua baadhi ya marika zangu ambao wamepitia kitendo hichi kibaya katika jamii yangu na pia hakuna utayari wa kuchukua hatua," ameongeza.

"Kazi yangu mimi kama mjumbe wa Umoja wa Mataifa, ni kukumbusha mataifa haki za afya, yanajukumu la kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na ripoti hii, pia ni lazima wahusika wachukuliwe hatua za kisheria."