Kwanini Kardashian alijaribu kufuta picha yake mtandaoni?

Khloe Kardashian

Chanzo cha picha, Getty Images

Anatoka katika moja ya familia maarufu zaidi katika ulimwengu wa burudani na ni mara chache Khloe Kardashian amewahi kupigwa picha akiwa na muonekano ambao thamani yake kipesa ni chini ya mamilioni ya dola, yaani muonekano wa kawaida tu.

Nyota huyo wa televisheni na mwenye ushawishi katika mitandao ya kijamii na timu yake kwa kawaida huwa na utaalamu wa kuonesha picha nzuri hasa walizopigwa kwenye umma.

Na hivyo basi baada ya picha yake ya kawaida tu kusambazwa kwenye mtandao wake wa kijamii " kwa bahati mbaya" walifanya kila wanaloweza kuiondoa mtandaoni.

Wametaka majukwaa ya mitandao ya kijamii kuindoa picha hiyo, ingawa juhudi hizo zimechochea wengine kuisambaza hata zaidi.

Picha hiyo ya familia ina muonesha Khloe Kardashian, 36, akiwa amevaa bikini katika kidimbwi cha kuogelea.

Nyota huyo wa televisheni anaonekana akiwa hajapaka vipodozi: kama ambavyo unaweza kuona picha ya rafiki yako ambaye anaogolea wakati anatekeleza amri ya kutotoka nje na wala huwezi kuifananisha na picha za awali ambazo zimezoeleka za kina Kardashian.

Timu ya Kardashian imesema kuwa picha hiyo imekiuka hakimiliki yake.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Sisters Kim, Kourtney and Khloe Kardashian

"Khloe alipigwa picha hiyo wakati wa mkutano binafsi wa kifamilia na ikawekwa kwenye mtandao wa kijamii bila ridhaa yake kwa bahati mbaya na msaidizi," Tracy Romulus, amezungumza na Page Six.

"Khloe anaonekana mzuri lakini pia ni haki ya mmiliki kuondoa picha mtandaoni ambayo ilichapishwa kwa bahati mbaya."

Kulingana na mtandao wa Twitter, picha hiyo inategemea ilani ya kuondolewa mtandaoni ya Digital Millennium Copyright Act (DMCA).

"Kulingana na sera yetu ya haki miliki, tunajibu malalamiko halali ya haki miliki yaliyotumwa kwetu na mmiliki wa haki miliki au wawakilishi wake walioidhinishwa," msemaji wa mtandao wa Twitter amezungumza na BBC Jumatano.

Baadhi ya watumiaji walioiweka kwenye mitandao yao waliona imeondolewa na badala yake kuna ujumbe unaosema: "Picha hiyo imefutwa kama hatua iliyochukuliwa baada ya kupokea ripoti kutoka kwa mmiliki wa haki miliki."

Pia picha hiyo haikuwepo katika mtandao wa Reddit, kukiwa na ujumbe unaosema "Imeondolewa kama hatua ya kujibu madai ya mmiliki".

Lakini wengine bado waliendelea kuisambaza, huku mitandao ya vyombo vya habari ikiwemo Page Six pia ikiichapisha.

'Kuondolewa kwa picha hiyo kutavutia zaidi.'

Chanzo cha picha, Getty Images

Elizabeth Ward, mkuu wa mawakili wa hakimiliki Virtuoso Legal, amesema jaribio lolote la kuondoa picha hiyo itavutia nadhari zaidi.

"Cha kuvutia zaidi katika mtazamo wa kisheria, haisemi ni nani hasa aliyepiga picha hiyo - inasema tu yeye ndio mmiliki wa picha hiyo. Mmiliki wa kwanza wa haki miliki kawaida huwa ni mpiga picha, kwahiyo, kama mimi nimepiga picha ya Khloe Kardashian, mimi ndio mwenye haki miliki, na hivyo basi itakuwa haki yangu kufanya ninachotaka."

Akizungumza kama mama wa kijana huyo, Bi. Ward alisema kuwa "inasikitisha" hili limekuwa suala nyeti kwasababu ya kusambaa kwa picha mtandaoni ambazo zinaonekana "zimefanyiwa ukarabati" kwa namna moja au nyengine.

"Sio halisi, zote zimefanyiwa ukarabati, na msichana kijana yoyote yule utakayemuuliza, anajua," alisema. "Lakini ni jambo wanakabiliana nalo kila siku kwahiyo lazima linawaathiri - hiyo picha sio halisi, sio ya kweli."