Dereva wa treni ya mwendokasi hatarini kuadhibiwa kwa kwenda msalani wakati wa kazi

JR Tokai's Tokaido Shinkansen bullet trains stand at platforms at Tokyo station in Tokyo, Japan, 18 May 2015.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Tukio hilo limetokea Jumapili asubuhi wakati treni ilikuwa inaelekea mkoa wa Shizuoka.

Dereva wa treni ya mwendokasi maarufu kama Shinkansen anakabiliwa na uwezekano wa kuadhibiwa baada ya kuachia usukani wa treni aliyokuwa anaendesha kwa dakika kadhaa kwenda chooni.

Alimuomba kondakta wake ambaye hakuwa na leseni wala mafunzo kuendesha treni hiyo iliyokuwa inasafiri kwa mwendo kasi wa kilomita 150 kwa saa, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Japani.

Treni hiyo kwa jina Hikari 633 ilikuwa imebeba abiria 160 wakati huo.

Inasemekana kuwa tukio hilo halikuathiri safari lakini kampuni hiyo ya reli imeliripoti tukio hilo kwa mamlaka na kuomba radhi.

Kampuni ya reli ya Japani ya kati maarufu kama JR line, imesema tukio hilo limetokea Jumapili asubuhi wakati treni ilikuwa inaelekea mkoa wa Shizuoka.

Dereva huyo, mwenye miaka 36, ambaye hakutajwa jina, alikuwa anaumwa na tumbo na alitaka kwenda chooni haraka mno.

Alimuita kondakta wake katika chumba cha dereva na kuondoka kwa takriban dakika tatu akiwa chooni upande wa abiria, kampuni hiyo imesema.

Moja ya sheria ya kampuni hiyo inasema, ikiwa dereva anahisi kuumwa au hayuko sawa anastahili kuwasiliana na kituo cha usafiri. Pia wanaruhusiwa kumuomba kondakta kuchukua usukani lakini ikiwa tu kondakta ana leseni ya udereva.

Dereva na kondakta wake sasa wanakabiliana na uwezekano wa kuchukuliwa hatua ya nidhamu, kampuni ya reli ya JR imesema.

Afisa mwandamizi Masahiro Hayatsu amewaambia wanahabari kuwa: "Kilikuwa kitendo kisichostahili kabisa. Tunaomba msamaha."

Treni za Japani zinazosifika sana kwa ufanisi wake zinasimamiwa kwa kuzingatia kanuni kali za viwango vya juu na ajali za treni ni nadra sana nchini humo.

Ajali kubwa ya treni kutokea ilikuwa ni mwaka 2005 katika mji wa magharibi wa Amagasaki iliyosababisha vifo vya watu 107.

Treni ya Shinkansen, ambayo inamilikiwa na mtandao wa treni za mwendokasi nchini Japani haijawahi kusababisha ajali katika kipindi cha miaka 57 ya historia yake.