Mzozo wa Israeli na Wapalestina : Yahya Sinwar kiongozi wa Hamas anayepambana na Israeli ni nani?

Yahya Sinwar, Kiongozi wa Hamas mjini Gaza

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Yahya Sinwar, Kiongozi wa Hamas mjini Gaza

Kiongozi maarufu wa kikundi cha wapiganaji wa Kipalestina Hamas, Yahya Sinwar, amekuwa na nyadhifa za ngazi ya juu za jeshi na siasa katika vugu vugu la Hamas, na sasa ni kiongozi wa makao makuu ya kundi hilo mjini Gaza.

Yahya Sinwar, alizaliwa mwaka 1962 katika kambi ya wakimbizi ya Khan Yonis iliyopo Gaza.

Alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha jela cha miaka minne mwaka 1988, bada ya kupatikana na hatia ya kuunda kikundi cha al-Jihad w cha Da'wah, kikosi cha usalama wa ndani cha Hamas .

Wakati alipoanzisha tawi hili kulikuwa na harakati za kwanza dhidi ya Israeli.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Yahya Sinwar (kulia) aliunda kikundi ndani ya Hamas

Aliachiliwa kutoka gerezani mwaka 2011 wakati Israeli ilipokubali kutoa wafungwa wa Kipalestina gerezani ili ipewe mwanajeshi wake,Gilad Shalit.

Miaka miwili baada ya kuachiliwa kwake, alichaguliwa kuwa mkuu wa ofisi ya Hamas.

Mwaka 2015 Marekani iliongeza jina lake kwenye orodha ya magaidi wa kimataifa.

Mnamo mwaka 2017, alichaguliwa kama mkuu wa kikundi cha Hamas katika Gaza.

Kaka yake mdogo, Mohammed Sinwar, anayefahamika zaidi kwa jina la Abu-Ibrhaim, alikuwa kamanda wa Kikosi cha Hamas kinachoitwa Al-Qasam Brigade.

Mohamed anasemekana kuwa alishiriki katika kutekwa nyara kwa Gilad Shalit mwaka 2006.

Mohammed alinusurika majaribio kadhaa ya kumuua yaliyopangwa na jeshi la Israeli, kulingana na taarifa ya mtandao wa habari wa Gaza wa -Qudsnet 2015.

Ana shahada kutoka Chuo Kikuu na amebobea katika masuala lugha ya Kiarabu.

Matukio muhimu kumuhusu Yahya Sinwar:

  • 1987 - Alianzisha Al-Jihad wa Da'wah - "Majd" - kundi la Hamas, katika harakati za mwamko dhidi ya Israeli
  • 1988 - Alikamatwa na kufungwa kwa muda wa miaka minne gerezani
  • 18 Octoba, 2011 - Alikuwa mmoja wa Wapalestina 1,027 walioachiliwa na Israeli kama sharti la kuachiliwa kwamwanajeshi wa Israeli Gilad Shalit
  • Aprili, 2013 -Alikuwa mjumbe wa vuguvugu la kisiasa la Hamas
  • 2015, Septemba 8 - Wizara ya mambo ya nje ya Marekani iliongeza jina lake kwenye orodha ya magaidi wa kimataifa.
  • 2017, 13 Februari - Alichaguliwa kama mkuu wa ofisi ya siasa ya Hamas katika Ukanda wa Gaza.
  • 2017, 5 Septemba - Alikutana na mkuu wa shirika la msalaba mwekundu la Red Crescent, Peter Maurer.Alikataakuruhusu shirika hilo kukutana na wafungwa walioshikiliwa Israeli. Alizungumzia maafa yaliyosababishwa na Israeli katika Gaza na mashambulio iliyoyafanya tangu mwaka 2007.
  • 2020, 2 Aprili - Aliionya Israeli kwamba kama vifaa vya tiba ya virusi vya corona havitatumwa kwenye mwambao wa Gaza, Hamas itachukua vifaa hivyo kwa nguvu.
  • 2021, 10 Machi - Alichaguliwa tena kama kiongozi vuguvugu la kisiasa la Hamas mjini Gaza.

Je Hamas inayopigana na Israeli ni kundi gani?

Hamas ni kundi kubwa zaidi la waasi linapigana kwa ajili ya Wapalestina . Lilianzishwa mwaka 1987 na linafahamika pia kwa jina Harakatul Muqawwamah Al-Islamiyah- Jina lake kwa Kiarabu ambalo humaanisha Vuguvu la Kiislamu na Hamas imeazimia kuiangamiza Israeli.

Kundi la wapiganaji wa Hamas `ni mojawapo ya makundi kadhaa ya wapiganaji wa Kipalestina ambayo yanadhibiti ukanda wa Gaza, eneo ambalo mara kwa mara hulitumia kukabiliana na Israel, taifa ambalo halilitambui.

Ghasia mbaya zaidi zilizuka mwezi Mei 2021 huku mamia ya roketi yakirushwa kutoka Gaza kuelekea Israel kwa siku kadhaa huku Israel ikijibu mashambulizi hayo katika eneo hilo hatua ambayo imesababisha uharibifu huku ikiwacha makumi ya watu wakiwa wameuawa katika pande zote mbili.

Jina lake kwa Kiarabu humaanisha Vuguvu la Kiislamu na chanzo chake kilianzia siku za kwanza za Intifada au mapinduzi ya Palestina 1987 dhidi ya maeneo yanayokaliwa na Israel katika eneo la West Bank na ukanda wa Gaza.Hii leo kundi hilo ndilo kubwa la kiislamu miongoni mwa raia wa Palestina.

Shughuli zake za kisiasa

Tangu lilipoanzishwa, kundi hilo lina matawi mawili yenye malengo yasiofanana: Mojawapo, Kundi la wapiganaji wa Qassam, linalosimamia mapambano ya kivita dhidi ya Israel ambao uwepo wake haujatumbuliwa na Hamas, na upande mwengine kuna wingi ya kisiasa, ambayo lengo lake ni kujenga shule, hospitali na kuisaidia jamii katika masuala ya kisiasa na kidini.

Lakini tangu 2005, upande wa Kiislamu ulichukua mwelekeo tofauti, ikiwa ni kuwashirikisha kisiasa watu wa Palestina .

Mwaka 2006, Hamas lilichukua utawala baada ya kupata ushindi katika uchaguzi wa bunge la Palestina lakini ushindi wake haukudumu kwa muda mrefu.

Hofu ya kisiasa na kundi jingine la Fatah, ilipelekea kuingia katika mapambano ya kivita.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wanajeshi wa Israel wakijiandaa katika mpaka na Ukanda wa Gaza

Mwezi Juni 2007, makundi hayo mawili yalikabiliana katika vita vikali ndani ya ukanda wa Gaza kabla ya vita hivyo kukamilika huku Hamas likichukua utawala wa ukanda wa Gaza huku mpinzani wake wa kisiasa Fatah likitawala kutoka West Bank.

Kwa Marekani, Canada, Japan na Muungano wa Ulaya kundi hilo la Kiislamu ni kundi la kigaidi kutokana na historia yake ya mashambulizi dhidi ya Israel na lengo lake la kutaka kuliangamizia taifa hilo kitu ambacho imeandika katika sheria yake.

Lakini kwa wafuasi wake ni vuguvugu halali la kupigania haki za Wapalestina.